Habari za Punde

Bei mpya za mafuta zatangazwa

Na.Mwashungi Tahir  Maelezo     8-2-2022

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi inaendelea kufidia bei katika bidhaa zote za mafuta hapa Zanzibar ili kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wake.

 

Hayo yamesemwa  na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Mbarak Hassan Haji, kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) wakati akizungumza na vyombo vya habari huko Ofisini kwake Maisara.

 

Alisema katika jambo hilo jumla ya shilingi 242 zinafidiwa na Serikali kwa bidhaa zote za mafuta ili kuendelea kuwahurumia wananchi katika  nishati hiyo.

 

Akitangaza bei za nishati ya mafuta kwa mwezi huu Mbarak alisema mafuta ya Petrol, Disel na mafuta ya taa imeshuka kwa mwezi huu ukilinganisha na mwezi uliopita.

 

Alisema bei ya Petroli kwa mwezi huu itauzwa kwa shilingi 2,298 tofauti ya shilingi 120 sawa na asilimia tano kutoka shilingi 2,418.

 

Kwa bei ya Diseli alisema itauzwa kwa shilingi 2,345 tofauti ya shilingi 70 sawa na asilimia tatu kutoka shilingi 2,415 ya mwezi uliopita huku upande wa mafuta ya taa kwa mwezi huu yatauzwa kwa shilingi 1,890 tofauti ya shilingi 46 sawa na asilimia mbili ukilinganisha na bei ya mwezi Januari ambayo ilikuwa ikiuzwa kwa shilingi 1,936.   

 

Hata hivyo alibainisha kuwa ZURA inapanga bei kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo kubadilika kwa wastani wa bei za uuzaji wa bidhaa hizo katika soko la dunia pamoja na soko la ndani kupitia bandari ya Dar es salam.

 

Hata hivyo, alisema ZURA inapanga bei kwa kuzingatia wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani kwa mwezi uliopita ili kupata kianzio cha kufanyika mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi huu.

 

Alisema jengine ni kuangalia gharama za uingizaji mafuta katika bandari ya Dar es salam, kuangalia thamani ya shilingi ya Tanzania kwa dola za kimarekani, gharama za usafiri, bima na premium hadi Zanzibar, kodi za serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

 

Aliwasisitiza wananchi kuwa bei hizo ndio bei halali na kuwahimiza kununua mafuta katika vituo vilivyokuwepo nchini na kudai risiti kila wanapopata huduma hiyo ili kuepuka usumbufu pale linapotoke tatizo. 

 

Akizungumzia utoaji wa risiti za kielektroniki za VFMS katika vituo vya mafuta alisema ZURA na ZRB watafanya kikao maalum ili kuweka utaratibu katika masuala ya mafuta na gesi.

 

“Zipo changamoto ambazo tunatakiwa tuzijadili kwa pamoja lengo ni kuona hakuna changamoto zinazowakumba watoa huduma, wananchi na hata katika ukusanyaji wa mapato katika maeneo yote ya nishati," alisema ofisa uhusiano Mbaraka.

 

Sambamba na hayo, alibainisha kwamba lengo la mamlaka hiyo ni kuhakikisha huduma hiyo inaimarika zaidi na kuahidi kwamba mamlaka itaendelea kutoa elimu kwa wananchi katika mambo yote ya nishati.

 

Mbarak akitolea ufafaunuzi suala la upangaji wa bei kwa nishati ya gesi alisema ZURA inaendeleoa kulifanyia kazi suala hilo na watatoa utaratibu wa kutoa bei ya nidhati hiyo kama wanayotoa bei  katika nishati ya mafuta.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.