Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ametembelea Familia za Warubani wa Kampuni ya Ndege ya Fly Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakiitikia dua ikisomwa na mmoja wa Familia ya Rubani Adil Sultan Khamis, baada ya kumaliza kutowa pole na kuifariji familia kwa kupotelewa na Kijana wao katika ajali ya Ndege iliyotokea Nchini Comoro hivi karibuni
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi walipofika nyumbani kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Abdalla Juma Mabodi,kumfariji kutokana na ajali aliyopata mtoto wake ambae ni Rubani wa Ndege wa Kampuni ya Fly Zanzibar Ashraf Andalla Mabodi iliyotokea Nchini Comoro hivi karibuni.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amezifariji familia ya Rubani Adil Sultan Khamis na Rubani Ashraf Abdalla Juma Mabodi kufuatia ajali ya ndege iliyotokea hivi karibuni huko Comoro.

Rais Dk. Mwinyi akiwa amefuatana na Mkewe Mama Mariam Mwinyi walifika nyumbani kwa familia ya Adi Sultan Khamis huko Mbweni na kuifariji familia hiyo huku akiinasihi kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hichi wakati taarifa sahihi zikitafutwa za raia hao wa Tanzania pamoja na abiria waliokuwemo katika ndege hiyo. aina ya Cessna Caravan 5HMZA

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi akiwa amefuatana na Mkewe Mama Mariam Mwinyi walifika nyumbani kwa familia ya Rubani Ashraf Abdallah Juma Mabodi huko Chukwani ambapo waliifariji familia hiyo huko Rais Dk. Mwinyi akiinasihi kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hichi wakati taarifa sahihi zikitafutwa juu ya tukio hilo.

Baba wa Rubani Asharaf Abdalla Juma Mabodi, Dk. Abdalla Juma Mabodi alimueleza Rais Dk. Mwinyi juhudi zinazoendelea kuwatafuta Marubani hao pamoja na abiria waliokuwemo katika ndege hiyo.

Aidha, familia hizo zilitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi pamoja na Mama Mariam Mwinyi kwa hatua walizozichukua za kwenda kuwafariji hasa katika kipindi hichi ambacho bado taarifa kamili hazijapatikana juu ya tukio hilo.

Mnamo Februari 27 ndege ndogo aina ya Cessna Caravan 5HMZA ikiwa na abiria 14 wakiwemo Marubani wa Tanzania wawili ilipotea katika rada kilomita 2.5 kabla ya kutua katika mji wa Fomboni, uliopo kisiwa cha Moheli ikitokea makamo makuu ya kisiwa cha Moroni.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar. OF RESPONSIBILITY ABUSE

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.