Habari za Punde

DC MOYO: Aonya Wapotoshaji wa Zoezi la SENSA Iringa.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Mohamed Hassan Moyo akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za Wananchi wa Wilaya hiyo na kufanikiwa kutumia mkutano huo kuhamasisha zoezi la sensa kwa wananchi  itakayofanyika mwakani 2022 Nchi nzima Tanzania.
Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Iringa wakimsikiliza mkuu wa wilaya  Mohamed Hassan Moyo akihamasisha zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022

Na Fredy Mgunda,Iringa.

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo ameagiza kukamatwa watu wote watakaobainaka kupotosha UMMA kuhusu ukweli juu ya Sensa ya watu na makazi kwa lengo la kukwamisha zoezi hilo la kitaifa lenye faida kubwa ya maendeleo kwa taifa la Tanzania.

Akizungumza na wananchi katika nyakati tofauti kwenye Mikutano ya hadhara anayoendelea kuifanya Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa serikali haitokuwa tayari kushuhudia watu wanaopinga zoezi hilo kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mipango endelevu ya Serikali kwa wananchi wake.

Moyo alieleza kuwa mkakati wa Serikali kupitia Sensa hiyo ya watu na makazi itakyofanyika nchi nzima mwaka 2022 ni kushuhudia kila mtu aliyepo nchini siku hiyo anahesabiwa huku akieleza lengo mahususi la kufanya hivyo ni kutengeneza dira ya maendeleo kwa Taifa kwa kuwa na mipango thabiti itakayoweza kufanikisha kila mwananchi kupata huduma za msingi kwa ukaribu na ukamilifu zaidi.

Alisema kuwa kuna watu wanaojiita wanaharakati wamekuwa wakipita maeneo mbalimbali kupotosha UMMA juu ya zoezi la sensa ambalo limepangwa kufanyika mwakani kwa lengo la serikali kupata idadi kamili ya wananchi wa taifa la Tanzania.

“Nawaombeni wananchi kutowasikiliza wanaharakati hao ambao wamekuwa wanaposha wananchi wenginge juu ya zoezi la sensa huku wakidai kuwa zoezi hilo linalengo la kukibeba chama cha mapinduzi katika uchuguzi wa mwaka 2025 jambo ambalo sio la kweli na upotoshaji mkubwa”alisema Moyo.

Moyo alisema kuwa zoezi la sensa halina dini wala siasa bali ni zoezi ambalo linalengo la kujua idadi ya wananchi wa taifa la Tanzania ili kuiwezesha serikali kuandaa vizuri dira ya taifa kwa maendeleo ya wananchi wa Tanzania.

Hivyo mkuu wa wilaya huyo Mohamed Hassan Moyo aliwataka viongozi wa ngazi ya kitongoji,kijiji,kata,tarafa na wilaya kwa ujumla kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria kwa mwananchi yoyote atakayekuwa anapotosha kampeni ya SENSA wilayani humo.

Moyo alisema kuwa tangu taifa la Tanzania kupata uhuru mwaka 1961 zoezi la sensa ya watu na makazi limefanyika mara sita na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2012 hivyo wananchi wanatakiwa kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa makalani ambao watakuwa wanaandikisha.

Alisema kuwa wananchi wa wilaya ya Iringa wanapaswa kujitokeza kwa wingi na kuhamasishana kulipokea zoezi hilo la sensa ambalo linaumuhimu mkubwa katika kupanga mipango ya kimaendeleo ya taifa la Tanzania.

Moyo alitilia mkazo suala la kukamatwa kwa wanasiasa na wanaharakati ambao wamekuwa wakipotosha maswala muhimu yanayotangazwa na serikali kwa ajili ya maendeleo ya serikali.

Aidha mkuu wa wilaya Moyo aliwataka wananchi wa wilaya ya Iringa kuendelea kupata chanjo ya UVIKO 19 kama ambavyo serikali imeagiza na kuwataka kuachana na taarifa za upotoshaji zinazotolewa na wanasiasa na wanaharaka ambao halitakii mema taifa na wananchi kwa ujumla.

Awali baadhi ya wananchi walisema kuwa wamekuwa wakiambiwa na baadhi ya wanaharakati kuwa wasikubari kuhesabiwa na kutoa taarifa zao kwa mawakara wa zoezi hilo kwa kuwa zoezi la sensa litakuwa linafaida kwa chama chama mapinduzi (CCM) katika uchanguzi wa mwaka 2025.

Walisema kuwa wameambiwa kuwa kuanzishwa kwa zoezi la sensa kunalengo la kuisaidia CCM kuiba kura wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Lakini mara baada ya kupokea ujumbe wa mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo baadhi ya wananchi na viongozi wa vijiji,vitongoji,kata na tarafa walisema kuwa sasa wameilewa vilivyo kampeni hiyo na wapo tayari kuendelea kutoa elimu na umuhimu wa sensa ya watu na makazi kwa ajili ya faida ya taifa.

Walisema kuwa wananchi wote wanatakiwa kuwapuuza wanasiasa na wanaharakati ambao wamekuwa wakipotosha zoezi la sensa ya watu na makazi kwa ajili ya kutengeneza dira ya taifa ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.