Habari za Punde

UTANI WA WARANGI

Na.Adeladius Makwega-DODOMA                                                                                              

Warangi ni kabila la kibantu linalopatikana katika mikoa ya katikati ya Tanzania ambayo sasa ni sehemu ya Dodoma. Kwa mujibu wa makadilio ya idadi ya watu ya mwaka 1999 kabila hilo lilikuwa na watu wanaofikia 350,000.

Jina lao linafahamika kama Warangi au Kirangi. Kama ilivyo kwa makabila mengi yanafanya utani, pia warangi hufanya utani katika sehemu tatu kwanza miongoni mwa wanakaya (familia) yao ambapo utana huu unaitwa BERESI. Lakini utani mwingine baina ya koo na koo, unafahamika kama UTERO.

Mambo haya ya BERESI na UTERO yamekuwa yakifanyika kwa karne kadhaa sasa ndani ya kabila hili.

Kwa upande wa BERESI, mathalani bibi anaweza kumuita mjukuu wake wa kiume kama MOSI WANE akimaanisha mume wangu. Bibi huyu anaweza kuwa wa upande wa mama au wa baba, yote hiyo ni aina ya utani ndani ya Warangi.

Utani mwingine wa BERESI ni wa mabinamu, hapa yanaweza kusemwa mengi mno, mathalani:

“Baba yako ni fukara sana, bila ya babu yangu kumuonea huruma baba yako na kuruhusiu binti yake aolewe na baba yako, wewe usingalizaliwa kabisa. Kwa hiyo wewe unatakiwa kumshukuru mno babu yangu.”

Anayeambiwa maneno hayo anaweza kujibu kwa kusema kuwa:

“Kama baba yangu angekuwa fukara basi asingaliweza kuoa, sisi ni matajiri kuliko nyinyi na ndiyo maana tumeweza kulipa posa na kuoa kwenu.”

Utani huu unaweza kwenda mbali mno kati ya binamu wa kike na wakiume hadi wakafunga ndoa. Ndoa ya binamu na binamu kwa Warangi ni halali.

Utani kwa Warangi pia huwa baina wa wifi na wifie, hapo yanaweza yakasema maneno mengi 

“Wewe unasema watoto wa kaka yako wachafu, mimi nitawezeja kuwaogesha watoto na wewe wasafi kama kaka yako anashindwa hata kununua sabuni ?”

Utani kwa Warangi unafanyika hata siku ya harusi ambapo upande wa bwana harusi unapofika kumfuata bibi harusi wanaweza kuimba wimbo huu.

“Seyi sama turkunguvala, vene n’gombe twingire, tiji twikale.”

Wakimaanisha kuwa tupisheni njia sisi ndiyo tuliolipa posa, tulicholipa ndicho chenye nguvu, tupeni kiti, sisi ni washindi. Maneno haya yanaweza kujibiwa na upande wa bibi harusi kuwa sawa mmelipa ng’ombe lakini wachache sana, kwanza tunaweza kuwarudishia ng’ombe zetu na sisi kuondoka na binti yetu.

Upande wa bwana harusi unaweza kusema kuwa chakula kilichopikwa hakijapikwa vizuri na kibichi.

Utani mwingine wa Warangi ni wa UTERO baina ya koo na koo, chanzo kikubwa cha utani huo ni mipaka baina ya ukoo mmoja na ukoo mwingine. Hapo huwa kuna maneno mengi ya utani juu ya koo fulani namna ilivyo.

Utani baina ya koo moja na nyingine inaaminika kuwa uliongezeka kutokana na kufanya kazi baina ya koo na koo .

Mathalani ukoo wa Vanazya na Vasalu, Vakanya(Varimbo) na Vafuchu, Visi na Vafuchu, Vanjeja na Vawino,Vanyau na Vaombe, Vasongo na vaomba, Vivira na Vachao na Vanajimba na Varamboa.

Japokuwa utani huu haupo sana kwa sasa kutokana na ujio wa dini. Hasa dini ya Kiisilamu ilifika mapema eneo hilo na kuwa sehemu ya utamaduni wa Warangi.

Dini nyingi zilipiga marufuko Matambiko na Utero. Wakoloni hao wakaleta mahakama na polisi ambao walisababisha utani huo ukaondoka na yule aliyefanya hivyo alishitakiwa.

Aina ya tatu ya utani kwa Warangi ni ule wa kabila hilo na makabila mengine. Warangi hufanya utani na makabila kama vile Wahehe, wa Iringa, Wanyiramba wa Kiomboi. Ikiaminika kuwa chanzo cha utani huo ni vita baina yao.

Wahehe waliwahi kuwavamia Warangi mara mbili huku wakiteka mifugo na kuondoka nayo mara zote Warangi walipigwa.

“Tuliweza kuwavamia na kuchukua mifugo yenu kwa kuwa mlikuwa wadhaifu.” Anasema H.J KIVINA katika andiko lake lenye kichwa–FURTHER NOTES ON RANGI UTANI-UTANI RELATIOSHIP IN TANZANIA VOLUME SEVEN EDITED BY SPEPHERN A.LUCAS  wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 1976.

Kutokana na ujio wa wakoloni ugomvi huo ulipotea na Warangi wakasahau uadui wao na kuwa ndugu, wakawa watani hadi leo.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.