Habari za Punde

Uzinduzi wa Mradi wa Mifumo ya Sayansi na Teknolojia Ubunifu.

Na Maulid Yussuf WEMA ZANZIBAR.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndg.Ali Khamis Juma amesema, Serikali Pamoja na Taasisi za Sayansi na Utafiti zinachukua hatua za kuimarisha sera, Utawala pamoja na Taasisi katika kufanya tafiti na kuongeza ubunifu ili kuleta maendeleo endelevu katika nchi.

Amesema hatua hiyo inafanyika kwa kutekeleza mradi wa kuimarisha mifumo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kufikia maendeleo Endelevu kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, Wizra ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Bara pamoja na Tume ya Taifa ya UNESCO.

Katibu Mkuu ameyasema hayo wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa kuimarisha Mifumo ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu, huko katika ukumbi wa Madinat Al Bahr Mbweni Mjini Unguja.

Amesema utekelezaji wa.mradi huo umelenga unahusisha maeneo makuu matano yakiwemo, Tathmini ya awali ya uwekaji wa alama ya mifumoya kitaifa ya kisayansi, teknolojia na ubunifu. Ushawishi wa kuyafanyia kazi Mapendekezi ya Sayansi na Watafiti wa Sayansi 2017.

Maeneo mengine ni Ujenzi wa uwezo wa Serikali, taasisi, watunga sera, na wadau kubunj sera ya utekelezaji wa mradi huo. Pia kufuatilia utekelezaji wa mradi. Pamoja na Maendeleo na utekelezaji wa mpango kazi wa vipaumbele vya kitaifa dhidi ya mradi huo.

Amesema amefarajika kuona mashirikiano kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Shirika la umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO Tanzania, kwa kuandaa  Mkutano huo muhimu kwa lengo la kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya Umma na Binafsi katika ngazi ya Taifa ili kuchangia Taarifa ya uandishi wa Ripoti hiyo.

Bwana Ali amesema ana matumaini makubwa kuwa maazimio yatakayofikiwa yatachangia kwa kiasi kikubwa  namna gani kwa pamoja wataweza kushirikiana katika kuchangia uimarishaji wa mifumo ya sayansi teknolojia na ubunifu, katika kufanya maamuzi shirikishi kwa lengo la kuimarisha maisha ya jamii na kujikinga na maradhi na athari za mabadiliko ya Tabianchi ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu katika nchi.

Aidha amesisitiza kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ipo tayari kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha wanatimiza azma ya mradi huo kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Pia amewaomba wadau wote kuunga Mkono jitihada za Serikali na UNESCO pamoja na Taasisi mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha uimarishaji wa mifumo ya Sayansi,Teknolojia na ubunifu, inapata nafasi ya kuchangia maendeleo ya kijamii na uchumi pamoja na kuikinga jamii na majanga yanayotokana na matokeo ya tafifi za kisayansi.

Nae  Mwakilishi wa Katibu Ntendaji Tume ya  Taifa ya UNESCO ambae pia ni Mkuu wa Programu za Sayansi Asilia bw Joel Abduel Samuel amesema lengo kuu ni kufanya tathmini ya mifumo yao ya Kisayansi na teknolojia katika eneo zima la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujua maeneo gani mradi wataweza kuyafanyia kazi yakiwemo ya sayansi ya jamii.

Pia kuangalia kwa namna gani wataweza kuboresha mifumo yao ya Sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuleta Maendeleo endelevu.

Kwa upande wake mratibu wa Mradi huo kutoka UNESCO Tanzania bw Keven Robert amesema pamoja na uzinduzi wa mradi huo, pia wadau wataweza kutoa maoni yao kwa kuona kiwango gani Serikali imeweza kutekeleza maazimio 10 ya tarehe 13.11.2017 yaliyofikiwa kati ya UNESCO pamoja na Nchi wanacha wa Umoja Mataifa, yanayolenga namna gani tafiti za kisayansi zinaweza zikahusika katika kuimarisha haki, usawa na utu, pamoja na tafiti za kisayansi zinakuwa karibu na jamii. 

Mradi huo unatekelezwa kwa Ushirikiano wa Wizara za Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, pamoja na Tume ya Taifa ya UNESCO chini ya ufadhili wa  Wakala wa Shirika la Maendeleo SIDA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.