Habari za Punde

Migogoro ya Ardhi Bado ni Kitendawili -- Mhe.Othman.

 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameeleza ulazima wa kuwatumia wataalamu wa milki kuu (‘Real Estate Professionals’) kutokana na ufinyu mkubwa wa ardhi ili kuleta maendeleo ya kweli ya kiuchumi nchini.

Makamu wa Kwanza ameitaja Zanzibar kwa ujumla wake kuwa ni eneo la kitalii ambalo linapokea wageni wengi wa kimataifa tangu asili, na hivyo linahitaji kutoa kipaumbele katika matumizi bora ya ardhi yanayoweza kuchangia kupendezesha mitaa na mandhari ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Mhe. Othman ameyasema hayo leo, wakati akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Pili wa Mwaka wa Taasisi ya Wataalamu wa Milki Kuu Tanzania (AREPTA) unaofanyika katika Hoteli ya Verde, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Akiongelea juu ya tatizo sugu la biashara holela ya majengo na mizozo katika umiliki wa ardhi, Mhe. Othman amesema, “binafsi ninaamini kuwa iwapo suluhisho la migogoro ya ardhi litapatikana, wananchi watatekeleza majukumu yao ya kilimo, ufugaji na ujenzi kwa tija zaidi kulikoni hali ilivyo sasa”.

Mhe. Othman ametoa wito kwa waandaaji wa kongamano hilo kutafakari namna bora ya kutumia akiba kubwa ya wataalamu waliobobea, ili kutafuta muarubaini wa tatizo sugu la matumizi holela ya ardhi na biashara ya majengo na kusaidia kuikwamua nchi kiuchumi; huku akieleza utayari wa Serikali katika kuunga mkono juhudi hizo.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Rais wa Taasisi ya Milki Kuu Tanzania, Bw. Andrew Katto alibainisha mahitaji makubwa ya sheria itakayodhibiti wimbi kubwa la biashara holela ya umiliki wa majengo na ardhi, akisema azma hiyo itawezekana kwa mashirikiano makubwa ya Serikali.

Mkutano huo wa siku mbili unawajumuisha wataalamu na wanataaluma wa nyanja mbali mbali za maendeleo ya ardhi ambao ni pamoja na Wathamini, Maafisa ardhi, Mawakala wa milki, Wasimamizi, na Wachambuzi wa biashara za majengo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.  

Dhamira ya kongamano hilo ni pamoja na kujadili njia muafaka na endelevu ili kuifikisha Zanzinar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla katika uchumi bora kupitia tasnia ya milki kuu sambamba na utatuzi wa migogoro ya ardhi inayoendelea kubaki kuwa donda ndugu nchini.
 
 *Kitengo cha Habari*
*Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Zanzibar*
 26/08/2021

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.