Habari za Punde

Jumuiya ya Watoa Huduma katika sekta ya Mafuta na Gesi (ZAOGS) wakutana na Uongozi wa ZPRA na ZPDC Zanzibar

 Mkurugenzi Mtendaji Adam Abdulla Makame wa nne kulia akipata picha ya pamoja na uongozi wa Jumuiya ya Watoa Huduma katika sekta ya Mafuta na Gesi (ZAOGS)  ukiongozwa na Balozi Abdulsamad Abdulrahim wa tano kulia

Mkurugenzi wa ZPDC bwana Mikidadi Ali Rashidi wa nne kulia akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Jumuiya ya Watoa Huduma katika sekta ya Mafuta na Gesi (ZAOGS) ukiongozwa na Balozi Abdulsamad Abdulrahim

Kikao kikiendelea kati ya ZPDC, ZPRA na ZAOGS

Na Mwandishi wetu

Kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi alililitoa Disemba 5, 2020, kuhusu kuazishwa mchakato wa kuunda Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi Zanzibar ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali hizo pale shughuli za uchimbaji na uzalishaji zitakapoanza.

Kufiatia agizo hilo, Jumuiya ya Watoa Huduma katika sekta ya Mafuta na Gesi (ZAOGS) imekamilisha usajili na kuanza majukumu yake rasmi ambapo leo Bodi yake ikiongozwa na Balozi Abdulsamad Abdulrahim imekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi Zanzibar Petroleum (Upstream) Regulatory Authority (ZPRA) na Zanzibar Petroleum Development Company (ZPDC).

Majadiliano na maazimio katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kuitambulisha Bodi na Sekreteriat yake, pamoja na kujadiliana kwa kina namna ya kushirikiana na Serikali na kuandaa warsha za pamoja zitakazotoa elimu juu ya fursa za biashara ziliopo kwenye mnyororo wa thamani katika sekta hiyo, pamoja na kuelimisha wananchi juu ya viwango vya kimataifa kwa maslahi ya uchumi wa Zanzibar na wananchi kwa ujumla.

Pia kusaidia kuongeza ushirikiano na serikali katika kuboresha sheria zinazosimamia ushiriki wa wananchi (Local Content) katika sekta ya mafuta na gesi na mapato pamoja na kushirikiana na Serikali katika kutengeneza na kuboresha kanuni zitakazowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu na kunufaika na rasilimali hizo na kusimamia maslahi ya wananchi wetu katika rasilimali za mafuta na gesi asilia.

 “Leo Bodi yetu imekutana na kufanya mazungumzo na ZPRA na ZPDC yenye lengo la kujenga nyumba kwa pamoja. Sisi wajibu wetu kutetea na kuhamisha wananchi wafaidike na fursa ziliopo kwenye miradi. Vile vile kuhakikisha Makampuni yatakayowekeza katika miradi mbali mbali ya sekta ya mafuta na gesi na miradi ya kimkakati kununua huduma na bidhaa zinazopatikana nchini. Na pale ambapo huduma na bidhaa hazipatikani nchini, basi makampuni hayo yanapawa kununua kutoka katika kampuni za ndani yenye wabia nje ya nchi” alisema Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Balozi Abdulsamad Abdulrahim.

“Kuanzishwa kwa Jumuiya hii ni kuunga mkono juhudi na sera za Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi zilizodhihirisha kiwango cha juu cha uongozi na dira yake na kuhakikisha anawaunganisha watoa huduma waliopo Zanzibar ili kuchukua fursa zitakazotokana na miradi hii. Jumuiya imeshaundwa na imeanza kufanya kazi tukitambua kwamba kazi hii itahusisha kujenga uwezo wa watoa huduma wetu,” alisema Balozi Abdulsamad.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.