Mke wa Makamu wa Kwanza Wa Rais wa Zanzibar, Bi. Zuhra Kassim Ali, amesema Serikali imejipanga kuwahudumia wananchi wote na hasa wajasiriamali wanawake, kwa kutatua kero zao kwa haraka ili kuendelea kuweka mazingira bora ya kutekeleza shughuli zao za kiuchumi.
Bi.Zuhra ameyasema hayo katika Mahafali ya mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake yaliyoendeshwa kwa njia ya mtandao yaliyofanyika katika ukumbi wa wakfu ya Wangazija Forodhani jitini, ambayo yalioandaliwa na taasisi ya wanawake wajasiriamali (AWE) kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani.
"Serikali inaendelea kusimamia jambo hili kwa karibu ili kuhakikisha wajasiriamali wote wanapata mazingira mazuri kwa ajili ya kufanya shughuli zao za ujasiriamali".Hivyo Bi.Zuhra aliwataka Wanawake hao kuitumia vyema fursa na elimu waliyoipata katika mafunzo hayo ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi.
"Nawaomba sana wahitimu, kufanya kazi kwa mashirikiano baada ya kupata mafunzo haya na kuwaelimisha wajasiriamali wengine waliokosa fursa hii, ili kusaidia kuboresha biashara zao, kupambana na changamoto ya ajira pamoja na kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla" alinasihi Mke huyo wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Muwakilishi wa Balozi wa marekani nchini Tanzania Bi. Amy Hart Vrampas, amesema lengo la mradi huo ni kuona wanawake wanakuwa chanzo kikubwa cha maendeleo kwa kuwapatia ujuzi wa kujiwezesha kujipatia kipato cha kila siku.
Akisoma risala fupi iliyoandaliwa na wanafunzi waliomaliza mafunzo hayo Ndg. Mwanaidi Said, wameiomba Serikali kuunga mkono jitihada hizo ili waweze kunyanyuka kiuchumi pamoja na kuwapatia fursa mbali mbali za kimaendeleo.
Katika hafla hiyo wanafunzi kumi na saba (17) wametunikiwa vyeti kwa kuhitimu mafunzo hayo yalioanza mwezi wa kwanza hadi wa sita mwaka 2021 ikiwa ni mara ya kwanza kwa taasisi ya AWE kutoa mafunzo hayo hapa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment