Habari za Punde

Makamu wa Rais wa Tanzania Ziarani Nchini Uganda

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiongozana na mwenyeji wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wakiwasili katika uwanja wa sherehe wa Kololo uliopo Kampala Uganda kwaajili ya kuhudhuria hafla ya kutoa maamuzi ya mwisho ya uwekezaji (Final Investement Decision) katika mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga  nchini Tanzania (EACOP). Februari 1,2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitoa salamu za serikali ya Tanzania kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kutoa maamuzi ya mwisho ya uwekezaji (Final Investement Decision) katika mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga  nchini Tanzania (EACOP)



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango pamoja na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wakiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Nishati wa Tanzania na Uganda pamoja  wakuu wa Mashirika ya Petroli ya Uganda na Tanzania mara baada ya tamko la maamuzi ya mwisho ya uwekezaji (Final Investement Decision) katika mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga  nchini Tanzania (EACOP)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango pamoja na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wakiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Uganda Meja Mstaafu Jessica Alupo mara baada ya tamko la maamuzi ya mwisho ya uwekezaji (Final Investement Decision) katika mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga  nchini Tanzania (EACOP). 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 1 Februari 2022 amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kutoa maamuzi ya mwisho ya uwekezaji (Final Investement Decision) katika mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga  nchini Tanzania (EACOP). Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya sherehe vya Kololo vilivyopo Kampala Nchini Uganda.

Makamu wa Rais ameungana na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museven kushuhudia tamko la pamoja la Makampuni wabia wa mradi huo pamoja na mashirika ya petroli ya nchi za Tanzania na Uganda ya kuanza uwekezaji katika mradi huo.

Akizungumza katika hafla hiyo Makamu wa Rais Dkt. Mpango  amesema serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Bomba hilo ikiwa tayari imelipa fidia kwa wananchi ambao mradi unapita katika maeneo yao pamoja na kutoa kiasi cha shilingi bilioni 259.96 kwa shirika la maendeleo ya petroli Tanzania kwa ajili ya ushiriki katika mradi huo.  

Makamu wa Rais amesema kutokana na umuhimu mkubwa  wa mradi, wananchi wa Tanzania na Uganda wanapaswa kuwa wazalendo katika mradi huo ikiwemo kulinda bomba hilo litakalojengwa, kulinda mazingira na kutoa taarifa za haraka katika  kudhibiti viashiria vyovyote vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wa mradi huo. Makamu wa Rais amewataka maafisa forodha kutoka pande zote mbili kuharakisha uingizaji wa vifaa vinavyotumika katika mradi huo pamoja na kuwaasa wahusika wote wa utekelezaji wa mradi huo kuchukua hatua stahiki za kulinda mazingira ,kufuata sheria za kazi pamoja na haki za wananchi wa maeneo husika wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Aidha Makamu wa Rais amehimiza sekta binafsi kutumia fursa ya ujenzi wa bomba hilo kushirikiana na kampuni za kimataifa katika kutoa huduma mbalimbali na kuziomba kampuni za kimataifa kutoa fursa hizo ili kuwajengea uwezo na kuwapa nafasi wataalamu wa ndani hasa vijana.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amesema mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta utaongeza ukuaji wa uchumi ambao umeathiriwa na Uviko 19. Amesema mradi huo unatarajia kukuza biashara ,viwanda vya uzalishaji, kuongeza ajira pamoja na kuvutia wawekezaji mbalimbali ambao wanatarajiwa kuongeza teknolojia pamoja na ujuzi kwa wananchi wa Tanzania na Uganda.

Kwa upande wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni amesema ujenzi wa Bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima hadi Chongoleani utakua mkombozi wa usafirishaji kwa jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na baadhi ya nchi ikiwemo Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  kuwa nishati hiyo. Rais Museven amesema Tanzania na Uganda zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu ulioimarishwa na  biashara za kindugu hivyo mradi huo ni faida kwa pande zote mbili.

Amesema anafurahishwa na mradi huo kuelekea nchini Tanzania kutokana na Tanzania kujitoa katika changamoto za nchi zingine mara kwa mara tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  aliejitolea  kupambana utawala wa nduli Idd Amin kwa kuwasaidia wananchi wa Uganda pamoja na kupambana na  ukoloni wa nchi zingine ikiwemo za kusini mwa Afrika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.