Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Akutana na Kuzungumza na Mkurugenzi wa ZIFF Prof.Mhando Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mkurugenzi wa Tamasha la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF) Prof. Martin Mhando akitowa maelezo ya Malengo na Dhamira ya Tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika  kesho 21/7/2021 katika viwanja vya Ngome Kongwe Jijini Zanzibar,mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Mkurugenzi wa Tamasha la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF) Prof Martin Mhando, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kutowa maelezo ya malengo la Tamasha hilo la Ziff, linalotarajiwa kufanyika katika viwanja vya ngome kongwe Jijini Zanzibar 21-7-2021, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa kuwepo kwa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF),  ni njia moja wapo ya kuukuza na kuutangaza utalii pamoja na urithi wa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF), ukiongozwa na Mkurugenzi wake Profesa Martin Muhando.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina unga mkono juhudi hizo zinazochukuliwa na ZIFF ambazo alisisitiza kwamba ndio njia muhimu ya kuukuza na kuutangaza utalii wa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi huo wa ZIFF kwa kazi kubwa inayofanya ambayo imekuwa ikileta tija katika kuutangaza na kuukuza utalii visiwani Zanzibar kwa kila mwaka.

Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Nane itaendelea kutoa ushirikiano wake katika kuhakikisha Tamasha hilo linaendelea kupata mafanikio zaidi.

Akieleza kuhusu suala zima la uigizaji wa Filamu kwa vijana, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema vijana wakapewa elimu sambamba na kuunganishwa pamoja ili waweze kukuza na kuendeleza vipaji vyao walivyonavyo katika tasnia mbali mbali.

Rasi Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema ikawepo sehemu maalum ya kutoa vipaji hasa ikizingatiwa kwamba vipaji hapa Zanzibar vipo na kinachohitajika hivi sasa ni kuendelezwa tu na kutoa shukurani kwa ZIFF kwa kuendeleza Tamasha hilo. 

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kwa upande wa tasnia ya muziki wa kizazi kipya, tasnia hiyo imeweza kupiga hatua kubwa na kuweza kufika mbali hivi sasa na kuweza kufananishwa na miziki kutoka nje ya Tanzania.  

Rais Dk. Mwinyi pia, alieleza haja ya kuanzishwa kwa vyuo vya kuzalisha vipaji hapa nchini huku akisisitiza kwamba kuwepo kwa semina zinazoendeshwa na ZIFF kutawasaidia kwa kiasi kikubwa vijana.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba matamasha ya Kimataifa likiwemo Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF), ambalo kwa jina jengine linaitwa Tamasha la Kimataifa la Nchi za Majahazi yanauwezo mkubwa wa kuutangaza utalii pamoja na kutangaza soko la kuuza filamu.

Mapema Mkurugenzi wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF), Profesa Martin Mhando  alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Tamasha hilo lililoanza miaka 24 iliyopita na kuweza kuleta mafanikio makubwa hapa Zanzibar ambalo linatarajiwa kufanyika kuanzia Julai 21 hadi 25 mwaka huu hapa Zanzibar.

Mhando alisema kuwa  katika Tamasha la mwaka huu filamu ya kwanza iliyoshinda ni kutoka Tanzania, lakini hata hivyo Tanzania ilipoanza ilikuwa ikifanya filamu ndogo lakini kila siku zikiendenda mafanikio zaidi yameonekana na kusema kwamba imefika wakati filamu zinazozalishwa nchini ziwe na taaluma.

Aidha, alisema kuwa kati ya filamu 65 za mwaka huu Tanzania ina filamu 16 na kumuhakikishia kwamba wanamatumaini makubwa ya kupata zawadi kutokana na filamu hizo za Tanzania kuwa nzuri.

Alisema kuwa Tamasha hilo ni la muda mrefu na limeweza kudumu kwa kiasi kikubwa hasa ikizingatiwa kwamba Tamasha la  ZIFF ni la pili kwa ukubwa katika bara la Afrika likitanguliwa na Tamasha la nchini Bukina Fasso.

Pia, alieleza azma yao ya kuanzisha soko la filamu hapa hapa Zanzibar kwani Zanzibar ni sehemu nzuri ya kutengeneza filamu na imekuwa ikijitangaza na kujiuza wenyewe.

Alisema kuwa lengo kubwa walilokuwa nalo hivi sasa ni kuiunganisha tasnia ya filamu na tasni ya utalii kufanya kazi moja ya kuitangaza Zanzibar.

Aliongeza kuwa mwaka huu katika mafunzo wanayoyafanya yakiwemo mafunzo ya upigaji wa picha ambayo imejikita zaidi kwa vijana wa Zanzibar ambao malengo makubwa ni kuutangaza uchumi wa Buluu sambamba na vijana wenyewe kupata kipato.

Alisema kuwa mwaka huu kwa kushirikiana na chuo cha DW cha Ujerumani wanafanya mafunzo ya filamu hasa kwa kuzingatia haja ya kuwa na filamu zenye muendelezo, na ksuema kwamba wamepanga kuchagua hadithi tano na kila hadithi italipwa dola za Kimarekani elfu kumi.

Aliongeza kwamba mwaka huu Tamasha limejitahidi kuangalia upande wa wanawake kwani filamu inayofungua Tamasha mwaka huu imetengenezwa hapa hapa Tanzania na aliyetengeneza ni mwanamke na ndiyo filamu iliyochaguliwa kufungua Tamasha la ‘Pan African Film Festival (PAFF)’ huko nchini Marekani.

Nae Bi Farida Nyamachumbe  mratibu wa ZIFF alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuliunga mkono Tamasha hilo tokea kuanzishwa kwake.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.