Habari za Punde

Balozi wa China ZANZIBAR

Na Mwandishi wetu, Zanzibar Jumanne Mei 24,2022

Balozi mdogo wa Jamhuri ya watu China aliyepo Zanzibar Bwana Zhang Zhisheng amesema Jamhuri ya watu wa China itachukua kila juhudi kuhakikisha kuwa uhusiano wa kihistoria baina ya nchi yake na Zanzibar katika sekta ya habari unaendelea kuimarika kwa maslahi ya nchi hizo mbili na wananchi wake.

Bwana Zhang Zhisheng amesema hayo leo katika mazungumzo kati yake na uongozi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar yaliyofanyika katika ofisi za Idara ya Habari Maelezo zilizopo Rahaleo mjini Unguja.

Amesema mahusiano baina ya China na Zanzibar katika masuala ya habari yalianza tokea mara tu baada ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1964, ambapo Jamhuri ya watu wa China ilikuwa ikitoa filamu zenye maudhui ya kuwahamasisha wananchi wa Zanzibar kufanyakazi kwa kujitegemea na kusahau kufanya kazi walizokuwa wamezizowea kabla ya Mapinduzi yaliyowakomboa wanyonge.

Alisema wakati huu ambapo China imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi, Zanzibar na Tanzania kwa jumla inayo nafasi ya kipekee kujifunza mbinu na mikakati ambayo China imetumia hadi kufikia kuwa moja kati ya mataifa yenye nguvu kiuchumi duniani.

Amesema ameridhishwa na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya nane na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha sekta za kiuchumi na kijamii na kwamba nchi yake imeshafanya mazungumzo na Serikali ya Zanzibar kuona namna itakavyoshirikiana nayo katika sekta tofauti ikiwemo sekta ya Habari.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Ndugu Hassan Khatib Hassan ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa misaada yake mbali mbali inayotoa katika kusaidia kuimarisha sekta ya Habari Zanzibar

Amesema ni Dhahiri kwamba wananchi wa Zanzibar wanayo mengi ya kujifunza kutoka China kutokana na mafanikio makubwa ambayo nchi hiyo imeyapata na kwamba vyombo vya habari vinaweza kuwa moja miongoni mwa njia muafaka zitakazosaidia kufikisha elimu hiyo kwa umma.

Mkurugenzi wa Habari Maelezo amesisitiza haja ya kuendelea kushirikiana katika kubadilishana taarifa na namna ya kuzifikisha taarifa hizo katika ngazi za chini, ambako wananchi wanayo mahitaji makubwa ya taarifa hizo.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Idara ya Habari Maelezo Bwana Yussuf Omar Chunda.

Imetolewa
Idara ya Habari Maelezo ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.