Habari za Punde

CCM Haitosita Kumchukulia Hatua Mtendeji Yoyote wa Serikali Atakayezorotesha Utekelezaji wa Ilani ya CCM.-Mhe Abdulla.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na viongozi na watendaji wa CCM mkoa wa kaskazini Pemba Katika Ukumbi wa Halimashauri ya Wilaya ya Micheweni ikiwa ni muendelezo wa vikao vyake vya kuimarisha Chama.
Viongozi na watendaji wa Chama Mkoa wa Kaskazini Pemba wakifuatilia hotuba ya Mhe. Hemed Mjumbe wa  Kamati Kuu alioitoa katika Ukumbi wa Halimashauri ya Wilaya ya Micheweni.
Na.Abdi Kassim. OMPR. 

Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema chama cha Mapinduzi hakitosita kumchukulia hatua mtendaji yoyote wa serikali atakaezorotesha  utekelezaji wa Ilani ya Chama cha mapinduzi.

Mhe. Hemed alieleza hayo wakati akizungumza na viongozi pamoja na watendaji wa CCM wa Mkoa wa Kaskazini Pemba katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema kwa Mujibu wa Katiba na sheria za Nchi zinaelekeza kuwa chama kilichoshinda ndio chenye dhamana ya utekelezaji wa ilani kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wake, hivyo kwa vile CCM ndio ilioshinda kupitia uchaguzi mkuu wa Mwaka 2020 viongozi wote walioteuliwa wana jukumu la kuitekeleza ilani hiyo kwa vitendo bila ya kujali itikadi ya chama mtu anachotoka.

Alisisitiza kuwa, uwepo wa mfumo wa serikali ya umoja wa Kitaifa hautoi fursa kwa viongozi wanaotoka vyama vyengine kufanya kutotekeleza ilani badala yake inaelekeza kutekeleza ilani ya chama kilichoshinda kwa maslahi mapana ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar katika kuwaletea maendeleo.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu alisema bajeti iliopitishwa hivi karibuni na wajumbe wa baraza la wawakilishi ina lenga kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi  amewataka viongozi wa chama kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha pesa zilizopangwa kutekeleza bajeti hiyo zinatumika kama ilivyopangwa.

Mhe. Hemed aliwashauri viongozi wa majimbo pamoja na watendaji wa Chama kuchukua jitihada za makusudi kwa kushuka ngazi za chini kwenda kuzungumza na mabalozi kwa lengo la kujenga uhai wa chama.

Aliwakumbusha kwamba kitendo cha kusubiri kukaribia kwa uchaguzi hatimae kuanza kujitokeza kwa kuwafikia wananchi hakina tija badala yake wanapaswa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kujishusha ili kutatua matatizo na kero zinazowakabili  wananchi.

Aidha, Mhe. Hemed aliwataka viongozi hao wa Chama kutoka Mkoa wa Kasakazini Pemba kufanya kazi kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuhakikisha wanaweka takwimu sahihi juu ya wanachama kuanzia ngazi ya mashina, Matawi, majimbo, wilaya hadi ngazi ya Mkoa.

Nae, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mzee Mberwa Hamad Mberwa alimuhakikishia Mjumbe huyo wa Kamati kuu kuwa Ungozi wa Chama Mkoa wa Kaskazini utayafanyia kazi maagizo yote alioyatoa kupitia Mkutano huo kwa lengo kukiimarisha Chama cha Mapinduzi Katika Mkoa Huo.

Mzee Mberwa alieleza Chama katika Mkoa wa Kaskazini kitaendeleza utaratibu wake wa kufanya vikao kama ilivyolekezwa na katiba ya Chama kutokana na umuhimu wake katika kukijenga Chama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.