Habari za Punde

Wafadhili Mradi wa Kuwarejesha Watoto Skuli Ngazi ya Msingi Waridhishwa na Hatua ya Wizara ya Elimu Zanzibar.

Na Maulid Yussuf WEMA

Wafadhili wa mradi wa kuwarejesha watoto Skuli, katika ngazi ya msingi, wameelezea kuridhishwa na hatua ya Wizara ya Elimu juu ya namna walivyoanza kuwarejesha Skuli watoto.

Wakizungumza wakati walipofanya ziara kuangalia baadhi ya Skuli waliopo Wanafunzi hao wamesema, juhudi kubwa bado zinahitajika kuwarejesha watoto hao hasa wanawake.

Wamesema imeonekana idadi kubwa sana ya watoto waliorejea hadi sasa ni wanaume kuliko wanawake, hali ambayo inaonesha kuwepo kwa muamko mdogo kwa wazazi na walezi katika kuwarejesha watoto wao Skuli hasa wanawake.

Aidha wameahidi kuyafanyia kazi mahitaji yao yote wanayoyataka ili kuhakikisha wanawasaidia watoto hao kusoma na kuweza kuwa viongozi bora wa baadae.

Nae Mkurugenzi Idara ya Mipango Sera na Utafiti Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar bwana Khalid Masoud Waziri amesema, madhumuni ya ziara hiyo ni kuona kwa vitendo namna mradi huo ulivyoanza kutekelezwa tokea kuzindiwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Amesema mpaka sasa tayari wanafunzi 4009 wamesharejeshwa Skuli kwa Unguja na Pemba ambapo bado wanaendelea kuwahamasisha jamii na viongozi wa ngazi za Shehia, Wilaya na Mikoa ili kuweza kusaidia kuwarudisha Skuli  watoto hao.

Nao Wanafunzi wamepata nafasi ya kuiomba Wizara ya Elomu pamoja na ufadhili huo,  kuwapatia sare za Skuli, vifaa vyote vya kusomea pamoja na kuwawekea miundo mbinu bora ya Skuli zao ili waweze kusoma kwa ufanisi zaidi.

Skuli walizotembelea ni pamoja na Skuli ya Msingi Fukuchani, Skuli ya Msingi Potoa na Skuli ya Msingi Mkokotoni.

Mradi wa kuwarejesha watoto Skuli unatekelezwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa ufadhili wa Shirika la UNICEF pamoja na Taasisi inayoshughulikia masuala ya elimu kwa wote EAC kutoka Qatar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.