Habari za Punde

Katibu Mkuu CCM ziarani Zanzibar kuanzia kesho


 Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Catherine Peter Nao


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa Daniel Chongolo  anatarajiwa kuwasili visiwani hapa mnamo 4 Julai 2021 kwa mara ya kwanza tangia ateuliwe na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ikiwa ni ziara yake ya siku mbili.

Akizungumza Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine Peter Nao alisema ziara hiyo inatarajiwa kuanza Julai 4 hadi 5,  2021.

Katibu huyo alisema Katibu Mkuu huyo ataambatana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa  wanatarajiwa kupokelewa saa 3:00 asubuhi katika bandari ya Malindi Unguja na kwamba baadaye kiongozi huyo atakutana na Makamu Mwenyekiyi wa CCM Dk.Ali Mohamed Shein.

Alisema kuanzia saa 8:00 mchana Katibu huyo Mkuu na ujumbe wake atapokelewa na wanachama wa CCM katika mzunguko wa barabara ya Kisonge 'round about' na kunatarajiwa kuwepo kwa matembezi kuelekea Ofisi kuu ya CCM Kisiwandui Unguja.

"Atakapofika hapa katika ofisi kuu za CCM Katibu Chongolo atapokelewa kwa heshima zote za chama na kupokea gwaride la Jumuiya ya Umoja wa Vijana pia atazuru kaburi la rais wa kwanza hayati Abeid Amani Karume na kutumbuizwa na ngoma ya asili kisha atazungumza na wanachama na wakereketwa wa chama katika viwanja vya ofisi kuu,"alisema

Katibu huyo alisema dhamira ya ziara hii ni kujitambulisha na kuyasemea mambo ya uchaguzi wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwakani lakini pia kupata nafasi ya kuzungumza na wazee na wafanyakazi wa Chama cha Mapinduzi(CCM).

"Mwakani CCM itafanya uchaguzi wa kupanga safu yake vizuri kwa ajili ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwani chama chetu kinakuwa mwanzo wa uchaguzi ndio mwisho wa uchaguzi mwingine,"alisema

Katibu huyo wa NEC, aliwaomba wanachama na wakereketwa kujitokeza na kumsikiliza Katibu Mkuu huyo juu ya muelekeo wa ilani ya CCM na utekelezaji wake kwa waliyokabidhiwa.

"CCM ina ilani hivyo wanachama hawatafanya dhambi  kuja kumsikiliza kwani anatoa muelekeo wa ilani kama tunavyojua vikao vya Bunge na Baraza la Wawakilishi vimemalizika hivyo Julai mosi utekelezaji wa ilani kwa wenzetu tuliowakabidhi ndio wanaanza kwa hiyo anakuja kukuelezeni muelekeko wa ilani hiyo na utekelezaji wake,"alisema

Kwa mujibu wa ratiba iliotolewa na Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar Katibu Mkuu Chongolo anatarajiwa kuzungumza na Baraza la wazee la Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar na wazee watano kwa kila mikoa ya Unguja ikiwemo Mjini,Magharibi,Kaskazini na Kusini.

Mbali na hilo,Katibu Mkuu huyo anatarajiwa kukuonana na watumishi wote wa chama na jumuiya kwa mikoa minne ya Unguja pamoja na kupata fursa ya kuzungumza na Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi.

Pamoja na hayo Catherine, alieleza kuwa maandalizi ya mapokezi ya Viongozi hao katika  viwanja vya Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui tayari yamekamilika.

Wakizungumza baadhi ya wanachama visiwani hapa wameelezea matamanio na shauku zao ya kushuhudia Katibu Mkuu Chongoli atakapoelezea muelekeo na misimamo ya chama katika viwanja vya ofisi Kuu ya CCM kisiwandui atakapowahutubia wanachama hao.

Fatma Said Juma  ni miongoni mwa wanachama hao ambaye pia ni mkazi wa Kiembe Samaki alisema hali hiyo ya kuwa na shauku inatokana na mabadiliko makubwa yaliofanywa na Mwenyekiti wa Taifa Rais Samia baada ya kupitishwa na mkutano mkuu jijini Dodoma.

Alisema yeye kwa upande wake hawezi kukosa kuja kumsikiliza Katibu Mkuu huyo kwa sababu anaamini kuwa kiongozi huyo atakuja kuelezea misimamo na muelekeo wa mpya wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025.

Naye Bakar Issa Abdallah  mkaazi wa Mwanakwerekwe alisema akiwa mwanachama wa CCM amefurahishwa na ujio wa Katibu Mkuu huyo kutokana na kuwa tangia ateuliwa kushika nafasi hiyo wana-CCM wa visiwani hapa hawajawahi kumuona wala kusikia nasahaa zake.

"Kwangu mimi nifaraja sana kusikia taarifa kama hiyo kutokana na kuwa wanachama tutaweza kunufaika kufahamu muelekeo wa chama kwa ujumla na msimamo wake juu ya utekelezaji wa ilani kwa serikali zote mbili hususan kwenye kipindi hiki cha kuanza kwa bajeti ya serikali,"alisema

Alisema ujio wake wa Katibu Mkuu huyo pia itasaidia kuchochea zaidi kasi ya uhamasishaji kwa wanachama katika kuelekea uchaguzi mdogo  wa jimbo la Konde Mkoa wa Kaskazini lilopo Pemba ambapo wanachama watajitosa bila uoga wowote kuhakikisha jimbo hilo CCM inashinda kwa kura nyingi.

Kwa upande wake Khadija Salum Faki, Mkaazi wa Bububu alieleza kwamba Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kuimarika kutokana na kuwa na Viongozi na Watendaji wengi ambao ni Vijana waliobobea katika siasa za kisayansi zinazoendana na wakati wa sasa.

Alisema sera za Katibu Mkuu Chongolo, zimekuwa na mvuto na haiba ya kipekee kwa wanachama wa CCM hivyo matarajio yao ni kumsikia na kumshuhudia akizitoa kwa wanachama wote wa  CCM visiwani humo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.