Watumishi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wameaswa kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu na kwa misingi ya uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa wadau wake.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Tixon Nzunda alipotembelea ofisi za Mfuko kwa ajili ya kufuatilia shughuli zinazofanywa na WCF.
“Nimefanikiwa kuzungumza na watendaji wa idara na vitengo vyote na moja ya maelekezo yangu ni kuwahimiza kutoa huduma kwa umma kwa kuzingatia misingi ya ueledi, uwajibikaji na usikivu na kuzingatia misingi na miongozo ya uendeshaji kazi serikalini”, alisema Bw. Nzunda.
“Pia nawasisitiza kuhakikisha kuwa utendaji wa shughuli za umma unazingatia misingi ya kujenga ustawi wa wananchi. Tumieni rasimilimali zilizopo kwa kuzingatia thamani ya fedha na uwekezaji ufanyike katika maeneo yenye tija ili kulinda amali za fidia kwa wanachama”.
Bw. Nzunda ameelekeza Mfuko kuhakikisha unaimarisha zaidi mifumo ya kielektroniki kutoka asilimia 80 hadi 100 ili huduma zote za madai ya fidia zifanyike kwa njia ya kielektroniki.
Naye Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dkt. John Mduma, amesema Mfuko utazingatia
kuimarisha huduma za kielektroniki ambapo pia unaendelea kuutangazia umma
kuhusu punguzo la Tozo ya michango lililofanywa na Serikali kwa sekta binafsi
kutoka asilimia 1.0 hadi 0.6. Aidha, Dkt. Mduma ameishukuru Serikali kwa hatua
hiyo muhimu na kuwasisitiza waajiri sekta binafsi kuzingatia mabadiliko husika.
No comments:
Post a Comment