Na.Kassim Abdi. OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amezitaka taasisi mbali mbali na jamii kwa ujumla kuthamini kazi nzuri inayoendelea kufanywa na wasanii Nchini kutokana na mchango wao katika kufanikisha maendeleo ya taifa.
Mhe. Hemed alieleza hayo wakati akizindua rasmi tamasha la kwanza la washairi Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa washairi nchini kutokana na kazi yao nzuri ya kufikisha ujumbe jamii ikiwemo kupinga vitendo vya udhalilishaji, kupiga vita madawa ya kulevya pamoja na kutoa elimu kuhusiana na masuala ya Afya.
Alieleza kuwa mchango huo unaotolewa na wasanii ikijumuisha wasanii wa utanzu wa mashairi imepelekea Serikali zote mbili kuunda Wizara maalum zinazohusiana na Utamadun, sanaa na Michezo katika kuhakikisha kuwa tasnia hiyo zinapiga hatua.
“Washairi wamekuwa mstari wa mbele kuisadia jamii hasa katika kufikisha ujumbe katika kukemea matendo maovu, kushajiisha ustawi wa wananchi kiafya wakati wa maradhi ya miripuki ya maradhi kama vile Kipindupindu, Ukimwi na hata janga la covid 19” Alisema Mhe. Hemed
Akizungumzia suala la kuhifadhi kazi za wasanii Makamu wa Pili wa Rais alizitaka Jumuiya za Hakimiliki COSOTA na COSOZA kusimamia vyema kanuni ziliopo za ukusanyaji wa mirabaha kutoka kwa watumiaji wa kazi za sanaa ili wasanii wanufaike na matunda ya kazi zao.
Aidha, Mhe. Hemed aliyakumbusha Mabaraza yanayosimamia sanaa Tanzania kuendelea kuwalea wasanii wa mashairi na sanaa nyenginezo na kuyataka mabaraza hayo kuwawekea mazingira rafiki washairi ili wafaidike kazi zao za sanaa.
Katika hotuba yake Makamu wa Pili wa Rais aliwataka washairi kutumia mitandao ya kijamii kama vile Face book, Youtube,Instegram na ticktok ili kuuza kazi zao na kujikamua na ukali wa maisha.
Kuhusiana na changamoto zinazowakabili washairi hao Mhe. Hemed aliutaka uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha kuwa wanakaa pamoja na washairi hao ili kuzimaliza changamoto zote hasa ile ya kukosa ofisi za kudumu huku akisisitiza serikali ya awamu ya nane itaendelea kuikuza sanaa ya ushairi.
Nae Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Mauid Mwita aliwapongeza washairi kwa kuandaa tamasha hilo hali iyo iliopelekea kurudisha hadhi ya mashairi nchini na kuwataka washairi hao kuiga na kusoma kupitia washairi waliotangulia.
Mhe. Tabia amesema kuwa jamii hunufaika kupitia kazi za washairi hasa katika kuelemisha kukosoa na kuburudisha kutokana na matumizi mazuri ya lugha ya Kiswahili katika kazi hizo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa umoja wa washairi Tanzania (UWASHATA) Bwana Hassan Ligile alisema tamasha hili litakuwa endelevu ambapo kila mwaka hali itakayosaidia kurudisha hadhi ya mashairi nchini.
Ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa wizara ya habari Zanzibar kutokana na mchango wake mkubwa katika kufanikisha kufanyika kwa Tamasha hilo na kuahidi tamasha lijalo litafanyika kupitia upande mwengine wa Muungano.
Akisoma risala ya washairi Ndugu Said Suleiman Ali ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuziomba taasisi husika za kumbukumbu na historia kuzitambua kazi za washairi na kuzitunza ili kukuza Idara ya Nyaraka, kwa lengo la kuacha athari kwa kizazi cha sasa na baadae.
Kupitia tamasha hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.Mhe Hemed Suleiman Abdulla, amezindua kazi mbali mbali za watunzi wa mashairi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa Jamii.
No comments:
Post a Comment