Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman
Abdulla akishuhudia Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw.
Abdallah Hamis Mitawi akitia saini mkataba wa makabidhiano ya eneo la mradi kwa ufukwe wa Sipwese, Pemba hafla
iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi leo Aprili 29, 2022.
Anayeshuhudia ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Bw. Dustun Shimbo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed
Suleiman Abdulla amesema utekelezaji wa miradi upande wa Zanzibar ni matunda ya
ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Amesema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini
wa makabidhiano ya eneo la mradi kwa
ufukwe wa Sipwese, Pemba kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi ambapo mradi huo
utatekelezwa na Kampuni ya Dezo Civil Contractors Co. Limited.
Mhe. Hemed alisema kuwa SMZ inafarijika kuona
mradi huo unaanza kutekelezwa kwa vitendo na kwamba utaleta manufaa makubwa kwa
wananchi watakaonufaika na mradi huo.
Pia alitumia nafasi hiyo kutoa pongeza na
shukrani kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango pamoja na Ofisi yake kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa SMZ.
Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi
ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Bi. Mary Maganga, alisema tathmini katika
ufukwe wa Sipwese ilionesha kuwa maji ya bahari yameingia katika maeneo ya
kilimo cha mpunga na wananchi wa Shehia ya Mkungu, Kijiji cha Sipwese eneo la
kwa Mgogo.
Mitawi alisema kujaa kwa maji haya pia
yamesababisha kukatika kwa mawasiliano kutoka upande wa pili takribani kilometa
3.360 ambako ndiko wananchi
wanafuata huduma za jamii kama vile shule hali inayosababisha watoto wa shule
kuvuka maji shingoni kuweza kuifikia shule.
“Mmomonyoko
wa fukwe zilizo katika Bahari ya Hindi kwa upande wa Tanzania Bara na Tanzania
Visiwani umeendelea kuwa ni changamoto katika maeneo mengi ya fukwe na umeanza
kuleta athari katika baadhi ya maeneo kwa kusababisha uharibifu wa miundombinu
iliyopo kama vile barabara, majengo, makazi ya watu na madaraja.
“Hali
hii imesababisha Serikali kutumia fedha nyingi katika kukarabati miundombinu
iliyoharibiwa, Fedha ambayo ingeweza kupelekwa katika maeneo mengine muhimu kwa
ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijami,” alisema Mitawi.
No comments:
Post a Comment