Habari za Punde

TAMKO LA SIKU YA KUHIFADHI TABAKA OZONI

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ofisi ya Makamu wa Rais Taarifa kwa vyombo vya Habari Iliotolewa na Mhe. Selemani Said Jafo (MB.) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira katika Kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni 16 SEPTEMBA, 2021

 Ndugu Wananchi,

1.  Tarehe 16 Septemba mwaka huu  tutaungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni kama ilivyoagizwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Azimio lake nambari 49/114 la tarehe 19 Desemba 1998 kama kumbukumbu ya tarehe ya kutiwa saini Itifaki ya Montreal (Montreal Protocol - 1987) kuhusu kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni angani.

 Ozoni ni hewa iliyoko kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 10 hadi 50 juu ya ardhi. Kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya mnururisho  wa mionzi kama “Ultraviolet B” isifike kwenye uso wa dunia. Ujumbe wa mwaka huu ni Montreal Protocol - Keeping us, our food and vaccines cool”. Mkataba wa Montreal: Tulinde Afya ya Binadamu, Hifadhi ya chakula na kuhakikisha chanjo za Uviko 19 ni salama” Ujumbe wa maadhimisho haya una lengo la kukumbusha Jumuiya ya Kimataifa kuwa utekelezaji wa Itifaki ya Montreal kuhusu udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni umeweka mfumo thabiti wa kuhakikisha kuwa afya ya binadamu na mazingira zinalindwa ikiwemo tabaka la ozoni.

Vilevile, ujumbe huu unazikumbusha nchi wanachama wa Itifaki ya Montreal kuhakikisha kemikali mbadala (gesi) zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu ili kuchangia katika hifadhi ya chakula na jitihada za kupambana na janga la maambukizi ya Ugonjwa wa virusi ya Korona (UVIKO – 19) katika kuhakikisha kuwa chanjo zinakuwa salama.

                                                                                              

2.     Tabaka la Ozoni linapoharibiwa huchangia kuruhusu mionzi zaidi ya “Ultraviolet B” kufika kwenye uso wa dunia na hivyo kusababisha kuongezeka kwa magonjwa kama vile saratani ya ngozi, uharibifu wa macho yaani "mtoto wa jicho" unaosababisha upofu, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi. Aidha, madhara mengine ni kuharibika kwa mimea hasa mazao ya kilimo kutokana na kuathirika kwa maumbile na mifumo ya ukuaji. Vile vile, baadhi ya kemikali hizi husababisha kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi.

3.     Ili kulinda tabaka la Ozoni, Serikali za mataifa mbalimbali zilikubaliana kuunda Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka 1985. Mkataba huu unasisitiza ushirikiano katika utafiti, usimamizi na ubadilishanaji wa taarifa za hali ya Tabaka la Ozoni kutokana na kupungua kwa matumizi yake. Vile vile ilianzishwa Itifaki ya Montreal (Montreal Protocol) inayohusu udhibiti wa kemikali zinazomong'onyoa Tabaka la Ozoni na Itifaki hii ilipitishwa  tarehe 16 Septemba, 1987. Lengo kuu la Itifaki hii ni kupunguza uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong'onyoa Tabaka la Ozoni kwa ratiba maalum ili kutoa nafasi kwa mabadiliko ya teknolojia na upatikanaji wa kemikali mbadala hasa kwa nchi zinazoendelea.

Ndugu Wananchi,

4.     Aidha, baadhi ya kemikali mbadala zilizopendekezwa kuwa rafiki kwa Ozoni, zimegunduliwa kuwa zinachangia ongezeko la joto duniani na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.

5.      Itifaki ya Montreal imefanyiwa marekebisho mara tano (5) hadi sasa kufuatia ongezeko la orodha ya kemikali ambazo ama zina athari kwa tabaka la ozoni au ni rafiki kwa ozoni lakini zinachangia mabadiliko ya tabianchi. Marekebisho ya hivi karibuni yalifanyika Kigali, Rwanda mwaka 2016. Mwezi Novemba, 2019 Tanzania iliridhia Marekibisho ya Kigali yenye lengo la  kupunguza na baade kuondosha uzalishaji na matumizi ya kemikali ambazo hapo awali zilikuwa ni mbadala wa kemikali zinamong'onyoa Tabaka la Ozoni na baadae kugundulika kuchangia katika ongezeko la joto duniani na kusababisha mabadiliko ya tabianchi. Kupitishwa kwa marekebisho haya kutachangia katika jitihada za kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Baada ya kuridhia marekebisho ya Kigali Tanzania inafanya mapitio ya Kanuni za Usimamizi wa Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni za Mwaka 2007 ili kuhuisha marekebisho ya Kigali katika kanuni husika.

 

6.     Hadi sasa Itifaki ya Montreal imepata mafanikio makubwa ya kupunguza takribani ya kiasi cha asilimia 98 (takribani tani 1.8) ya uzalishaji wa matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni. Punguzo hilo la matumizi ya kemikali hizi limechangia katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu baadhi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni pia husababisha kuongezeka kwa joto duniani. Kwa mfano, kiasi cha kemikali kilichoondolewa katika matumizi ni takriban tani bilioni 135 za hewa ukaa na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, matokeo ya tafiti yanathibitisha kwamba kiwango cha kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni angani kinaendelea kupungua na inakadiriwa kuwa iwapo jitihada za utekelezaji wa Itifaki hii zitaendelea, Tabaka la Ozoni litarudi katika hali ya kawaida ifikapo katikati ya karne hii.

 Ndugu Wananchi,

           7.     Ili kufanikisha utekelezaji wa Itifaki ya Montreal, mwaka 1996 Serikali                            iliandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya                              kemikali hizi. Mikakati ya kitaifa ndani ya Programu hii ni pamoja na:

                             i)     Kujenga uwezo wa Taasisi zinazosimamia utekelezeji wa Mkataba;

                           ii)     Kuweka takwimu za kemikali hizo;

                          iii)     Kutoa elimu kwa wadau na kwa umma wa Watanzania kuhusu umuhimu wa Tabaka la Ozoni na hatari zinazolikabili;

                         iv)     Kusambaza habari kuhusu kemikali na tekinolojia mbadala;

                           v)     Kubadilisha tekinolojia katika viwanda vinavyotumia kemikali haribifu;

                         vi)     Kutoa mafunzo yanayolenga kuimarisha ujuzi katika sekta ya kuhudumia viyoyozi na majokofu;

                        vii)     Kuimarisha mbinu za upunguzaji wa matumizi ya kemikali husika kwa kuanzisha mtandao wa kunasa, kusafisha na kurejeleza vipoza joto;

                      viii)     Kuhamasisha na kuhimiza matumizi ya kemikali na tekinolojia mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni; na

                       ix)        Kuweka taratibu za kudhibiti uingizaji na matumizi ya kemikali zinazodhibitiwa na Mkataba wa Montreal.

 

8.     Hatua hizi zimewezesha Tanzania kuondosha kemikali hizi kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa na Itifaki kwa kudhibiti uingizaji wa kemikali husika kupitia mipaka ya nchi yetu.

 Aidha, wafanyabishara wengi ambao ni wauzaji wa kemikali husika wamekuwa na uelewa mkubwa na hivyo biashara ya kemikali mbadala imeendelea kukua mwaka hadi mwaka.

 

9.     Chini ya Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali haribifu, Serikali iliandaa Mpango wa Usimamizi wa Vipozi (Refrigerant Management Plan) ambao utekelezaji wake umefanyika kama ifuatavyo:

                 i.          Kuandaa Kanuni za Usimamizi wa Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la hewa ya Ozoni na zilianza kutumika tarehe 7 Desemba 2007 ambayo inafanyiwa mapitio ili kuhuisha marekebisho ya Kigali katika kanuni husika;

               ii.          Jumla ya mafundi mchundo wa viyoyozi na majokofu 500 wamepatiwa mafunzo kuhusu njia bora za kuhudumia vifaa hivyo bila kuathiri Tabaka la hewa ya Ozoni;

             iii.          Kusambazwa kwa Vitambuzi vya kemikali hizi vipatavyo 18 kwa ajili ya usambazaji katika vituo vilivyo mipakani mwa nchi yetu;

             iv.          Mashine 20 za kunasa na 5 za kunasa na kurejeleza  gesi chakavu zimenunuliwa na kusambazwa kwa karakana 20 na Vituo vitano vya Kikanda vya kunasa na kusafisha gesi chakavu za Majokofu na Viyoyozi katika vyuo vya VETA vya Mwanza, Chang’ombe - Dar es salaam, Kigoma, Mbeya na Mkokotoni-Zanzibar;

               v.          Jumla ya maafisa forodha na wasimamizi wa sheria 200 wamepatiwa mafunzo kuhusu udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la hewa ya Ozoni.

Ndugu Wananchi,


10. Hapa nchini maadhimisho haya yatafanyika kwa njia ya uelimishaji umma kuhusu Tabaka la Ozoni, faida zake, madhara ya kuharibika kwa Tabaka hili na matumizi salama ya bidhaa zenye kemikali rafiki kwa Tabaka la ozoni. Aidha, mafunzo yatatolewa kwa maafisa forodha na wasimamizi wa sheria kuhusu namna ya kudhibiti uingizaji wa kemikali zinazoharibu tabaka la ozoni. Hivyo kupitia kwenu wanahabari naamini elimu hii itaendelea kutolewa kwa jamii ya Watanzania ili kuongeza ushiriki wao katika kutekeleza jukumu hili muhimu la kulinda sayari hii.

 

11.    Ni muhimu tuzingatie kwamba juhudi za kila mmoja wetu zinatakiwa ili kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na bidhaa tunazonunua na kutumia majumbani au sehemu za biashara. Natoa wito kwa kila mwananchi kushiriki katika kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

          i.          Kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mitumba) na ambavyo vinatumia vipoozi aina ya R22 na R134. 

        ii.          Kuingiza nchini vipoozi mbadala na rafiki  kwa tabaka la Ozoni kama vile R209, R407, R404 na R717.

       iii.          Kununua bidhaa zilizowekwa nembo rasmi isemayo “Ozone friendly” yaani “sahibu wa Ozoni” au “CFC-free” ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni. 

      iv.          Kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni aina ya “CFCs” na “halon. Hivyo, ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mafundi ama mamlaka zinazohusika. 

        v.           Kuepuka  matumizi ya kemikali aina ya “Methyl bromide” kufukizia udongo, na badala yake kutumia mbinu mbadala na salama pamoja na mbinu tungamanishi za udhibiti wa wadudu waharibifu yaani “integrated pest management”.

      vi.          Mafundi wa majokofu na viyoyozi wahakikishe kuwa wananasa na kutumia tena vipoozi (refrigerants) kutoka kwenye viyoyozi, na majokofu wanayohudumia badala ya kuviachia huru visambae angani.  Aidha, mafundi watoe elimu kwa wateja wao juu ya njia rahisi za kutambua uvujaji wa vipoozi kutoka katika majokofu na viyoyozi wanavyotumia.

 

12.    Nawatakieni maadhimisho mema ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni.

 SELEMANI SAIDI JAFO (MB.)

WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS

 MUUNGANO NA MAZINGIRA

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.