Habari za Punde

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan na Vipaumbele vya Sensa katika Shughuli za Maendeleo

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akibonyeza kitufe kuzindua rasmi Mpango wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Septemba 14,2021 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Na Rehema Kasimu, MAELEZO.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi ifikapo mwezi Agosti 2022. Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), ipo kwenye maandalizi ya kufanya Sensa hiyo.

Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012, sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini, kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum, hivyo sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi.

Takwimu hizi za msingi ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo.

Umuhimu wa kipekee wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa;

Umuhimu mwingine ni pamoja na taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali, taarifa za msingi za hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote;

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzania (NBS) sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa sababu inatoa tahtmini ya takwimu zitakazosaidia kukokotoa viashiria vingine mfano pato la mtu mmoja mmoja,pato la taifa, ajira na ukosefu wa Ajira na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi pamoja na taarifa itakayowezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira; na

Aidha NBS pia imesema sensa itasaidia kuleta msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia. Takwimu sahihi za Sensa zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa.

Katika kuhakikisha sensa ya watu na makazi inafanikiwa nchini Tanzania,Rais wa Jamhuri ya Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameviomba Vyombo vya Habari kuelimisha na kuhamasisha   jamii kuhusu umuhimu wa sensa hiyo  kwa kutumia mbinu na nyenzo  za kuwafikia wananchi wa rika zote na mahali  kote kupitia  vipindi vya radio,  televisheni ,  magazeti na  Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya  mitandao ya  kijamii  na jumbe za simu ili kufanikisha zoezi hilo.

Aliyasema  hayo Septemba 14, 2021 wakati akizindua wa  mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi  uliofanyika Jijini Dodoma, na kuvitaka vyombo hivyo vitenge muda na kuandaa vipindi mbalimbali vitakavyohamasisha na kuelimisha jamii kuhusiana na zoezi hilo nchini kote ambapo pia aliwataka Wasanii kutumia vipawa vyao katika utoaji wa elimuya sensa.

Rais Samia alieleza kuwa Sensa inaisaidia Serikali katika kufanyaji wa maamuzi  kuhusu ugawaji wa rasilimali za taifa zikiwepo za Maji, Umeme, Afya, Elimu na Ujenzi wa Miundombinu ya huduma za jamii, hivyo kuwataka wananchi kuhamasika na  kushiriki katika zoezi hilo ikiwa ni moja ya njia itakayotumika kutatua chamgamoto zinazozikabili jamii zao.

“Sensa pia itatusaidiaSerikalikufanya maamuzi katika ugawaji wa rasilimali za taifa na kupeleka hudauma mbalimbali kwa wananchiikiwemo afya elimu maji na ujenzi wa miundombinu kwenye maeneo mbalimbali kulingana na idadi ya watu na mahitaji ya maeneo hayo”. Alisema  Rais Samia

Pia aliongezea kuwa serikali kwa sasa haina idadi kamili ya majengo hivyo  sensa itakayofanyika 2022 itahususha kuhesabu majengo ili kurahisisha zoezi la ukusanyaji wa tozo za majengo  kwa kuwa makazi ni kipimo cha maendeleo.

“Aidha makazi ni kipimo muhimu cha maendeleo, kama mnavyofahamu tumeweka tozo ya makazi  kulipiwa kiasi fulani cha fedha, lakini hatukuwa na idadi sahihi ya nyumba na makazi ya watanzania nchini, kwa hiyo zoezi hili litakwenda kutupa  ubora na kujiamini kuwa tunafanya kazi kwa kujua idadi ya nyumba zilizopo”. Alisema Rais Samia

Pamoja na hayo Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu  Nchemba  alieleza dhumuni la  mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji  wa sensa ya watu na makazi   kuwa ni kukabiliana na mila na fikra potofu ambazo zitaweza kukwamisha zoezi hilo, hivyo kabla ya sensa kuanza ni  muhimu watu wapewe mafunzo kuhusu zoezi hilo.

Alibainisha kuwa Serikali imeshatoa maelekezo ya fedha zitakazotumika kuratibu na kusimamia shughuli zote za sensa ya Watu na Makazi  ili kuwezesha ukusanyaji wa taarifa  hizo kwa ufanisi, na matokeo ya sensa hiyo ni dira ya Wizara ya fedha kupanga mikakati ya kimaendeleo kwa wananchi.

Aidha Mtakwimu Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)  Dkt. Albina Chuwa, alifafanua kuwa sensa itakayofanyika mwaka 2022,  itakuwa ya kipekee  kuwahi kufanyika miongoni mwa zote tano zilizowahi kufanyika tangu uhuru kwani  walitumia teknolojia ya makaratasi kwa asilimia 95  na ya mwaka  2012 walitumia  teknolojia ya scanning ambayo ilitoa matokeo ndani ya miezi 3 Hivyo sensa ya mwakani itatoa matokeo ndani ya mwenzi mmoja.

Alisema katika sensa tano zilizopita uchambuzi uliishia katika ngazi ya Wilaya, hivyo sensa itayofanyika mwakani itahusisha ngazi za Kata, Vijiji na Vitingoji  ambapo watu na majengo yao vitahesabiwa  nchini kote na anwani ya kila makazi   kurekodiwa  kwenye Kazi Data ya Taifa.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.