Habari za Punde

Naibu Waziri Mhe.Mwanaidi Ataka Ulinzi Kwa Wanawake na Watoto Dhidi ya Vitendo vya Ukatili

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza na wafanyakazi wa Nyumba salama ya Wote Sawa (hawapo pichani) alipotembelea nyumba hiyo kuona shughuli za kuwahifadhi kwa wahanga wa vitendo vya ukatili zinavyoendeshwa. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu na kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Jamii, Juma Samwel

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW       

Mwandishi Wetu, Kasulu Kigoma

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amewataka watendaji wanaosimamia utekelezaji wa Sheria ya ulinzi wa haki za wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili kuhakikisha haki inapatikana ndani ya kipindi kilichowekwa na ikiwezekana ipatikane kwa haraka zaidi.

Naibu Waziri Mwanaidi amesema hayo, Wilayani Kasulu mkoani Kigoma alipofika katika nyumba moja ya kuwahifadhi wanawake na watoto waliokumbana na vitendo vya ukatili katika jamii kwenye nyumba salama ya Wote Sawa iliyoko Wilayani humo.

Naibu Waziri Mwanaidi amesema kuwa jamii inatakiwa kutoa taarifa dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia hususan kwa wanawake na watoto ili kuwawezesha wahanga wa vitendo hivyo kupata haki yao.

“Serikali inaandaa mazingira ya kukabiliana na vitendo ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kwa hiyo msikae kimya dhidi ya ukatili wa vitendo hivyo, Tumieni mifumo iliyopo kutoa taarifa na Sheria iweze kuchukua mkondo wake na wahanga hao kupata haki”alisema Niabu Waziri Mwanaidi.

Vilevile amesema kuwa ukimya katika jamii dhidi ya vitendo hivyo una madhara makubwa kwa waathirika na wakati mwingine ukimya huo unasababisha kutoweka kwa ndoto za waathirika katika maisha yao baadaye kutokana na kuathirika kimwili na kisaiklojia.

Aidha amependekeza mifumo iliyopo katika kusimamia na kuchunguza mashauri ya unyanyasaji wa kijinsia kuangaliwa upya kwa kuwa muda uliowekwa ni mwingi ilhali wahanga wanakuwa wakiteseka kwa muda mrefu kabla ya mashauri hayo kufanyiwa kazi kikamilifu na kufikishwa mahakamani.

Akizungumza kuhusu uendeshaji wa nyumba salama ya Wote Sawa, Meneja wa nyumba hiyo Jaqueline Ngalu amesema hatua iliyofikiwa ni kutokana na Serikali kwa kushirikiana na wadau kuandaa mwongozo wa kitaifa kuanzisha na kuendesha nyumba Salama.

Amesema kuwa watoto na wanawake wanaokidhi sifa za kupokelewa katika nyumba hiyo wanajihusishe na shughuli mbalimbali za ujasiriamali huku wakiendelea kupata huduma za ushauri nasaha ili wasiendelee kuathirika.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea kituo cha taarifa za maarifa kilichoko katika Kata ya Nyasha ambacho kinawaelimisha wanawake waliofanyiwa ukatili namna ya kupata haki zao kwa mujibu wa Sheria.

Naye Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Adrofina Mkuyu amesema kikundi hicho kimetokana na vikundi vya malezi chanya kwa jamii ambapo mwaka 2018 kilikuwa na wahudumiwa 48 idadi ambayo imeongezeka hadi 164 mwaka 2021.

Kituo cha Nyasha kinaendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu UNFPA na TGNP Mtandao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.