Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akizungumza na wakazi
wa Kongwa kuhusu agenda ya mazingira mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya
siku moja Wilayani hapo, Kushoto ni Mkuu
wa Wilaya ya Kongwa Bw. Remidius
Emmanuel
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Bw. Remidius Emmanuel akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kongwa kabla ya
kumkaribisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Selemani Jafo kuzungumza nao. Waziri Jafo amefanya ziara ya
kikazi ya siku moja Wilayani hapo kuhimiza agenda ya mazingira.
Sehemu ya wakazi wa Kongwa
wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani) aliyefanya ziara ya siku moja
Wilaya hapo hii leo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Selemani Jafo ametoa rai kwa wakazi wa Kongwa kutoa msukumo wa dhati katika
agenda ya mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti rafiki kwa mazingira.
Akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Wilayani Kongwa Waziri Jafo
ametoa rai hiyo leo kwa wana Kongwa na kuwataka kuunga mkono juhudi za Serikali
za kuifanya Dodoma kuwa ya Kijani.
"Ndugu zangu Kampeni ya
kukijanisha Dodoma ni endelevu, na Kongwa ni sehemu ya Mkoa wa Dodoma, natoa
rai kwenu mpande miti kwa wingi, sambamba na kilimo cha Korosho kama zao la
kimkakati" Jafo alisisitiza.
Amesema agenda ya mazingira iende sambamba na upandaji wa miti kwa kila
kaya walau miti mitatu ikiwemo ya kivuli na matunda ili jamii iweze kunufaika
nayo sambamba na hifadhi ya mazingira ikiwa ni pamoja na ulinzi endelevu wa
miundombinu kama vile barabara na madaraja.
Amesema Kongwa ya sasa si sawa na Kongwa ya zamani kutokana na uharibifu
mkubwa wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu kama
Ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni na mkaa.
Waziri Jafo amesema Ofisi ya imezindua Kampeni Kabambe ya Kitaifa
ya Uhifadhi na Usafi wa Mazingira kwa lengo la kunusuru taifa na majanga yatokanayo na uharibifu wa mazingira.
Ametoa wito kwa kila kaya kupanda miti walau mitatu, ikiwa ni pamoja na
miti ya kivuli pamoja na matunda. Amesema upandaji wa miti utasaidia kuhifadhi
miundombinu ya barabara na madaraja.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Bw. Remidius Emmanuel amesema Wilaya ya yake
inaendelea kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kutunza mazingira ikiwemo
kutokata miti, kutoharibu vyanzo vya maji, kutovamia misitu, kupanda miti na
kuhifadhi visiki asili na takribani visiki hai 1,470,252 vimeainishwa na
kutunzwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment