Habari za Punde

Huyu Ndiye Dkt.Jakaya Kikwete.

 

Na.Adeladius Makwega-Arusha

Kabla ya Jakaya Kikwete kuwa mbunge wa Bagamoyo jimbo hilo lilikuwa likiongozwa na wabunge kadhaa akiwamo Kapteni Baruti Ramia, ambaye huyu alikuwa na nasaba na shekhe mkubwa sana wa dini ya Kiisilamu Mohammed Ramia, miongoni mwa wazee wa TANU ambao walikuwa ni marafiki wa karibu wa Julius Nyerere.

Jakaya Kikwete alipogombea jimbo la Bagamoyo kwa mara ya kwanza wengi wao wakisema kuwa alishinda kwa kishindo kikubwa mno hadi sasa rekodi hiyo haijavunjwa.

Wilaya ya Bagamoyo wananchi wake wakati huo ndani ya mawazo yao waliigawa katika maeneo mawili yaani Bagamoyo ya Bara na Bagamoyo ya Pwani. Watu wa Pwani ya Bagamoyo walikuwa jirani na bahari na wale waliokuwa mbali na bahari waliitwa watu wa Bara yakiwamo maeneo ya Msoga, Msata, Lugoba, Mboga na Chalinze.

Katika ushindi huo wa Jakaya Kikwete ulikuwa ni ushindi wa Bagamoyo ya Bara ambayo kwa desturi walikuwa ni watu wanaotazamwa kuwa duni mno kwani walikuwa mbali na Pwani. Baadhi ya watu wanaotazama siasa za eneo hilo kitendo cha kutenganisha Bagamoyo na Chalinze ukiondoa sifa za kawaida pia hii dhana ya Ubara na Upwani wengine wakiitaja.

Kwa hiyo kitendo cha Jakaya Kikwete kushinda kilikuwa ni kitendo cha ushindi kwa watu wa bara ambapo kimaendeleo Bagamoyo ya Bara ilikuwa nyuma kwani hata kuitika waliitika Bagamoyo ya Pwani.

Bagamoyo ya Bara ilikuwa mbali na bahari huku pia ikiwa mbali na maji. Bagamoyo ya Bara ilipata tumaini na kuondolewa kero ya kupata maji safi ya kunywa aliposhinda mtoto wao wa Bara (Msoga) Jakaya Kikwete japokuwa pia wazazi wake waliishi Bagamoyo ya Pwani.

Jakaya Kikwete aliandaa mkutano wa kuwashukuru wapiga kura wake, hapo kilipikwa kilichopikwa, wakacheza ngoma na kunywa huku mbunge Jakaya Kikwete akiwashukuru nduguze kwa kumchagua.

Kwa desturi Wakwere, Wazaramo na makabila mengi ya Pwani huwa ni wachangamfu, wapenda sherehe, burudani na ngoma. Hii ni sehemu ya maisha yao na utamaduni. Ngoma ya Bigililo na Bugi zilitumbuiza.

Jakaya Kikwete alipanda jukwaani na kusalimia nduguze kwa salama ya Kikwere.

“Jamani Goya.”

Wapiga kura wakajibu Goya.

“Jamani zile ahadi nilizoahidi, nataka kuzitekeleza, sasa nawaulizeni katika ahadi mbili za Maji na Umeme, Mimi nataka nianze na moja nikisema zote mbili nitazifanya kwa pamoja itakuwa ngumu sasa nianze na ipi?”

“Mwolonda chianduse mazi ama umeme.”

Akimaanisha mnataka nianze na maji au nianze na umeme

Wananchi wakamjibu mbunge wao kwa shangwe

“Cholonda umeme, chimelemete.”

Wakimaanisha tunautaka umeme ili tumelemete.

Kweli mbunge Jakaya Kikwete alipambana na kupatikana kwa umeme katika baadhi ya maeneo ya jimbo lake.

Jakaya Kikwete alikuwa mbunge mfanya vikao na wananchi wake, alipokamilisha hilo akafanya mkutano tena na wapiga kura wake.

“Sasa mulenge wa dimwe kwa dimwe, tayari?”

“Enaaa!”

Akimanisha sasa mbaramwezi ya mchana na usiku ipo tayari?

Ndiyo!

Baada ya hapo ndipo maji yakafikishwa katika jimbo hilo ambalo baadaye likagawanywa na kuwa majimbo ya Bagamoyo na Chalinze.

Alipokamilisha maji alifanya mkutano na wananchi wake

Akasema

“Maze mwongwa?” 

Maji mnakunywa?

“Maze chongwa”

Maji tunakunywa

Idadi ya watu inaoongezeka, inawezekana mbunge wa sasa anapambana na changamoto ambazo Jakaya Kikwete alipambana nazo , shida kubwa ni kuongezeka kwa idadi ya watu tu. Ndiyo maana mabomba ya zamani yanafukuliwa na kuwekwa mabomba makubwa yanayopitisha maji mengi kukizi mahitaji ya sasa.

Mwanakwetu huyo ndiye Jakaya Kikwete namna alivyokuwa mbunge. Baadaye akawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiongoza Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, ndani yake ikiwa PWANI na BARA ile ya Bagamoyo ya Shekhe Mohammed Ramia.

“Mulenge wa dimwe kwa dimbwe, tayari?”

Enaaaaaa!

Wakwere na watani zenu mpo?

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.