Habari za Punde

UAE watia nia kuisaidia Zanzibar

Mkurugenzi Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Dkt. Msafiri Marijani (alievaa koti) akiwatembeza maafisa kutoka Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii ya Abu Dhabi wakiwa na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu Nchini Tanzania Bw. Khalifa Almarzouqi (kulia) kwa malengo ya kuisaidia Serikali ya Zanzibar katika sekta ya afya na maendeleo ya jamii.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dkt. Omar Dadi Shajak (wa saba toka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na maafisa mbalimbali kutoka Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii ya Nchini Abu Dhabi wakiongozwa na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu Nchini Tanzania Khalifa Almarzouqi walipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja.

Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Nchini Tanzania Khalifa Almarzouqi wa pili kushoto na ugeni wake akiwasalimiana wanafunzi wa Skuli ya Mtopepo walipofika kujionea changamoto zinazowakabili skulini hapo.

Picha na Makame Mshenga.

Na Issa Mzee    Maelezo   28/06/2021

Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dkt. Omar Dadi Shajak amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kushirikiana na wahisani wa maendeleo katika kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma bora za afya nchini.

Akizungumza na Balozi wa Umoja wa falme za Kiarabu nchini Tanzania Bw.Khalifa Almarzouqi wakati alipotembela hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja amesema Nchi za kiarabu ni miongoni mwa wadau wakubwa wa maendeleo hasa katika sekta ya afya Zanzibar.

Katibu huyo alieleza lengo kuu la ziara ya balozi huyo ambae ameambatana na maafisa mbalimbali kutoka Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii kutoka nchini Abuu Dhabi ni kuona upatikanaji wa huduma za afya na kutafuta namna ya kuisaidia Serikali ili iweze kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.

“Serikali pekee haiwezi kukamilisha huduma zote kwa wakati mmoja hivyo wamekuja kutizama ili kuona namna ya kuisaidia serikali kadri ya uwezo wao katika maendeleo ya jamii na sekta ya afya”,  alisema Katibu Mkuu.

Katika ziara hiyo pia wageni hao walipata fursa ya kutembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya katika kijiji cha Mbuzini ambapo Katibu Mkuu alifafanuwa kuwa katika eneo hilo inatarajiwa kujengwa hospitali ili kupunguza msongamano katika hospitali ya Mnazi Mmoja.

Aidha Katibu Mkuu alisema mara tu baada ya ziara hiyo maafisa hao wanatarajia kupeleka ripoti  na kujadili namna bora ya kuisaidia Zanzibar katika sekta ya afya.

Wakati huohuo Katibu Mkuu alimsimamisha kazi Afisa Tabibu Msaidizi wa kituo cha Wazee Welezo Bwana Seif Hamad Suleiman kwa kosa la kulewa wakati wa kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.