Habari za Punde

MHANDISI HAMAD MASAUNI: VIJANA WAANZA KUCHANGAMKIA KILIMO NCHINI

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Fedha, Uchumi, Mipango ya Maendeleo na Mtangamano wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao, jijini Dodoma.

Na. Benny Mwaipaja, Dodoma

KUKUA kwa Sekta ya Viwanda na upatikanaji wa masoko ya bidhaa za kilimo nchini kumetajwa kuwa chanzo cha vijana wengi kuanza kujihusisha na kilimo.

Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yusuff Masauni wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Fedha, Uchumi, Mipango na Maendeleo na Mtangamano wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya Mtandao.

Mheshimiwa Masauni amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, viwanda mbalimbali vikiwemo vya kuchakata mazao ya kilimo vipatavyo 8,477 vimejengwa na kuchangia kutoa ajira kwa makundi mbalimbali wakiwemo vijana.

 “Vijana wengi hivi sasa wanajihusisha na kilimo biashara na shughuli nyingine za ujasiriamali kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa za kilimo, pamoja na kupambana na ukosefu wa ajira ambapo maeneo mengi yanayowavutia vijana ni kuongeza mnyororo wa thamani katika ufugaji wa kuku, kilimo cha mbogamboga na matunda, ufugaji, uvuvi na kilimo cha mazao ya misitu” alisema Mhe. Masauni

Alisema kuwa takwimu zilizopo hivi sasa zinaonesha kuwa vijana wanaojihusisha na kilimocha kuongeza thamani ya mazao imeongezeka kutoka milioni 7.2 (milioni saba nukta mbili) mwaka 2014 hadi kufikia milioni 8.1 mwaka 2020 sawa na ongezeko la zaidi ya vijana 900.

Mhe. Masauni alisema kuwa Vijana walioajiriwa katika sekta ya kilimo na kulipwa mishahara imeongezeka kutoka 171,841 mwaka 2014 hadi kufikia vijana 191,439 mnamo mwaka 2020 huku vijana wanaojihusisha na kuongeza mnyororo wa thamani katika kilimo walifikia milioni 2.3 kutoka vijana milioni 2.1 mwaka 2014.

Alibainisha kuwa hatua hiyo imefanya idadi ya vijana wanaojihusisha na kilimo ikiwafanya vijana wanaojihusha na kilimo kuongeza uzalishaji kwa asilimia 11.4 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015 hadi 2020).

Aidha, Mhe. Masauni kwa ujumla Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya kilimo kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji, uvuvi na mifugo, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima ambapo kupitia Benki ya Kilimo zaidi ya shilingi bilioni 22 zimekopeshwa.

 

Katika Mkutano huo, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika  wamekubaliana kuongeza  uwekezaji katika kilimo pamoja na kuvutia zaidi sekta binafsi kuwekeza katika kilimo, ujenzi wa viwanda na ukuzaji wa mitaji ili vichangie katika ukuaji wa uchumi.

 

Wajumbe wa Mkutano huo wamekubaliana kuwa mapinduzi ya viwanda hayawezi kufikiwa kikamilifu kwa nchi wanachama bila kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa barani Afrika na kwamba kupitia uwekezaji wa sekta binafsi na ukuaji wa matumizi ya teknolojia za kisasa zitalifanya bara hilo kusonga mbele kiuchumi na kuondoa changamoto za umasikini za watu wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.