Habari za Punde

Haki Ndiyo Silaha ya Mahakama

 

Na.Adeladius Mkwega -Dodoma. 

Nadhani kati ya mwaka ya 2007 Mahakama Kuu kanda ya Iringa walikuwa na sherehe ya Siku ya Sheria. Siku hiyo Jaji Mkuu wa Kanda hiyo wakati huo Mheshimiwa Faki Jundu ndiye alikuwa anaisimamia kanda hiyo. Mahakama siku hiyo nakumbuka walikuwa na ugeni wa Jaji Mkuu wa wakati huo Marehemu Augustino Ramadhani.

Waandishi wa habari walialikwa kupitia Iringa Press Club chini ya Mwenyekiti wa Club Frank Leonard na Katibu wake kama sijakosea alikuwa ni Marehemu Daud Mwangosi. Mimi nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa lakini nikiandikia habari THISDAY na KULIKONI-Media Solution LTD ya Dar es Salaam na mimi nilijulishwa juu ya mwaliko huo.

Katika siku hiyo nilipofika nilibaini kuwa mahakama walitoa mwaliko pia kwa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa ambapo wanafunzi wote wa sheria wa mwaka wa tatu walifika wakiwa na mhadhiri wao Jaji Mstaafu Mwaikasu katika viwanja vya Judicial Square Iringa kwa wale ambao wanaifahamu Iringa ya zamani ni pale ilipokuwa makao makuu ya bendi ya tankuti Almasi Ochestra.

Yalizungumzwa mengi juu ya uhuru wa mahakama lakini ambaye alitoa somo lililonivutia sana ni Profesa Paramagamba Kabudi ambaye nilibaini kuwa Profesa huyu ni mwalimu mzuri sana, tena sana sana, shida yake labda, leo hii ni kucheza karata za siasa tu. Binafsi namuombea Mungu amsaidie sana ili acheze karata zake vizuri katika mchezo wa siasa maana siasani kulamba magarasa ni jambo la kawaida na inaweza kutibua sifa yake nzuri ya Ualimu.

Siku hiyo Profesa Kabudi alitumia zaidi saa moja kuelezea maana ya uhuru wa mahakama na hali ilivyokuwa kwa Tanganyika huru na hadi wakati huo akitolea mifano ya kesi nyingi na namna baadhi ya viongozi wa serikali walivyokuwa wakiingilia maamuzi ya mahakama na kukata utekelezaji maamuzi hayo kuna wakati hadi mahakimu walitakiwa kukamatwa na viongozi wa serikali.

Mada hii ya Profesa Kabudi ambaye nilikuwa namuona kwa mara ya kwanza uso kwa uso ilinipa picha kuwa huo uhuru wa mahakama unaosemwa leo hii kumbe wapo watumishi wa mahakama ambao walionja joto ya jiwe ya hicho sasa kinachoweza kusemwa ni uhuru wa mahakama, tena chini ya serikali ya Mwalimu Julius Nyerere mara baada ya uhuru ambapo ilomlazimu Jaji Mkuu wa wakati huo Ralph Windham kwenda kumueleza mwalimu Julius Nyerere juu ya uhuru huo wa mahakama na changamoto walizokuwa wakipata kutoka serikalini.

Mada ya Profesa Kabudi ilinishawishi na mimi kujifunza zaidi juu ya somo la uhuru wa mahakama ambapo kwa wakati huo nilimtafuta rafiki mmoja aliyekuwa akisoma shahada ya sheria na akiwa mwakilishi wa kitivo hicho katika vikao vya Seneti la Chuo cha Tumaini Iringa, Philipo Filikunjombe (sasa ni Dkt wa sheria ). Ndugu huyu alinipa Kitabu cha Profesa Chris Peter Mahina–Human Rights in Tanzania:Selected Cases and Materials ambapo kiliandika juu ya uhuru wa mahakama na mipaka baina ya Mahakama, Bunge na Serikali na msahauri mengi yanayaohusi haki za kibinadamu..

Nilipokisoma kitabu hicho mimi binafsi niliona uwezo wa Bunge na uwezo wa Mahakama inalingana lakini uwezo wa Serikali ni mkubwa kuliko mihimili hii miwili kwa kuyafanikisha mambo yake hasa kama kuna tija wanayotaka (serikali) kuyashinikiza kufanyika.

Ukiitazama mahakama namna ilivyo ni watu wanajifungua katika chumba huku wakisikiliza mashauri mbalimbali na kuyafanyia maamuzi na ndivyo ilivyo Bunge ni watu wanaokaa pamoja na wanajadiliana mambo tena kwa wakati maalumu na mwisho wanafanya maamuzi juu ya mambo hayo. Wote hawa Mahakama na Bunge wanatarajiwa kulindwa kwa kutumia Vyombo vya Usalama vya Serikali.

Je Mahakama inaweza kuwa huru? Upo kwenye kesi nje yupo jamaa anayekulinda akitokea Serikalini anakulinda/upo katika kikao cha Bunge na nje yupo bwana mkubwa mmoja anakulinda akitokea Serikalini.

Ili MAHAKAMA iweze kuwa huru na huru zaidi inatakiwa kwanza kulinda ile tabia ya muhimili huo ya kukaa ndani na kujifungua huku wakifanya maamuzi tena na tena nasema wanatakiwa kufanya maamuzi ya haki na sahihi kwa kila mmoja anayepeleka au kupelekwa hapo. Kama mambo yakiwa hivyo imani itakuwa kubwa kwa jamii nzima watatambua hilo na litasemwa midomoni mwa watu.

“Ahh jamani ukienda mahakamani wanakupokea vizuri. wanakusikiliza, hawana usumbufu na pia wanatoa maamuzi ya haki na kwa wakati.”

Kauli kama hii niulinzi mkubwa kwa jamii zaidi ya ulinzi wa Silaha na Mabomu. Hilo linaweza kuonekana hata katika mandhari ya mahakama watu wote wanaofika kusikiliza kesi, wanakaa kwa utulivu, shauri linaendelea kama shauri lina wasikilizaji wengi panatafutwa sehemu penye uwazi ambapo watu hao wote wanasikiliza shauri hilo bila ugomvi. Kwa kuwa mwenendo wa kesi utasikilizwa na wote hata kama mahakama inamtia hatiani mtuhumiwa fulani kunakuwa hakuna wa kulalamika maana mwenendo wa shauri umeonekana tangu mwanzo hadi tamati.

Hata vyombo vya ulinzi vitaweza kujifunza kuwa ukienda mahakamani wao wana utaratibu wao mzuri kabisa na vyombo vya ulinzi havitakuwa na kazi ngumu ya kuyalinda mazingira ya kimahakama. Kwa hilo litatoa picha kuwa mtuhumiwa kutafautisha kuwa hapa ni mahakamani kwa kuwa hata idadi ya polisi wachache,utulivu mkubwa anayesikilizwa pale ni mheshimiwa Jaji/ Hakimu tu. Hapa inalinda heshima ya mandhari ya kimahakama.

Kwa hiyo kutenda haki kwa mahakama hiyo ndio silaha nambari moja ya kuilinda mahakama isingiliwe na mihimili mingine. Kinyume na hapo mahakama inaweza kushindwa kufanya kazi yake vizuri. Mathalani Kenya, kuna wataki aliitwa Mkuu wa Jeshi la Polisi tena  kwa wito wa jaji hakutokea mahakamani.

Je kwanini hatokei mahakamani? anatambua kuwa mahakama haiwezi kufanya kazi yake vizuri mpaka ulinzi kutolewa nayeye.Sasa mathalani mahakama imeagiza mtuhumiwa aachiwe huru kwa mazingira kama hayo inawezekana mtuhumiwa ataendelea kukaa kololoni.

Ukweli ni kuwa sheria inafanya kazi vizuri sana kama kukiwa na hali ya utulivu tu panapokuwepo na vita migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kinachoweza kuokoa jahazi ni maridhiano tu. Hapo hakuna mahakama wala sheria.

“Ukitaka kujua nchi mbaya ndugu yangu kuwa na kesi mahakamani, kuwa na mgonjwa hospitali au shauri polisi.”

Haya ni maneno yanayozungumzwa mitaani yanapaswa kubadilika kwa kila mhusika kutenda haki.

Kwa kumalizia viongozi mahakama wafahamu kuwa wao ni watu wa maamuzi katika chumba cha mahakama, wanapaswa kuwa wavivu mno wa kuongea katika mikutano ya hadhara na mikutano ya siasa. Viongozi wa mahakama wawe wakaa kimya maana kwenye siasa mambo yakiharibika yatafika kwao kwa maamuzi .

“Kuna mambo mengi sana mnaweza kushirikiana na Muhimili wa Bunge na Muhimili wa Serikali bila ya wao kuwaingilia, na nyinyi kuwaingilia, na duniani ndivyo wanavyofanya hivyo, najua vile vitabu tulivyokuwa tunafundisha Chuo Kikuu Separation of Powers (Mgawanyo wa Madaraka wa Mihimili) wengine mnakuja nayo lazma ujenge mstari kabisa. Attoney General (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) akionekana amekaa karibu na Jaji Wambali mnaweza kusema independent of Judicial(Uhuru wa Mahakama) ipo hatarini au siyo si ndiyo mawazo hayo? Kwenye mitandao, mnataka ule mstari/ dunia ya sasa ni tofauti/dunia ya sasa ni tofauti ukijichimbia shimo lako linazidi kwenda chini, wenzako wanazidi kukufunika na mchanga.” Jaji Mkuu Ibrahimu Juma. Aliyasema hayo wakati akiwahutubia mawakili wapya 601 waliokuwa wakinukiwa uwakili wao, mbele yake hivi karibuni.

Kwa maelezo ya Jaji Mkuu alibainisha kuwa ushirikiano wa Mahakama na mihimili mingine ni jambo la msingi, mimi naona ushirikiano ni sawa lakini Jaji Mkuu atambue kuwa mahakama inapaswa kuwa mbali na mihimili mingine ili wakutane kwenye mashauri tu mahakanani. Nichukulie mfano kila kikao cha Bunge Jaji Mkuu yupo, hilo litafanya jamii kumzoea mheshimiwa wetu, Jaji lazima aogopwe. Nakumbuka zamani ukimuona Jaji Mkuu Taifa akimuapisha Rais haumuoni tena hadi baada ya miaka mitano.

Mahakama inapokuwa jirani na mihimili mingine inawezekana upande dhaifu kumezwa kwa haraka na hapo mahakama itashindwa kufanya kazi yake vizuri. Wakatoliki wanasema kuwa Padri huwa anakaa Parokiani, padre huyu hata kama anayo madhaifu yake ya kibinadamu anayeweza kuyajua ni yule anayeishi naye parokiani, siye wauumini wote kijijini bali padri tunakutana naye dominika (jumapili).

Nimalizie kwa kusema kuwa heri mahakama ikijichimbia shimo huko mahakamani na wakikutaka watakufuata huko huku mahakamani na ukiwataka unawatumia wito wanakufuata wewe.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.