Habari za Punde

Serikali Yajipanga Kuboresha Uchumi Kupitia Sekta ya Madini

Na Beatrice Sanga, MAELEZO February 23

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema Serikali imedhamiria kuona Tanzania inanufaika na Madini yake, huku Wawekezaji wakipata manufaa kwa kuwekeza mitaji na ujuzi wao, ambapo mwaka 2017 serikali iliamua kufanya maboresho ya sheria  mbalimbali za madini  ili kuongeza mchango wa sekta hiyo  katika Pato la Taifa.

Ameyesema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, uliohusisha  washiriki 1,200 kutoka ndani na nje ya nchi  wakiwemo Mawaziri, Manaibu Waziri  Makatibu Wakuu na Mabalozi.

Dkt Mpango amesema maeneo yaliyozingatiwa katika maboresho hayo ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa nchi na wananchi katika mnyororo wa uchumi wa madini, na kuhakikisha uongezaji thamani unafanyika zaidi hapa nchini, ambapo Maboresho haya yote yameleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Madini.

“Kwa kuzingatia haya, Mpango wetu wa maendeleo wa miaka mitano (5) umeongeza lengo la mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025/26, ukilinganisha na kiwango cha asilimia 6.7 kwa mwaka 2020/21 Kwa upande wa thamani ya mauzo nje ya nchi kutokana na madini, lengo ni kuyaongeza kutoka dola za Marekani bilioni 3.4 mwaka 2020 hadi dola za Marekani bilioni 5.5 ifikapo mwaka 2025/26, Hatuna budi kushirikiana na kuhakikisha malengo haya yanafikiwa ili sekta hii iweze kuchangia zaidi jitihada za Taifa katika kupunguza umasikini.” Amesema Dkt Mpango

Aidha Dkt Mpango ameongeza kuwa serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo zilijadiliwa na wadau, ikiwemo malalamiko kutoka kwa wamiliki wa mashamba kutohusishwa  katika utoaji wa leseni za uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali, ambapo mpaka sasa tume ya madini inatoa leseni hizo kwa kutoa kipaumbele kwa wamiliki wa mashamba kote nchini.

“Mmeeleza hapa kuwa bado kuna changamoto nyingi ambazo baadhi mlizijadili katika mikutano iliyopita. Serikali imeendelea kuzifanyia kazi na kuzipatia ufumbuzi baadhi ya changamoto hizo. Kwa mfano, malalamiko ya wamiliki wa mashamba kutohusishwa katika utoaji wa leseni za uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Bulumbaka Gold Rush yamepatiwa suluhisho ambapo Tume ya Madini sasa inatoa leseni hizo kwa kutoa kipaumbele kwa wamiliki wa mashamba.” Amesema Dkt Mpango.

amesema Serikali pia imeongeza ufanisi katika utoaji wa leseni ambapo hivi sasa mwekezaji anaweza kupata leseni ndani ya miezi sita baada ya kukamilisha masharti na taratibu zote ikilinganishwa na hapo awali ambapo ingechukuwa hata miaka miwili na zaidi.

“Kutokana na juhudi hizi, hivi karibuni tumetoa leseni mpya za uchimbaji mkubwa na wa kati ambazo zimetolewa kwa kampuni ya uchimbaji madini ya Sotta, kampuni ya uchimbaji madini ya Kinywe ya Faru (Faru Graphite Mining) na kampuni ya uchimbaji madini ya Black Rock. ”Amesema Dkt Mpango

Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania (FEMATA), John Bina amesema licha ya sekta hiyo kuwa na mafanikio ikiwemo wachimbaji wadogo kuchangia asilimia 40 katika Sekta ya Madini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo  kukosa mitaji  ambapo suala hilo limekuwa likikwamisha shughuli za uzalishaji  madini licha ya benki kuonesha nia ya kukopesha lakini wamekuwa wakikopesha zaidi wafanyabiashara  na si wachimbaji

“Tunaipongeza STAMICO kwa kuanza kusaini mikataba na benki za CRDB, NMB, na KCB ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wanakopesheka , Benki zisijikite katika kufikiria katika madini hayo bali hata kwa yale viwandani” Alisema Bina

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.