Habari za Punde

TAMWA Zanzibar Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani *Haki na Usawa wa Kijinsia ni Muhimu kwa Maendeleo Endelevu

 

Katika kuelekea maadhimisho ya siku wanawake duniani tarehe 8 Machi  Asasi za kiraia Zanzibar ambazo ni watetezi wa  haki za wanawake  zinaungana na wanaharakati wengine ulimwenguni  kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani kwa kuandaa shughuli ambazo zitatoa fursa kwa wadau  kukaa pamoja na kujadili changamoto na mafanikio ya wanawake hapa nchini.

Mwaka huu asasi hizo zilizo chini ya mtandao wa asasi za kiraia Zanzibar (CSO’s Networking Forum) zimekuja na Kauli mbiu isemayo  “Haki na Usawa wa Kijinsia katika Nafasi za Uongozi kwa Maendeleo Endelevu;” ambayo inasisitiza umuhimu wa kuchukua hatua katika kuhakikisha kwamba haki na usawa unazingatiwa katika ngazi zote za utoaji wa maamuzi.

Miongoni mwa shughuli ambazo zimeandaliwa na Asasi  hizo katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni pamoja na makongamano/mijadala ya wazi yenye lengo la kuimairisha na kukuza usawa wa kijinsia katika nyanja zote za maendeleo ikiwemo kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Pia kutakuwa na mjadala wa kuangalia nafasi ya wanawake wenye ulemavu hasa katika mazingira ya vyuo ambapo wanavyuo kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Zanzibar watajadiliana na kuangalia nini kifanyike ili kuhakikisha kwamba haki na usawa wa kijinsia kwa wote unapatikana.

Mada mbalimbali zitawasilishwa katika makongamano hayo ambayo yataanza tarehe 9 Machi, ikiwemo kuangalia mapungufu na mazuri yaliyopo katika sheria na miongozo inayohusiana na ushiriki wa wanawake katika masuala ya siasa na uongozi, ikiwa ni pamoja na kuangalia mapungufu yaliyomo katika katiba za vyama vya siasa katika kutimiza azma ya  kufikia asilimia 50/50 katika ngazi za uamuzi.  

Jamii  inapaswa  kuelewa umuhimu wa wanawake unaenda sambamba na ushiriki wao katika siasa na uchaguzi, kwani asilimia ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uchaguzi ni ndogo sana na hivyo hupelekea ushiriki wao katika nafasi za  uongozi pia kuwa mdogo.

Mathalan katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwa Zanzibar, jumla ya wanawake 216 walipendekezwa na vyama vyao vya siasa kugombea kupitia nyadhifa mbalimbali zikiwemo nafasi 61 za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Madiwani nafasi 74 na 81 Ubunge, wanawake walioshinda viti vya ubunge ni wane tu (4) sawa na asilimia 8, walioshinda viti vya uwakilishi ni wanane (8) sawa na asilimia 16 na waliofanikiwa kupata nafasi za udiwani ni 25 sawa na asilimia 23.

Pia tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa bado katika jamii zetu mwanamke anapewa nafasi finyu ya kushiriki katika ngazi za uamuzi, hivyo wakati umefika sasa dunia kutambua umuhimu wa wanawake katika uongozi na kuendeleza uwezeshaji zaidi wa wanawake ili wawezea kuingia katika vyombo vya maamuzi kwani wanawake wanapokua katika uongozi ni chachu ya kuondoa ubaguzi wa kijinsia na kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi ikiwa na lengo la kutoa fursa kwa wanawake, taasisi za kiserikali na asasi za kiraia  na wadau mbalimbali kupata fursa ya kukaa pamoja kujadili mafanikio na changamoto zinazomkabili mwanamke katika jamii na pia kutafakari jinsi ya kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo 2030.

Asasi zilizo chini ya mtandao wa asasi za kiraia Zanzibar (CSO’s Networking Forum) ni pamoja na Umoja wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Zanzibar Gender Coalition (ZGC), Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Shirika la Kupambana na Changamoto za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO), Mashirika ya Wasaidizi wa Kisheria Zanzibar (ZAPAO), Mtandao ya Kupinga Vitendo vya Udhalilishaji Zanzibar, Kijiji cha Watoto SOS, Jumuiya ya Vijana na Elimu Kaskazini (JUVIEKA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ ).

Dkt. Mzuri Issa,

Mkurugenzi,

TAMWA ZNZ

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.