Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Akifungua Jengo la Utafiti wa Uvuvi na Rasilimali za Baharini Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikata utepe akifungua Kituo cha Utafiti wa Uvuvi na Rasilimali za Baharini Zanzibar, akiwa katika ziara yake katika Wilaya ya Mjini Unguja kutembelea Miradi ya Maendeleo katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema ufunguzi wa Jengo la Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi na Rasilimali za Baharini, kutafanikisha azma ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo cha kuzalisha mazao ya baharini yatakayoendana na Uchumi a Buluu.

Dk. Mwinyi amesema hayo katika hafla ya Ufunguzi wa Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi na Rasilima za Bharini, hafla iliofanyika Maruhubi, Mkoa Mjini Magharibi.

Akizungumza na wananchi na wadau wa sekta ya Uvuvi, Dk. Mwinyi alisema sekta ya Uvuvi ndio sekta kiongozi katika Uchumi mpya wa Buluu hapa nchini.

Alisema azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa bahari, kamwe haiwezi kukamilika endapo hakutakuwa na utafiti, hivyo alisema hatua ya kukamilika ujenzi w ajengo hilo ni muhimu katika kufanikisha azma hiyo.

Alisema azma ya  Serikali ni kuwapata  wavuvi wakubwa watakaokuwa na uwezo wa kuvua bahari kuu na kuanzisha viwanda vya kusarifu samaki , pamoja na kuwawezesha wavuvi wadogo ambao ndio wengi hapa nchini kutapata vifaa vitakavyowawezesha kuelekea kwenye uvuvi wenye tija.

Dk. Mwinyi alieleza kuwa miongoni mwa kazi za taasisi hiyo ni pamoja na kufanya utafiti wa rasilimali za bahari na kutoa vyeti vya Ithibati vya ubora wa mazao ya baharini, kwa wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika Viwanda vya kusarifu samaki.

Aidha, Dk. Mwinyi  alikaguwa ujenzi wa Soko Malindi na kuzungumza na wavuvi na kusema Serikali imekusudia kuhakikisha wavuvi wanatumia Vyombo vikubwa na vya kisasa  vyenye uwezo wa kuwafikisha mbali ili waweze kupata tija  kutokana na kazi wanazofanya.

Alisema  hatua hiyo mbali na kuwanufaisha wavuvi hao, lakini pia itaondosha uwezekano wa kutokea kwa vitendo vya uharibifu wa mazingira, ikiwemo uvuvi haramu.

Aliitaka Wizara ya Uchumi wa Buluu  na Uvuvi, Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Wavuvi wenyewe kukaa pamoja ili kuwabaini watu wanaoendesha vitendo hivyo.

Alisema umasikini unaweza kuondoka kwa kuwa na uvuvi wa kisasa, huku akibainisha kuwepo kwa Wawekezaji walionyesha nia ya kuwekeza katika kutenegeneza vyombo vya kisasa vya  uvuvi.

Alisema hali ya usalama bahari itaweza kupatikana kwa Wizara husika pamoja na vyombo vya Usalama kukaa pamoja, huku akiwataka wavuvi wao wenyewe kujiangalia kuhusiana na shughuli wanazozifanya.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali haina azma ya kuwapa watu wengine nyumba za wakaazi wa Mji Mkongwe, bali inalenga kuzinusuru nyumba hizo na kuanguka, kutokana na kukabiliwa na  hali mbaya (ubovu).

Alisema Serikali inakusudia kuurekebisha Mji Mkongwe na kuwa Mji wenye ‘Master Plan’ na utakaokuwa na miundombinu yote muhimu itakayokidhi mahitaji.

Kauli ya Dk. Mwinyi inatokana na dhana iliojengeka miongoni mwa wakaazi wa eneo hilo kuwa Serikali ina dhamira ya kuzichukua nyumba hizo.

Alisema Serikali inamtaka kila mkaazi wa Mji Mkongwe mwenye uwezo kutengeneza nyumba yake bila vikwazo vyovyote.

Alisema uingiaji wa magari mengi katika eneo hilo, ni miongoni mwa sababu zinazosababisha nyumba nyingi kubomoka.

Katika ziara hiyo Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuzitembelea nyumba za Maendeleo Kilimani na kuona hali ya uchakavu unaozikabili nyumba hizo, zilizojengwa mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.

Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo, Dk. Mwinyi alitowa wazo la kuja na mradi mpya wa Ujenzi wa nyumba za kisasa katika eneo hilo, ili ziweze kuchukua nafasi ya nyumba zilizopo ambapo hivi sasa ziko katika hali mbaya.

Alisema hatua hiyo itatowa fursa ya eneo hilo kuwa mji wa kisasa utakaokuwa na miundo mbinu ya kutosheleza pamoja na maeneo ya kupumzikia, maduka na michezo na mengine.

Katika hatua nyengine, akiendelea na ziara  yake Dk. Mwinyi alipata fursa ya kutembeela miradi mbali mbali ya Maendeleo pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi.

Maeneo hayo  ni pamoja na Ufukwe wa Bahari kwa Mchina Tambi Malindi na soko la muda Msikiti Mabuluu, Saateni tangi la Maji, pamoja na kutembelea Kituo cha Afya Jang’ombe,

Aidha, wananchi wa maeneo hayo nao walipata fursa ya kueleleza changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.