Habari za Punde

Taasisi ya Friends of Mwinyi Kufanya Kongamano la Kuelekea Siku Mia za Uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
TAASISI ya Friends of Mwinyi imesema inatarajia kufanya kongamano la kuelekea siku 100 za uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambapo litafanyika 4 Julai mwaka huu katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Wakili.

Imesema katika kongamano hilo kunatarajiwa kujadiliwa mada kuu nne ikiwemo kuhusu uzoefu wake katika nafasi za uongozi alivyokuwa kwenye serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja alipokuwa nafasi za chama.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Katibu wa Taasisi ya Friends of Mwinyi Fatuma Suleiman Sarhan alisema pamoja na mambo hayo washiriki wa kongamano hilo watapata fursa ya kujadili mambo makubwa ambayo Rais Samia aliyoweza kuyafanya katika siku 100 za uongozi wake.
 
Katibu huyo alisema katika kuelekea siku hizo kwa upande wa taasisi hiyo inatafsiri siku hizo ni kuwa Rais Samia ana uwezo mkubwa wa kufanya mambo mbalimbali ambayo yatasaidia Tanzania kufika azma iliyokusudiwa.

Fatuma alisema katika kuelekea siku hizo 100 Rais Samia ameonyesha uwezo wake wa kukutana na makundi mbalimbali ambayo ya lika tofauti ikiwemo vijana wanawake na wazee na kwamba katika suala hilo anaonyesha dhamira yake ya kutaka usawa 50 kwa 50 na usawa wa jinsia zote.

"Katika suala hili la usawa Rais Samia ameonyesha kuwa katika serikali anayoiongoza anataka kuhakikisha makundi ya lika zote wakiwemo wanawake, wazee na vijana wanashirikishwa ili kufikia usawa ambao yeye anaona una umuhimu ndani ya uongozi wake,"alisema

Alisema katika kuelekea siku 100 za uongozi wake Rais Samia ameonyesha kuendeleza masuala ya ushirikiano wa kimataifa na kikanda na kwamba bado inaonyesha mahusiano ya Tanzania na nchi jirani kuwa ni mazuri.

"Lakini pia tumeona katika kuelekea siku 100 hizo Rais Samia amehakikisha anayaendeleza na kuyakamilisha mambo ambayo yaliachwa na Hayati Rais Dk.John Pombe Magufuli hivyo tumeona dira yake katika kipindi hiki cha kuelekea siku hizo,"alisema

Alisema kabla ya kufanyika kwa kongamano hilo kutakuwepo na dua maalum ya kumuombea Rais Samia awe na nguvu pamoja na afya njema pamoja na kukingwa na jambo baya dhidi yake."Kabla ya kongamano hilo litaanza kufanyika bonanza la michezo mbalimbali.

Pia kwa upande wa bonanza tunatarajia kuwepo kwa kukimbia ambapo itaanza uwanja wa maisara kupitia madema Kisonge,Raha Leo,Darajani,Mnazi Mmoja na kumalizia Maisara na baada ya hapo kutakuwepo na mashindano ya mbio za baiskeli tumeshirikiana na chama cha baiskeli Zanzibar(CHABAZA) ambapo yataanzia Maisara na kuelekea Fumba kupitia njia ya Mazizini na wakati wa kurudi tutapitia njia ya Amani,"alisema

Alisema mbio hizo za baiskeli anatarajiwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid na atagawa zawadi kwa mshindi wa kwanza atakabidhiwa sh.300000,mshindi wa pili atakabidhiwa sh.200000 na mshindi wa tatu atakabidhiwa sh.100,000.

Pia,alisema baada ya mashindano hayo kutakuwepo na mechi kati ya Mbolibolini FC dhidi ya Kajengwa FC ambapo mgeni rasmi katika mechi hiyo anatarajia kuwa mume wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hafidh Ameir utakaonza saa 10 jioni.

"Mshindi wa mechi hiyo atakibidhiwa kikombe,jozi moja ya jezi,mpira mmoja wa miguu na sh.milioni moja na wa pili atapata sh.500,000 pamoja na jozi moja ya jezi na mpira wa miguu,"alisema  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.