Habari za Punde

Kiongozi wa Uamsho kutoka Zanzibar aiomba Serikali kuchunguza kwa haraka Kesi za Wananchi wanaopelekwa rumande


 Na Hamida Kamchalla, TANGA.


SERIKALI nchini imeombwa kuharakisha kufanya upelelezi wa kesi za watuhumiwa pindi wanapofikishwa mahakamani kutokana na kuwepo kwa kesi nyingi za kubambikiwa huku wananchi wakiendelea kuteseka magerezani

Rai imetolewa jana kwenye Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) nchini na Kiongozi wa Uamsho wa Zanzibar Shekhe Farid Mussa ambapo  alisema kipindi alichokaa gerezani amejifunza na kuona mengi ambayo yanaumiza na kukatisha tamaa hasa kwa wale wanaobambikiwa kesi ambazo hawajahusika nazo.

Shekhe Mussa alisema kwenye kesi yao walikuwa watu mia mbili na ishirini lakini wametoka thelathini na nne na wenzao waliobaki wapo ambao wanaendelea kupata mateso ya kesi ambazo haziwahusu na kutolea mfano wa mzee wa miaka tisini na sita ambaye alikamatwa kwa niaba ya watoto wake waliotoroka.

"Kwahiyo Muheshimiwa kesi za kubambikwa ziko nyingi sana, tunaomba kesi za watuhumiwa zifanyiwe uchunguzi kwa haraka sana, siku moja tu inauma katika jela achiliambali miaka, muheshimiwa wewe ni muumini wa dini ya Kikristu, maandiko yanasema hivi, Isaya moja, kumi na sita kumi na saba, jiosheni, jitakasheni, ondoeni matendo yenu ya uovu usiwe mbele ya macho yangu, acheni kutenda mabaya jifunzeni kutenda mema, takeni hukumu na haki, wasaidieni walioonewa" alisema Shekhe Mussa.

"Muheshimiwa watu wameonewa, mpatieni yatima haki yake, watu wamewekwa ndani wameacha watoto wao kama mayatima wanalia, mteteeni mjane, muheshimiwa sisi tumewekwa ndani tumewaacha wake zetu kama wajane mwanamke unamuacha miaka saba miaka nane yupo tu anajizuia na anavumilia, tuwaombee dua sana, inauma sana" aliongeza.

Aidha Shekhe Mussa alitoa mifano kadhaa ya vitabu vya dini na kusema kuwa mbali na kufunza mema lakini pia imekatazwa kwa mwenye mamlaka kutenda jambo ambalo litamnyima haki mwengine na kuongeza kuwa hata Waandishi wanaoandika maneno ya kupotosha nao husababisha haki ya muhitaji kupotea.

"Lakini Biblia pia inaonya ikisema, ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu ili kumpotosha muhitaji asipate haki yake, na hicho ndicho kilichojiri kwa muda ule, wamepotosha watu maandiko, sisi tumezungumzia mchakato wa Katiba na kutoa maoni yetu kwa mujibu wa taratibu za kisheria na Bunge likaupitisha, lakini maoni yetu hayakuwapendeza wengi tukaonekana tunataka kuvunja Muungano, kutaja matatizo ya Muungano ni kwamba unaupenda na unauthamini ili uboreshwe na uwe safi lakini haikuwafurahisha hayo na baadae kilichotokea hapo wapeni kesi ya ugaidi ya mauaji wakae ndani" aliongeza.

Hata hivyo Shekhe huyo aliiomba Serikali endapo atapatiwa nafasi ya kuongea anao ushauri wa kujenga amani ambapo pia alidai ataeleza mengi ambayo yanahitaji muda wa kusikilizwa kwakua alichojifunza akiwa gerezani ni kutumia fursa kwa muda muafaka.

Kwa upande wake Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango alimuhakikishia Shekhe Mussa na Watanzania kwa ujumla kuwa muda wowote Ofisi ya Rais iko wazi kupokea ushauri na wako tayari kushirikiana na wananchi ili kujenga Taifa lililo bora.

Dkt. Mpango alieleza kuwa moja ya majukumu ya viongozi wa dini ni kuwaelekeza waumini wao kiroho na kijamii na hasa kuwahimiza wamche Mola wao, hivyo pamoja na huduma za kuwaelimisha kiroho zipo pia huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi za kidini kwa ajili ya maendeleo ya jamii ya Kitanzania.

"Naomba nitambue mchango mkubwa unaotolewa na BAKWATA katika shuhuli mbalimbali za kijamii katika nchi yetu mijini na vijijini, nafahamu pia mnayo miradi mbalimbali ya kijamii mnayoisimamia na hasa kwa upande wa sekta ya Afya, najua mna Vituo takribani kumi na nane, Zahanati tisini na tisa" alissma.

"Kwa upande wa Elimu serikali inafahamu zipo shule za awali kumi na tano, shule za msingi thelathini na mbili, sekondari mia moja sabini na tano, shule za kidato cha tano na sita thelathini na tano, vyuo vya kati vinne, vyuo vya ufundi sita pia kuna chuo kikuu kimoja ĺakini bila kusahau madrasa kwa ajili ya elimu ya dini, lakini tukija kwa wa maji mna visima visivyopungua elfu moja pamoja na vituo vya kutunzia na wale wanaotoka kwenye mazingira magumu" aliongeza.

Hata hivyo alitoa pongezi kwa Baraza hilo na kuongeza kuwa Watanzania wengi wamenufaika na wanaendelea kunufaika na huduma zinazotolewa na BAKWATA , serikali inawashukuru sana kwa mchango huo mkubwa na kuliomba liendelee kuwahudumia wananchi hasa wale wa kipato cha chini bila ubaguzi, huku akilihakikishia kwamba serikali inathamini sana mchango unaotolewa na BAKWATA, hakika inaendelea kuwa mdau muhimu na mshirika mzuri wa serikali katika kuwahudumia wananchi tangu ilipoanzishwa mwaka 1968

"Ipo mifano mingi tu ambapo unakuta nikiitaja iko maeneo ambayo hata serikali haijafika lakini ninyi mmeweza kufikisha huduma hizo sehemu hizo na juhudi hizo za kuunga mkono serikali zimechangia nchi yetu kupiga hatua kubwa katika kusogeza huduma kwa jamii karibu zaidi na wananchi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.