Habari za Punde

 
RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi jana aliwaongoza Waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi mbali mbali katika Maulidi ya kuadhimisha Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) kitaifa yaliofanyika katika viwanja vya Maisara Suleiman mjini Zanzibar.

Sherehe hizo za kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambazo hufanyika kila mwaka Kitaifa hapa Zanzibar ni miongoni mwa kawaida na mila ya Waislamu wa Zanzibar.

Alhaj Dk. Mwinyi aliungana na Waislamu na wananchi hao wakiwemo viongozi mbali mbali wa Dini na Serikali pamoja na wananchi ambapo pia, Mama Mariam Mwinyi nae alihudhuria Maulid hayo akiwa pamoja na viongozi wengine wanawake wa Kitaifa.

Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Othman Ngwali alitumia fursa hiyo kuwakaribishwa wananchi wote pamoja na viongozi mbali mbali akiwemo Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi katika sherehe hizo za Maulid.

Katika Sherehe  hizo, Waislamu walisisitizwa suala zima la amani, umoja na mshikamano miongoni mwao na kutakiwa kufuata nyayo za Mtume Muhammad (S.A.W) ili wapate kuongoka hapa duniani na kesho akhera.

Akisoma khutba Sheikh Momammed Ali Mohammed kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, aliwataka  Waislamu kuwa kitu kimoja huku akiwasisitiza umuhimu wa  kusaidiana na  kuhurumiana kwa lengo la kupata rehema za Allah.

Aidha, alieleza kuwa ni jukumu la Waislamu kusherehekea siku hii adhimu pamoja na kufuata mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W) aliyokuja nayo.

Sherehe hizo za Maulid ambazo husherehekewa duniani kote, zilianza kufunguliwa na Qur-an tukufu iliyosomwa na  Ustadhi Hamdan Haji Hamdan kutoka Magogoni na baadae kuendelea kusomwa Milango ya Barzanj pamoja na Qaswida kutoka madrasa mbali mbali za Zanzibar  yakiwemo Maulid ya Hom kutoka Jumuiya ya Maulid ya Hom Mtendeni, Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo nayo yalikuwa kivutio kikubwa katika sherehe hizo adhimu.

Akisoma hisroria fupi ya Maulid hapa Zanzibar  Mshauri Mkuu wa Kamati ya Maandalizi Sheikh Sherali Chapsi  alisema kuwa shughuli hizo za Maulid hapa Zanzibar zimeanzishwa mapema mnamo mwaka 1926 kwa mashirikiano ya Waislamu wote wanaoishi hapa Zanzibar.

Aliongeza kuwa Jumuiya ya Milade Nabii hapa Zanzibar iliundwa kwa dhamira ya kuwaunganisha Waislamu na kusimamia sherehe ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), ambapo mwaka huu 2021 inatimiza miaka 96 ya usimamizi wa shughuli za Maulid, wakati huo huo Sheikh Sherali Chapsi akitumia fursa hiyo kumkabidhi Alhaj Dk. Mwinyi Qasweeda ya mwaka 1443 Alhijra.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.