Habari za Punde

Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema nia njema ya Hayati Rais Benjamin William Mkapa ilichangia sana kupatikana kwa Muafaka wa kwanza wa kisiasa Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa nia njema ya Hayati Rais Benjamin William Mkapa ilichangia sana kupatikana kwa Muafaka wa kwanza wa kisiasa Zanzibar ambao ulirejesha hali ya amani na utuliu visiwani humo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar-es-Salaam wakati akitoa hutuba yake katika Maadhimisho ya Kumbukizi ya Hayati Rais Benjamin William Mkapa, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Muafaka huo wa Kwanza ulisaidia sana kutuliza joto la kisiasa Zanzibar na kufugua fursa za majadiliano na mashrikiano ya kisiasa katika visiwa hivyo vya Zanzibar.

Aliongeza kuwa msimamo wake juu ya Muuungano ulikuwa thabiti, usiyoyumba na alikuwa tayari kuusimamia na kuulinda Muungano kwa kauli na vitendo.

Alisema kuwa Hayati Mkapa ameifanyia nchi mambo mengi makubwa ya kiuchumi na soko ambayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa Zanzibar na kuweza kuifungua kutoka katika ukiritimba wa uchumi wa karafuu.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Zanzibar ni mnufaikaji mkubwa wa miradi ya Taasisi ya Benjamin Mkapa tokea mwaka 2007 ambao miradi hiyo imejikita katika sekta ya afya hususan kujenga uwezo wa watumishi wa afya katika kutoa huduma zinazohusu UKIMWI, Kifua Kikuu, Mlaria na Afya ya Mama na Mtoto.

“Tunajivunia mafanikio yaliyopatikana kupitia miradi hii ambayo kwa kweli imesaidia sana juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanziar kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wote”, alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa anafarajika kwamba mazungumzo ya mashirikiano kati ya Serikali anayoiongoza na Taasisi ya Benjamin William Mkapa yako katika hatua nzuri ambapo yakikamilika yatasaidia sana azma ya kupunguza uhaba wa watumishi wa sekta ya afya, pamoja na upatikanaji wa fedha za kuwezesha lengo la Serikali anayoiongoza kumpatia Bima ya Afya kila Mzanzibari.

“Nawahakikkishia ushirikiano wangu na wenzangu wote Srtikalini kufanikisha azma hii”,alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Kwa upande mwengine Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumuelezea Hayati Rais Mkapa ambaye kwa upande wake alikuwa ni Rais aliyempa fursa ya kuhudumu katika Serikali yake kwa nafasi ya Naibu Waziri kwa miaka mitano.

Alisema kuwa alikuwa ndie Rais wa kwanza kuvumbua kipaji chake cha uongozi na kumteua kuwa Naibu Waziri wa mnamo mwaka 2000 ambapo aliwekeza akwakwe Imani kubwa na alibeba dhana kubwa sana kumteua akaiwa akijana na mgeni katika siasa akitokea katika taaluma yake ya udaktari.

Aliongeza kuwa kupitia mikono ya ulezi ya Hayati Rais Mkapa alimlea akakua kufika hapo alipo leo ambapo alisikitika kuwa aliondoka kabla ya kushuhudia akiapishwa kuwa Rais wa Zanzibar kwani hana shaka angejivunia sana kuona matunda ya kazi ya ulezi wake.

Rais Dk. Mwinyi alifahamisha kwamba Hayati Rais Mkapa kwake alikuwa ni baba na alimchukua kama mwanawe wa kumzaa kwani wakati wote alipata fursa ya kumuona na kuvuna hekima na busara zake akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.

“Kwa kweli nimefaidika naye sana kwake nimejifunza uongozi, nimejifunza kuhudumu na nimejifunza nidhamu ya kazi, daima nilimjua kama kiongozi mwenye njozi, hofu ya Mungu na mwanazuoni, alikuwa wa kipekee sana itoshe tu kusema alikuwa Benjamin William Mkapa hana mfano wake, hakuwepo mwingine na hapatakuwa mwingine baada yake”.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa yeye ni mmoja wa wadau wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa ambaye alipata fursa ya kuhudumu katika Taasisi hiyo kwa nafasi ya Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya Wadhamini baada ya kuteuliwa na Hayati Rais Mkapa mwaka 2006.

Alieleza kufurahishwa kwake kwamba alitimiza wajibu huo ipasavyo na hajutii fursa ile na inapoitiza Taasisi ya Benjamin Mkapa imefikia miaka 15, anafarajika na kujivunia kuwa sehemu ya mafanikio yake.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ameguswa na uamuzi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa wa kuanzisha Mfuko wa Wakfu wa Benjamin William Mkapa kwa ajili ya kuendeleza kazi zake kupitia Taasisi hiyo.

Alifahamisha kwamba Wakfu hiyo ikifanikiwa itasaidia sana kupunguza utegemezi wa misaada na kujenga uwezo wa Taasisi kujitegemea kwani kujitegemea ilikuwa nadharia ya Hayati Rais Mkapa.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Zanzibar inatekeleza Dira ya Maendeleo ya 2050 ambayo inalenga kuifikisha Zanzibar kuwa nchi ya Uchumi wa Kati wa Juu ifikapo mwaka 2050.

Alisema kuwa Dira hiyo imejengwa kwenye nguzo nne ambazo ni Mapinduzi ya Kiuchumi, Raislimali Watu na Huduma za Jamii, Utawala Bora na Utimilivu na Miundombinu.

Kwa upande wa Rasilimali Watu na Huduma za Jamii, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kujenga jamii ya watu wenye afya bora, wenye kuweza kushindana na wengine duniani, wabunifu na wachapa kazi ili waweze kuchangia kikamilifu katika uchumi wa nchi.

Rais Dk.Mwinyi alitoa pongezi kwa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa kuazimisha Kumbukumbu hiyo mwaka huu na miaka ijayo na kusisitiza kwamba itapendeza miaka ijayo kufanyika maadhimisho hayo Zanzibar na kuahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila aina ya ushirikiano utakaohitajika.

Katika hafla hiyo pia, kulikuwa na mjadala ulioendeshwa na Dk. Faustine Ndugulile, ukiwa na agenda muhimu ya “Afya kwa Wote”.

Viongozi kadhaa walihudhuria wakiwemo Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Majane wa Rais Mkapa, Mama Anna Mkapa, mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dini, Mabalozi, Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Kiraia pamoja na viongozi wengine.

Pia, viongozi marafiki wa Hayati Rais Makapa duniani nao walipata fursa ya kumuelezea Hayati Rais Mkapa kwa njia ya mtandao akiwemo Rais Mstaafu wa Marekani William Jefferson Clinton, Rais Mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair, ambapo pia, viongozi wengine nao walipata fursa hiyo aliwemo Rais Mstaafu Kikwete na wengineo

Mapema Rais Dk. Mwinyi mara baada ya kuingia katika ukumbi huo wa Mlimani City alikagua kazi zinazofanywa na Taasisi ya Benjamin William Mkapa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.