Habari za Punde

Mhe Hemed azifariji familia za marubani waliopotea katika ajali ya ndege visiwa vya Comoro

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amezitaka familia za marubani waliopotea na Ndege ya Kampuni FLY ZANZIBAR iliyokuwa ikifanya safari yake kwenye visiwa vya Comoro kuwa na Subra katika kipindi hichi kigumu.

Hemed ametoa kauli hiyo alipofika kuifariji Familia ya mmoja  wa marubani wa ndege hiyo ADIL SULTAN KHAMIS  Al Mazrui nyumbani kwao Mbweni  Jijini Zanzibar.

Amesema Mtihani wa kupotea kwa Ndege hiyo ni katika mipango ya M/Mungu hivyo ni vyema kwa ndugu, marafiki na  Familia kuwa wamoja katika kipindi hichi kigumu.

Mhe. Hemed amesema Serikali kupitia Ubalozi wa Tanzania Nchini Comoro inaendelea kufanya jitihada za kuwatafuta wahanga wa tukio hilo na kuwataka wanafamilia na wazanzibari kwa ujumla kutoa Taarifa kwa kila wanachokisikia kupitia vyanzo tofauti vilivyopo nchini.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaombea faraja na Salama wahanga wa tukio hilo na kuitaka Familia hiyo kuwa tayari kupokea Taarifa Sahihi kutoka Serikalini kwani Serikali inafatilia kila kinachoendelea katika ajali hiyo.

Kwa upande wake Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Shekh Mahmoud Mussa Wadi amewataka wafamilia hao kuwa na Subra katika kipindi hichi na kuwataka watakapopata usahihi  wa Taarifa za tukio hilo kuripoti Ofisi ya Mufti kwa hatua zaidi.

Akitoa Shukran kwa niaba ya  Familia Baba Mzazi wa Ndugu Adil Sultan Bwana Sultan Khamis Al Mazrui  amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuona umuhimu wa jambo hilo na kuamua kuungana nao na kumtaka kuendelea kujumuika katika matukio ya kijamii jambo ambalo linajenga Imani zaidi kwa wananchi na serikali yao.

Wakati wa Mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amekutana na Uongozi wa Taasisi ya kuratibu ruzuku kutoka Mfuko wa Dunia (Global Fund Foundation) Ofisini kwake Vuga katika Kikao cha kujadili masuala mbali mbali yanayoendeshwa na Taasisi hiyo.

Katika kikao hicho Hemed  ameuhakikishia Uongozi huo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaongeza mashirikiano katika kufikia malengo yaliyokusudiwa na taasisi hiyo.

Sambamba na hayo Hemed amesema kuwa Taasisi hiyo imeisaidia sana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupambana na maradhi mbali mbali ikiwemo Malaria,Ukimwi na Kifua Kikuu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.