Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Akihutubia katika Maadhimisho ya Mwaka Mmoja wa Uongozi wake.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Maadhimisho ya Mwaka Mmoja wa Uongozi wake Madarakani, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ili Taifa liweze kufanikisha matarajio ya kukuza Uchumi katika mwaka wa Pili wa Uongozi wa Serikali ya Awamu ya nane, halina budi kuendelea kudumisha amani, uwajibikaji pamoja na  watendaji kujenga uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Dk. Mwinyi ametoa indhari hiyo katika Hotuba aliyotoa kwa wananchi katika kilele cha maadhimisho ya kutimiza mwaka mmoja wa Uongozi wake, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip iliopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.

Amesema katika mwaka wa Pili wa Uongozi wa Awamu ya Nane, Serikali imekopa jumla ya Shilingi Bilioni 460 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambazo shiligni Bilioni 230 kati ya fedha hizo zitatumika kufanikisha miradi katika sekta mbali mbali za kijamii, ikiwemo Afya, elimu, maji safi na salama na umeme pamoja na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Alisema Shilingi Bilioni 230 zilizobaki zitatumika kwa ajili ya kulipia madeni ya Wazabuni, kulipa fidia mbali mbali pamoja na kulipia haki mbali mbali za wafanyakazi.

Alisema fedha hizo (bilioni 230) zitakazoingizwa katika shughuli za kiuchumi ni nyingi sana na ni wazi kuwa zitaleta faida kubwa kwa Taifa pamoja na kurahisha maisha kutokana na mzunguko wa fedha.

Hivyo, alisema matarajio hayo yatakamilika tu endapo wananchi wataendelea kudumisha amani iliopo, sambamba na watendaji kuanzia ngazi za chini za uongozi  kuwajibika ipasavyo na kufanya kazi zao kwa uadilifu, hususan katika suala la tenda.

Alieleza kuwa katika kipindi kilichopita miradi mingi ilishindwa kukamilishwa vyema kwa sababu ya Rushwa na kubainisha viashiria vilivyoanza kujichomoza na kusisitiza kwamba yeyote atakaejaribu kuchota fedha hizo hatomuachia.

Rais Dk.Mwinyi alitoa indhari juu ya matumizi stahiki ya fedha hizo, huku akiahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria watendaji wote  watakaojihusisha na udokozi au upotevu wa fedha hizo.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa alizochukua kufanikisha kupatikana kwa mkopo huo pamoja na ukaribu wake kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao umekuwa chachu ya kuondokana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya uamuzi wa kuwalipa fedha zao (kiasi cha Shilingi Bilioni 38.7) wahanga wote wa iliokuwa Masterlife, ikiwa ni hatua ya kuwaondolea usumbufu wa maisha wananchi masikini walioweka fedha hizo.

Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.