Habari za Punde

Serikali ya Awamu ya Nane Itaendelea Kuwaenzi Kuwatunza na Kuwajali Wazee Inathamini Juhudi Kubwa Walizozifanya.

 

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Wazee wa Nyumba za Wazee Sebleni alipofika kuwatembelea na kutowa mkono wa Eid El Fitry. na kuwasilisha Salamu za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi.

MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kuwaenzi na kuwatunza wazee wa nyumba za Sebleni na Welezo pamoja na watoto wanaolelewa katika nyumba za SOS na Mazizini.

Mama Mariam Mwinyi aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti wakati alipowatembelea na kuwapa mkono wa Idd el Fitri wazee wa nyumba za Sebleni na Welezo pamoja na watoto wanaolelewa nyumba za SOS pamoja na Mazizini.

Akitoa salamau zake kwa wazee wa Sebleni, Mama Maria Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kuwaezi, kuwatunza na kuwajali wazee kwani inathamini juhudi kubwa walizozifanya.

Alisema kuwa ibada ya Swaumu ya Ramadhani imefanyika kwa salama na amani na kuwawezesha waumini kufunga na kufanya ibada mbali mbali za sunna na faradhi, hivyo alisisitiza haja ya kuidumisha na kuilinda tunu ya amani.

Mama Maria Mwinyi alitumia fusra hiyo kutoa salamu za Idd el Fitri kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi za kuwatakia sikukuu njema wazee na watoto wote.

Akiwa katika nyumba za wazee Welezo, Mama Mariam Mwinyi ambaye alifuatana na Watoto wake, aliwaeleza wazee hao kwamba ametimiza ahadi aliyowaahidi wakati alipokwenda kuwapa futari wakati wa mwezi wa Ramadhani kwamba atakwenda kuwapa mkono wa sikukuu ya Idd el Fitr pale itakapowadia.

Katika maelezo yake, Mama Mariam Mwinyi alieleza jinsi alivyofarajika kwa kukutana nao tena wazee hao kwa mara ya pili na kuwataka kuendelea kuwaombea dua viongozi wao pamoja na kuiombea dua nchi yao.

Nao wazee hao wanaoishi nyumba za Sebleni na Welezo walionesha furaha kubwa na bashasha kwa kutembelewa na Mama Maria Mwinyi na kumpongeza kwa ukarimu wake huo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Abeda Rashid Abdalla, alitoa shukurani kwa Mama Maria Mwinyi kwa kitendo chake hicho cha kiungwana cha kuwatembelea wazee na kuwapa mkono wa Idd el Fitri.

Wakati huo huo, Mama Mariam Mwinyi aliwatembelea Watoto wa Nyumba za SOS Mombasa Jijini Zanzibar na kueleza jinsi alivyofarajika kwa kukutana nao katika siku hii adhimu ya sikukuu ya Idd el Fitri pamoja na mapokezi mazuri waliyompa hali ambayo imeonesha upendo mkubwa kwake.

Alieleza matumaini yake kwamba watoto hao wataendelea kuwa ni watoto wema huku akitoa shukurani kwa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi kwa kutoa baraka zake na kuwa muwasisi wa kuanzishwa kwa kituo hicho wakati akiwa Rais wa Zanzibar.

Mama Mariam Mwinyi pia, alikubali na kupokea ombi la kuwa Balozi wa kutetea udhalilishaji wa watoto kwani anatambua janga hilo linavyoiathiri jamii na kueleza hatua za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ya kuanzisha Mahakama maalum ya Udhalilishaji ambayo itakuwa muwarubaini wake.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini kuhakikisha usalama unaimarishwa zaidi kwa watoto pamoja na wananchi wote.

Pia, alitoa tahadhari kwa madereva kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria zote za usalama barabarani ili kuepuka kuleta athari kwa watoto hasa katika kipindi hichi cha kusherehekea sikukuu ya Idd el Fitri.

Nae Mkurugenzi wa SOS  Bi Asha Salim Ali alitoa shukurani kwa Mama Mariam Mwinyi kwa hatua yake hiyo ya kwenda kuwatembelea watoto hao katika kijiji chao hicho kilichoasisiwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi na kuzinduliwa mwaka 1989.

Katika maelezo yake Mkurugenzi huyo alieleza historia ya kijiji hicho pamoja na kueleza shughuli zinazofanyika katika kijiji hicho ambacho watoto wote wanaishi kama familia moja huku akitumia fursa hiyo kueleza kadhia ya udhalilishaji wa watoto katika jamii na kumtaka Mama Mariam Mwinyi kuwa Balozi wa kutetea udhalilishaji  wa watoto.

Mama Mariam Mwinyi alimaliza ziara yake hiyo kwa kuwatembelea na kuwapa mkono wa Idd el Fitri watoto wanaolelewa katika nyumba ya Mazizini Jijini Zanzibar na kuwaeleza kwamba Serikali iko pamoja na wao na itaendelea kuwalinda na kuwaenzi.

Sambamba na hayo, Mama Mariam Mwinyi aliwataka watoto wa nyumba hiyo kuendelea kuyafanyia kazi mafunzo yote waliyoyapata katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani uliomaliza.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi alieleza madhumuni hasa ya kwenda kuwatembelea wazee pamoja na watoto akiwa amefuatana na watoto wake katika siku hii adhimu ya Idd el Fitri huku akitoa salamu za skukuu ya Idd el Fitri kwa watoto hao kutoka kwa  Rais Dk. Hussein Mwinyi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.