Habari za Punde

LUGHA YA KISWAHILI KUWA BIDHAA YA KIMATAIFA

Na Mwandishi Wetu

Serikali imeanzisha mipango wa kimkakati ya kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa ya Kimataifa ambapo tayari kuna wataalam wa Kiswahili wataalam 1318 ambao wamesajaliwa na tayari vifaa vya kisasa vya mafunzo ya ukalimani kwa vitendo na matumizi ya TEHAMA katika ukuzaji wa Kiswahili vimenunuliwa na vimegharimu kiasi cha zaidi ya Sh. mil.181.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amesema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima Mbunge wa Singida-Mjini alilouliza Je? Serikali ina mpango gani wa kuifanya Lugha ya Kiswahili kuwa bidhaa ya kimataifa ili kuendeleza na kukuza utamaduni wetu duniani?

“Tayari tunao mpango wa kufundisha Kiswahili kwa wageni kupitia Balozi zetu nje ya nchi na Serikali imeboresha na kuimarisha mafunzo ya stadi za kufundisha Kiswahili kwa wageni pamoja na kutoa machapisho ya Kiswahili Rahisi kwa wataalam wetu” amesema Naibu Waziri Gekul.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kusaidia nchi zilizoonesha nia ya kuingiza Kiswahili katika mitaala yao ya Elimu ikiwemo Afrika Kusini, Namibia, Rwanda na Uganda.

Naibu Waziri amesisitiza kuwa mwaka 2019 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Serikali ilifanikiwa kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha nne rasmi zinazotumiwa wakati wa vikao na mikutano ya Jumuiya hiyo.

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Sima kuhusu ongezeko la msamiati wa Kiswahili, Naibu Waziri amesema Serikali kupitia Baraza la Kiwahili la Taifa (BAKITA) imekuwa makini panapokuwa na mabadiliko yeyote ya kimazingira, kieneo au matukio yoyote, BAKITA wamekuwa wakitafuta misamiati mbalimbali na kuisanifisha misamiati hiyo.

Aidha, Naibu Waziri ametoa rai kwa Watanzania kutumia lugha ya Kiswahili ikizingatiwa dunia na nchi yetu mfano ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Korona (COVID-19), BAKITA tayari wamesanifisha jina hilo na kwa Kiswahili ugonjwa huo unaitwa UVIKO 19.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.