Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi akutana na wanahabari Ikulu

 


STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

Zanzibar                                                                                      28.02.2022

---

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya maamuzi ya makusudi ya kupunguza kodi ya sukari ili kuondoa gharama ya bidhaa hiyo katika soko ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wananchi wa Unguja na Pemba.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Wahariri pamoja na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari nchini ikiwa ni utaratibu wake aliojiwekea wa kukutana nao kila ifikapo mwisho wa mwezi.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo imechukuliwa na serikali ili kupunguza mfumko wa bei hasa katika kipindi hichi cha kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Alisema kuwa hapo siku za nyuma sukari ilikuwa ikitozwa asilimia ya 15 kodi ya ongezeko la thamani ya bidhaa (VAT) na asilimia 25 kodi ya ushuru wa forodha (Import duties) ambapo kwa hivi sasa itatozwa asilimia 12.5 tu kati ya asilimia 25 ili kupunguza gharama katika soko, na kutoa wito kwa wafanyabiashara kuona nia njema ya serikali katika kuwasaidia wananchi Unguja na Pemba.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa wafanyabiashara wa bidhaa hiyo kuona umuhimu wa kutopandisha bei ya vyakula hapa Unguja na Pemba na kusema kuwa sukari imewekewa bei elekezi isizidi 1900 kwa Unguja na 2000 kwa Pemba tofauti ambayo inatokana na usafiri wa Unguja kwenda Pemba.

Hivyo, aliitaka Tume ya ushindani kutimiza wajibu wake kwa kupita kila duka kuhakikisha bei elekezi zinasimamiwa na watendaji wake wasipofanya kazi hiyo inavyotakiwa basi Serikali itachukua hatua dhidi yao kwani wamepewa jukumu kisheria la kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuzuia mfumko wa bei usiokuwa na sababu.

Rais Dk. Mwinyi pia alieleza azma ya Serikali ya kutumia vifaa vya kukusanya ushuru na kueleza madhumuni ya kutumia mfumo huo na kuwasihi wafanyabiashara kutodharau mfumo huo na kueleza kwamba utaratibu utafanywa ili wafanyabiashara kulipia vifaa hivyo kwa awamu.

Alisema hatua zitakazochukuliwa katika kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya biashara zao hususan mara baada ya kumaliza ujenzi wa masoko unaoendelea.

Pia, alieleza utekelezaji wa miradi inayotokana na fedha za UVIKO 19, na kusema kwamba miradi ya afya, elimu na maji, umemena uwezeshaji kazi zinakwenda na huo ndio ujenzi wa nchi.

Alisisitiza usafi wa mji sambamba na kujiandaa na mvua za masika zinazotarajiwa kunyesha, na kuzitaka Halmashauri kusafisha na kufanya usafi na kutosubiri mafuriko na Mkurugenzi yoyote ambaye hatowajibika basi atawajibishwa na Serikali.

Akieleza mafanikio ya mfumo wa Sema Na Rais (SNR), Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kwa asilimia 73 mfumo huo umeweza kupunguza malalamiko na changamoto zinazojitokeza katika jamii na kuwasisitiza wananchi kuendelea kuutumia mfumo huo.

Akijibu masuala ya Waandishi wa habari, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Wizara husika kuangalia suala zima la sheria ya Habari kwa vile imepitwa na wakati sambamba na kulitolea maelezo suala la shamba la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lililoko Makurunge huko Bagamoyo, Tanzania Bara.

Pia, alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuongeza mishahara na kulipa maposho yote ya wafanyakazi wa Serikali pale makusanyo yatakapoimarika.

Alieleza haja ya redio jamii kuhakikisha nazo zinafaidika na matangazo huku Idara husika ya Elimu kuhakikisha inaondosha usumbufu kwa wanafunzi katika kuwapatia stakabadhi zao kwa kuwapelekea maskulini mwao.

 

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.