Habari za Punde

Ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Wilaya ya Kaskazini Unguja. Viongozi wa CCM Watakiwa Kukagua Miradi ya Maendeleo.

VIONGOZI na watendaji wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wametakiwa kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi wa maeneo husika.

Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Amesema endapo viongozi hao wa Chama kwa ngazi mbalimbali watakagua miradi inayotekelezwa na serikali itakuwa ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo maelekezo yaliyotolewa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.

Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kutoridhishwa na maelezo yaliotolewa na Meneja wa mradi wa ujenzi wa gati ya bandari ya Mkokotoni.

Amesema maelezo yaliotolewa na Meneja huyo hayafanani na maelezo aliopatiwa na Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla wakati alipofanya ziara yake ya kukagua ujenzi huo wa gati hiyo uliopo mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema maelezo yaliotolewa na Meneja huyo Jafar Majilanga ni kinyume na maagizo aliyotolewa kwa Makamu wa Pili wa Rais ambapo ujenzi huo ulitakiwa kuongezwa gati ya bandari hiyo mita 120.

Alieleza kuwa maelezo aliyopewa Makamu huyo wa Pili wa Rais wamekubaliana kuchimba kuongeza kina cha maji cha bahari kwakufikia mita 120 hata hivyo hadi sasa tayari wamefikia mita 70 na anatarajia kuongeza mita 30 ili wachimbe kwa lengo la kufikia mita 100 ndipo waanze kazi ya kuchimba.

 

Naibu alisema maelezo aliyopewa ni kinyume na maelezo aliyopewa Makamu huyo wa Rais na kwamba anataka suala hilo kuwa la wazi bila ya kuwepo kwa maelezo mawili tofauti na kwamba kwa mujibu wa maelezo yake hatua hiyo inafikia baada ya kufanya utafiti kuona kuwa hata mita 100 ifikia inawezekana kuchimbwa na si lazima hadi ifikie mita 120. 

"Maelezo yake ya Meneja yanatuchanganya kutokana na kuwa alipokuja Makamu wa Pili wa Rais aliambiwa gati hiyo itaongezwa mita hizo lakini hapa anatuambia wana angalia uwezekano wa kuchimba ili kuongeza kina cha maji sasa CCM inataka watueleze ukweli maelezo haya na tujionee wenyewe,"alisema Naibu Katibu Mkuu huyo    

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema CCM imedhamiria kutekeleza kwa vitendo ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kasi ya aina yake na kwamba amewataka wanachama wa CCM kutolaza damu na badala yake wajue kuwa muda huu ndio muda wa kushuka chini kwa wananchi kusimamia utekelezaji huo wa ilani.

Wakati huo huo Naibu Katibu Mkuu huyo alipotembelea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji wa kilimo cha mpunga bonde la Kibokwa aliwataka wakulima wa kilimo cha mpunga kutambua kuwa CCM itawanufaisha kupitia sera,ilani ya uchaguzi ya CCM.

Alisema CCM imeazimia kujikita katika kutekeleza miradi yote ambayo ipo kwenye ilani ya uchaguzi ikiwemo mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji wa kilimo cha mpunga katika wilaya hiyo ya Kaskazini 'A' na kwamba CCM haitaki kupotezwa malengo hivyo hakuna muda wa kulala kazi zitaendelea.

"CCM inataka kuwanufaisha wanzanzibar hasa wakulima hawa wa mabonde ya mpunga na  kwamba imesikia suala la ugawaji wa pembejeo hivyo tushaanza kulifuatilia serikalini kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo kuhakikisha wanagawa pembejeo hizo kuwafikia wakulima hawa wa kilimo cha mpunga kwa wakati,"alisema

Kwa upande wake Meneja Meneja wa mradi wa ujenzi wa bandari ya Mkokotoni Jafar Majilanga alisema mradi huo unatarajiwa kugharimu sh.bilioni 6.4 huku sh.bilioni 2.2 tayarizishatumika.

Alisema mradi huo ulianza Juni 8 mwaka huu na unatarajiwa kumalizika Septemba 21 mwaka huu huku ukikamilika kwa asilimia 50 na katika ujenzi huo wa gati katika bandari hiyo ni rasilimali zinazotumika kwenye mradi ni mawe na nondo.   

"Tumekubaliana na mshauri mwekelezi wakala wa ujenzi kuwa tutafanya utafiti kuona kama kuna uwezekano wa kuchimba ili kuongeza kina cha urefu wa maji ili jahazi ziweze kufika kwa urahisi katika gati hii na tutafanya hivyo kama tutashindwa kufikia mita hizo za 120,"alisema

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Umwagiliaji kutoka Wizara ya Kilimo Umwagiliaji na Mifugo, Haji Hamid Saleh alisema mradi huo wa ujenzi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji wa kilimo cha mpunga cha Kibokwa utasaidia kukuza uzalishaji wa chakula na kwamba  unatatarajiwa kuwanufaisha wakulima 15,000 wa eneo hilo.

"Mradi huu ni wa miaka mitatu na ulianza Aprili mwaka 2019 ambapo unafanyika eneo la zaidi ya hekta 147 na mradi umefikia asilimia 55 ukiwa unatarajiwa kuwa na ujenzi wa visima sita na mabwawa manne,"alisema

Alisema katika mradi huo ambao unagharimu dola za kimarekani 50 utasaidia wakulima kunufaika zaidi ambapo kwa kila hekta moja atakuwa anazalisha tani nne hadi sita.

Akizungumza katika majumuisho ya ziara hiyo, aliwataka Wana CCM kuendelea kushikamana katika kulinda na kukijenga Chama ili kiendelee kuimarika zaidi na kiwe na nguvu zaidi za kuendelea kubaki madarakani.

Alisema CCM kwa sasa inakabiliwa na uchaguzi wake wa Chama unaotarajia kufanyika mwaka 2022, hivyo wanachama na makada wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia ili kufanikisha uchaguzi huo na kuwapata viongozi bora watakaoendelea kuimarisha chama.

Kupitia ziara hiyo aliwapongeza viongozi mbalimbali wa serikali na Chama wa Wilaya hiyo kwa kazi kubwa wanayofanya ya utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM unaonufaisha wananchi wa maeneo mbalimbali wilayani humo.

Pamoja na hayo amesisitiza suala zima la Wananchi kuendelea kuheshimu na kulinda maridhiano ya kisiasa yaliyopo nchini kwani yameasisiwa kwa lengo la kudumisha amani na utulivu nchini ili kutoa nafasi pana kwa serikali kuwahudumia wananchi wake.

Dk.Mabodi, ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa bandari ya Mkokotoni,ujenzi wa kituo cha afya cha Kidagoni,ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji wa kilimo cha mpunga cha Kibokwa,ujenzi wa hoteli ya nyota tano ya Palolo na ujenzi wa Ofisi ya CCM Wilaya ya Kaskazini ‘A’  Unguja huko Gamba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.