Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma
Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inatarajia kuzindua “Jogging club” yao
hivi karibuni kuunga mkono juhudi za Serikali kuwahimiza watumishi wote pamoja
na wananchi kote nchini kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya zao.
Akizungumza
mara baada ya kuhitimisha mazoezi leo Agosti 28, 2021 katika Uwanja wa Jamhuri
Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bw. Bernard Marceline
amesema mazoezi hayo ni maandalizi ya uzinduzi rasmi wa Club Wizara hiyo.
“Watumishi
wengi wamejitokeza kufanya mazoezi, hii ni namna bora kwa watumishi kujiandaa kuelekea
uzinduzi wa jogging club yetu na kuweka miili yao kwenye utimamu na leo wameanza
kufanya mazoezi kuanzia saa 12:00-2:00 asubuhi hapa uwanja wa Jamhuri” amesema
Bw. Bernard.
Aidha,
Wizara hiyo imeweka utaratibu wa watumishi kufanya mazoezi kila wiki mara tatu
kwa wiki ambapo siku ya Jumatano watafanya mazoezi katika uwanja wa shule ya
sekondari Dodoma, Ijumaa watatembea kutoka Mkao Makuu ya Wizara hiyo zilizopo
Mji wa Serikali Mtumba hadi barabara kuu ya Dodoma-Dar es Salaam kuanzia saa
9:00 – 10: jioni wakati siku ya Jumamosi watafanya mazoezi kuanzia saa 12:00 –
2:00 asubuhi katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Tatu
Hamza mtumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo anasema mazoezi
yanasaidia kuimarisha afya na kuweka miili vizuri na yanasaidia kuimarisha
mwili hatua inayowafanya kutekeleza majukumu yao vema.
Katika
mazoezi hayo, watumishi wa Wizara wameungana na wananchi wa Jiji la Dodoma
wakiongozwa na Jumuiya ya Wanawake Tanzania ambapo Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Taifa
Dkt. Philis Nyimbi amewashukuru wananchi wa Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi
kufanya mazoezi kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwahimiza wananachi kufanya
mazoezi kuimarisha afya zao.
“Mazoezi
ni hazina ya afya, ukifanya mazoezi utaweka afya yako vizuri na kuimarisha
mfumo wako wa mwili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kujikinga na
tatizo la UVIKO-19 linaloisumbua dunia sasa ili kutimiza malengo yako” amesema Dkt.
Philis.
Amewahimiza
wananchi kutumia siku ya Jumamosi ya mwisho ya kila mwezi kufanya mazoezi nchi
nzima ili kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan la kuwahimiza wananchi kufanya mazoezi kuboresha afya zao.
Mazoezi
yanafaida nyingi kwa mwanadamu ambapo yanamfanya mtu kujisikia kuwa na afya
njema, kukupa mwili nguvu hatua inayosaidia mtu kufanya kazi kwa nguvu bila
kujiskia umechoka, hupunguza uzito, hunyoosha na kuimarisha misuli ya mwili,
kupunguza presha, husaidia kupunguza mafuta, huimarisha mifupa ya mwili,
husaidia kupunguza ugonjwa wa kisukari, huboresha usingizi na husaidia kuimarisha
sehemu za viungo vya mwili.
No comments:
Post a Comment