Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kumuomba Mwenyenzi Mungu Kuzindisha Amani Nchini.

Waumini wa Dini ya Kiislamu wakisikiliza Hutba ya Swala ya Ijumaa Iliyotolewa leo na Khatibu, Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume katika Masjid Jamiu Zinjibar,Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) pamoja na waumini wa dini ya kiislamu wakiitikia dua iliyoombwa na   Mufti Mkuu Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi (wa  pili kushoto) mara baada ya swala ya Ijumaa   katika Masjid Jamiu Zinjibar,Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo (kulia) Mkuu wa Mkoa Mjni Magharibi Mhe.Idrissa Kitwana Mustafa. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akisisitiza jambo alipofuatana  na Katibu wa Mufti Mkuu Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume (kushoto) mara baada ya swala ya Ijumaa pamoja na  Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Masjid Jamiu Zinjibar,Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo (kulia) Mkuu wa Mkoa Mjni Magharibi Mhe.Idrissa Kitwana Mustafa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo alipokuwa akitoa agizo kwa Katibu wa Mufti Mkuu Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume mara baada ya swala ya Ijumaa pamoja na  Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Masjid Jamiu Zinjibar,Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo.

JAMII nchini imetakiwa kuitunza na kuielendeleza amani iliyopo na kuwaombea dua viongozi wa Taifa hili ili waweze kuongoza na kuiletea nchi maendeleo endelevuyenye kheri na tija.

Akitoa neno la shukurani kwaniaba ya waumini wa Masjid Jamiu Zinjibar, Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi, mara baada ya sala ya Ijumaa Mkurugenzi wa msikiti huo Sheikh Shaaban Batwash alisema kuwa ni vyema kwa waumini na wananchi wote nchini wakawaunga mkono viongozi wao wa nchi katika kuiendeleza na kuisimamia amani.

Katika sala hiyo ya Ijumaa ambapo Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alijumuika pamoja na waumini wa msikiti huo, Mkurugenzi huyo wa Masjid Jamiu Zinjibar alisema kuwa uwepo wa amani ni amri ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake hivyo, kuna kila sababu ya kuidumisha.

Alisisitiza haja ya kumuomba MwenyeziMungu kuzidisha amani iliyopo nchini na kueleza kuwa viongozi waliopo nchini wamekuwa wakifundisha na kuhimiza amani.

Aidha, alieleza kwamba jamii wana wajibu wa kuitunza amani na kuwaombea viongozi ili wawaongoze zaidi kwa hekima na busara huku wakimuombea dua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan katika kutimiza siku zake mia za uongozi.

Pia, alimuombea kwa Mwenyezi Mungu kumpa wepesi Rais wa Zanzibar na Menyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Mwinyi katika kuyatimiza yale yote yenye kheri na manufaa kwa wananchi wa Zanzibar.

Akitoa hotuba ya sala ya Ijumaa msikitini hapo, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume alisema kuwa kuwepo kwa amani kunapelekea kuimarika kwa uchumi.

Alisema kuwa mafungamano ya amani na uchumi ni makubwa sana kwani maendeleo hayawezi kupatikana kama hakuna amani hivyo, ni vyema kuiendeleza na kuitunza neema hiyo ili isije ikaondoka.

Alisema kuwa amani, usalama na utulivu ni maisha ya viumbe vyote walioumbwa na Mwenyezi Mungu wakiwemo binaadamu na hata wanyama nao pia, huhitaji amani.

Hivyo, Sheikh Khalid Ali Mfaume alisema kuwa kiongozi mzuri ni yule anayehimiza amani, umoja na mshikamano kwa wale anao waongoza.

“Tusizungumze amani kila siku bali tuzungumze amani kila dakika kwani amani ndio maisha yetu, amani ndio maendeleo yetu, amani ndio mustakabali wetu kwani huwezi kulima, kusoma bila ya kuwepo kwa amani....basi kwa msingi huo asitokee mtu akaiharibu amani kwani ataharibu amani....mshairi anasema uhifadhi ulimi wako mwanaadamu kwa sababu ulimi ni nyoka mwenye sumu sana...kunyamaza ni salama...kwani sio kila kitu unasema”,alisisitiza Sheikh Khalid.

Aidha, Khalid pia, aliitaka jamii kushirikiana katika kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya pamoja na aina zote za vilevi kwani matumizi yake hupelekea kuondoka kwa amani hasa kwa vijana.

Alieleza kwamba iwapo vijana watajihusisha na matumizi ya dawa za kulevya watapelekea kudhorotesha uchumi pamoja na amani iliyopo kuanzia ngazi ya familia, jamii hadi Taifa.

Sambamba na hayo, Sheikh Khalid aliitumia fursa hiyo kueleza kwamba matumizi ya dawa za kulevya na vilevi vyengine huharibu uchumi kwani baadhi ya watumiaji huingia kwenye wizi ambapo hivi sasa hali hiyo imejitokeza hata vijijini ambapo kumeibuka wizi wa mifugo na mazao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.