Mtaa wa Fuguni-Malindi, wakaazi wake walikuwa watu wa makabila mengi, kama Wangazija, Waarabu, Wahindi, Makumbaro, Washihiri, Wagunya, Waswahili na Mabulushi.
Na Marehemu Salim Mohammed Mbamba
Nyumba yetu ilielekeana na nyumba ya Bwana Abdullah Jimbu, ambae alikuwa ni mvuvi wa samaki. Mkono wa kulia, ilikuwa nyumba ya Bwan Saleh Mngereza, dalali wa samaki markiti. Alikuwa na mwanawe akiitwa Ali Bin Hassan, na alikuwa mkubwa wa chama cha Beni cha watu wa Malindi na Funguni, kiitwacho Mashin Low (Marshall Law). Ali Bin Hassan sasa ana mtoto na wajukuu. Mwanawe anaitwa Saleh Ali, na yupo Uganda.
Nyuma ya nyumba yetu kulikuwa na nyumba akikaa Seyyid Mohammed Mansab na Bwana Rijali. Bwana Rijali alikuwa na mke akiitwa Bi Iki. Na Seyyid Mohammed Mansab alikuwa na Bi Dodo Msimu. Seyyid Mansab alipata watoto watano (1) Shariff, (2) AbdulRahman (3) Abubakar, (4) Khadija na (5) Eisha. Na Bwan Rijali alijaaliwa kupata mtoto mmoja, jina lake Zubeir Rijal.
Wote hao wakikaa nyumba moja. Katika hiyo nyumba pia alikuwepo bi Maryam Bit Khamesi ambae alikuwa na mtoto akiitwa Saleh Awadh, ambae alikuwa hirimu yangu. Mimi nae tumesoma chumba kimoja, lakini yeye akaacha skuli na kuingia ufundi alipofika 1st Primary katika mwaka wa 1927. Bi Maryam Khamesi alikuwa na mdogo wake akiitwa Bi Darasa.
Jirani yetu vile vile, kulikuwa na nyumba ya Bit Labidi ambae aliolewa na Said Mohammed Othman, lakini hawakuzaa. Ndugu wa bwana Said Mohammed Othman ni Bit Mohammed Seluwa, Idi Mohammed Othman na Bakari Mohammed Othman, maarufu Bakari Magoma.
Bit Seluwa alimzaa Zubeda wa Mzee El Kesi, na huyu Zubeda aliolewa na Maalim Abdulwadud na kuwazaa Abulrazak na Mohammed (John) Wadud. Nyumba hiyo baadae aliinunuwa ndugu yangu bi Maymuna Mohammed Mbamba, 1896-1992 (Bi Maulidi) kwa jina jengine.
Nyumba ya Bit Labidi, mlango mkubwa ulielekea nyumba ya mawe ambayo kwanza ilikuwa ya bwana Mawiya na baadae akainunuwa Bwana Mohammed Ameir El Hinawi.
Tena kulikuwa nyumba ya Mame Gagaga, ambae alikuwa na watoto: Bi Zamana, Bi Mshenzi na Bi Mtumwa. Huyu Bi Zamana, alimzaa: Mwan Riziki, Said Ali Idarus na Said Mohammed Idarus. Bi Mtumwa, aliwazaa: Mwanakheri na Luki. Bi Mshenzi, yeye aliolewa na bwana Mohammed El Haji ambae kazi yake ilikuwa akipeleka matunda melini, na wana mtoto wa kike, maarufu, Bai.
Tena kulikuwa nyumba ya bwana Ali Bin Dahman. Bwana Ali Bin Dahman kazi yake ilikuwa ni kuuza miti Gulioni. Na alikuwa na watoto: Mohammed Ali, Abdullah Ali na Sheikha Ali.
Tena nyumba ya bwana Hariri ambae ni mkubwa wake Sheikh Burhan Mkelle. Mkewe bwana Hariri, akiitwa Bi Ubwa, lakini hawakuzaa, wakilea tu.
Halafu kulikua nyumba ya kina Ahmed Said na Mohammed Said, ambayo ilielekeana na nyumba ya Bi Bahati, ambayo mwishoni akikaa Arafa na mama yake na ndugu zake. Mama yao kina Arafa, akiitwa Bi Mgeni.
Baada ya hapo, kulikuwa nyumba ya Maalim Juma, ambae alimzaa Maalim Abdulwadud. Maalim Juma alikuwa sheikh mkubwa wa dini, na watu wengi wakisoma dini kwake. Watu wa Funguni mpaka watoto, na mimi, niliwahi kusoma kwake. Watu wengine wakitoka ng’ambo kuja kusoma kwake. Nyumba yake Maalim Juma, ilitazamana na nyumba ya bwana Mohammed Ahmed. Huyu bwana Mohamed Ahmed, amemzaa Bimkubwa Ahmed. Nyumba hii ilitazamana na nyumba ya Bi Yaya Nguru, ndio umaarufu wake, kwani ndio biashara yake.
Ukiendelea, kulikuwa na nyumba ya Bit Idd au Mama Idd, ambae akiuza kisambu na mboga yamayugwa. Nyumba hii imeelekeana na nyumba ya Mohammed Mzee, maarufu, Mohammed Panganyile. Na kulia ilikuwa nyumba ya bi Msiha, ambae alikuwa na mtoto akiitwa Mtumwa wa Msiha.
Pia kulikuwa nyumba ambayo mlango wake mkubwa ukitazamana na nyumba akikaa dada yangu Bi MwanSharifu (Batuli) 1884-1926 pamoja na mumewe.
Na tena kulikua nyumba kukiuzwa fenesi ambayo ilielekeana na duka la Bi Remi Ismail Khoja. Watoto wake Kassu na Abdullah walikuwa hirimu yangu.
Hapo hapo, kulikuwa na nyumba ya Bwana Mdahoma, mvuvi wa samaki ambae alikuwa akivuwa pamoja na bwana Abdullah Jimba.
Pia kulikuwa na nyumba ya Bwan Slim ambae alikuwa ni jamaa wa Bi Ngomeni, na Fatma mkanga samaki, na Ma Tosha. Nyumba hii imeelekeana na nyumba ya Mwana Eisha Mhoma. Nyuma ya nyumba ya Mwana Eisha Mhoma, kulikuwa nyumba ya Bi Mwan Shariffu Ki-Chinchiri, na mama yake Ali na Rajab Saleh, watoto wa bwana Saleh Hamadi.
Tena nyumba ya Bi Mbahuwa, ambayo nyuma kulikuwa nyumba ya mama yake Mdehe wa Bwana na Safiya, mama wa Ahmed Mzee na Sheikha.
Pia, jirani na hapo kulikuwa nyumba ya kina Tobo, Bit Islahi, Mama Maida, Juma Msomali, Himidi Mbwanga, Salima Mahazi, Bi Mwana Amina wa Said Ali, na Mwan Zakiya na Bit Sultan, mama yake bi Mwenzao, ambae alimzaa Sadiq Rajab. Na hapo hapo kulikuwa na nyumba ya Hamadii na Mzee Bedeni na Mame Mwinyi.
Baadae kulikuwa na nyumba ya Mama Issa aliemzaa Bi Asha, mama yake Bi Rehema, aliemzaa Seif Rashid. Kwa mlango wa mbele, ndiko kwa Bwana Athumani, aliemuowa Zubeda wa Mzee El Kesi. Kwa mlango wa nyuma, kulikuwa nyumba ya Bi Hamisi.
Tena, nyumba ya Mama Harusi wa Sewa, ambae akipunga mashetani wa Shamng’ombe, na alikuwa na watoto wawili wanawake. Mmoja akiitwa Mgeni ambae tulisoma chuoni pamoja, na mkubwa wake, ambae aliolewa na Shariff Said Athumani. Nyumba hii imeelekeana na nyumba ya mama yake Mdehele.
Usoni kulikuwa na nyumba ya Ali Kipedi, ambae alikuwa na mtoto wake akiitwa Athumani, na alikuwa mmoja katika wakubwa wa ngoma ya Manganja. Nyumba hii alikaa Bi Mbahuwa, mkewe Maalim Ramadhan Mohammed Sabir. Nyumba hii ilielekeana na nyumba ya Yusuf Abdullah.
Halafu nyumba ya Bi Rahawani, ambayo baadae ikaliwa na Maalim Ramdhan Mohammed Sabir na mkewe Mbahuwa. Nyumba hiyo pia alikaa bi Kishoga akiuuza njugu.
Baadae kulikuwa nyumba ya kina Abdullah Kassum ambayo kwanza ilikuwa ya Mame Hamissuu na mwanawe. Jirani na nyumba ya kwanza, ilikuwa nyumba ya Bimkubwa Ahmed, ambae aliwahi kuolewa na kumzaa Ahmed Mohammed Othman, kwa jina jingine (Ahmed Kedi). Nyumba hii ilikuwa jirani na nyumba ya Saleh Bin Musa, kazi yake zamani akiuuza mbao.
Nyuma ya nyumba ya Saleh Bin Mussa, ndio upande aliokuwa akikaa mama mzazi wa Bit Seluwa na ndugu zake. Karibu na hapo kulikuwa nyumba ya mame Muhammed Mshanghama, Sheikh Muhammed Kheri, mama Rashid, na Bwana Yahya, fundi wa saa. Na baadae kulikuwa na nyumba ya mawe ilioandikwa “MALINDI-FUNGUNI” ambayo ilikuwa karibu na nyumba ya Sheha Juma na ya Mzee Kitipwa na mama yake mke wa Khamisi Mussa.
Hiyo nyumba ya mawe alikuwa akikaa Bwana Hamid ambae alikuwa wakili. Na jirani yake, ilikuwa nyumba ya Mattar Bin Saleh ambae akifanya kazi soko la samaki.
Karibu na nyumba ya bwana Mzee Mohammed, kulikuwa nyumba ya Bi Mwan Sokina ambae akikaa na watoto wake, Abdullah Jabu, Hassan Saghir na Abdulsattar. Na pia kulikuwa na nyumba ya mawe ya Mansur Abeid ambayo ilikuwa karibu na nyumba ya Fatuma Said. Nyumba hiyo asili yake ilikuwa ni ya Mwana Arafa au Bi Muhaza, mama yake Bi Asha Msindihizi na Mohammed Saleh Farsi. Nyumba hii ilielekeana na nyumba ya Khamis Nne-nne, na nyumba ya Bulushi Jamaddar, ambae akifuga mbuzi wa maziwa na wakupandisha.
Pia kulikuwa na nyumba ya Bi Tapu ambayo imeelekeana na nyumba ya Bwana Saleh na pia nyumba ya Bi Mkubwa Muhideen. Mkono wa kulia, ilikuwa nyumba ya babu yake Ali na Buda, maarufu “Ali Kona” ambae alikuwa jamaa yake bwana Osman, babake Sadiq na Bablo.
Baada ya nyumba ya Bi Mkubwa Muhideen kulikuwa nyumba ya kina Salum Said Admeri, na baadae kulikuwa nyumba ya mjomba wake Mohammed Kaleheza, akiitwa Mzee Shithi akifanya kazi ya mafuta kabla kampuni ya mafuta kuhamia Hospitali. Nyumba hii ilikabiliana na nyumba ya Khamisi Ba Hisawo na nyumba ya bwana Khalifa, ambae akishona charahani kwa kina Maalim Badi. Nyumba hii imeelekena na nyumba ambayo akikaa Bit Saleh Mwan Neema na mtoto wake, - mama yao Abdullah na Mussa Kassim na Bit Bakari, mama yake Bi Fatuma Islam au Ruzuna, jina ambalo akiitwa wakati tupokuwa chuoni.
Vile vile kulikuwa na nyumba ya Bi Mwalimu Mweupe ambayo akikaa Bi Mshenzi na Bi Msankule. Nyumba hiyo upande ukitumiwa kama Chuo cha kusomesha Quraan. Nyumba hii ilielekeana na nyumba ya Bi Safini na nyumba ya Bi Mwanzalifa.
Baadae tena kulikuwa nyumba ya Baharuni, nyumba ya Mwana Khadija Muhideen, nyumba ya Mwan Shariffu Kalathumi, nyumba ya Bit Saleh Mnubi na ndugu yake Bit Msimu, ambae alikuwa na athari ya jicho la mtoto. Na tena nyumba ya Bit Adamu, mama yake Salim Bin Hilal na Mohamemd Bin Hilal (Jinja), karibu ya Forodha ya Papa.
Kutoka kwa Bit Seluwa, kulikuwa nyumba ya Mzee Islam, baba yake Ahmed Mzee na Shekha, tena kulikuwa nyumba ya kina Jiddawi, nyumba ya Shaaban Boti, nyumba ya Bi Mwalimu wa Bwan Nassoro, nyumba ya Fatuma Mbaye, ambayo baadae aliiuza, na tena nyumba ya Mzee Risasi na ya Bi Shuu na Mzee Mtopa. Pia kulikuwa nyumba ya Bi Thurea na Mwanate, iliokuwa karibu ya msikiti wa Funguni na pia kulikuwa nyumba ya Sheikh Mohammed Kheri, na baadae nyumba ya kina Hamisani na Baubwa.
Karibu na hapo kulikua na nyumba ya Bi Zena, Bi Rubeya – mama wa Bwamkubwa Panganyile, bwana Rubeya, Saleh Bin Ahmed na mkewe Bi Zakia, mama yake Badu, Helewa, Matar Mlinda, Mwana Harusi ambae akipunga Kisomali. Pia, nyumba ya (Fundi Subira alimlea Mussa Kassim) na Mzee Hamadi wa Msali alikuwa na mwanawe akiitwa Msafiri.
Nyumba ya mawe wakikaa Makarwa, na nyingine ya bati karibu ya bwana Saleh Aaed, zote zilielekea pwani. Jirani ya msikiti wa Funguni akikaa mama Jibrolta.
Salim Mohammed Mbamba
(20 Dec 1910 - 8 May 1992)
No comments:
Post a Comment