Habari za Punde

Furaha ya Mheshimiwa Jackline Ngonyani.

Na.Adeladius Makwega-DODOMA.

“...Elimu ya kidato cha tano na sita, vijana wetu wanaotoka vijijini kwenye shule za kata wanafaulu kwenda kwenye mikoa ya mbali, mhe Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzama na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) anaguswa sana na tatizo hilo la watoto pamoja na wazazi wanaopata shida kutokana na ukweli kwamba hakuna shule za kidato cha tano na sita katika kata zetu. Kwa sasa wanafunzi wa kidato cha tano ni takribani 90,000 na wa kidato cha sita ni 56,000 huku mahitaji ya fedha ni bilioni 10.3, ili kupunguza gharama za watoto hao, mheshimiwa rais, kama aliivyoielekeza wizara yangu amependekeza kufuta ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.”

Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mipango na Fedha.

Mara makofi na vigegele vinasikika na wimbo unaanzishwa

“Tuna imani na Samiaaa oyaa oyaa oyaa…”

Gafla inasikika sauti ya Spika wa Bunge mheshimiwa Tulia Ackson,

“Mheshimiwa Jackline ! Mheshimiwa Jackline ! Mheshimiwa Jackline Ngonyani !. Waheshimiwa wabunge tafadhali ! Tafadhali ! Tafadhali. Simameni tu, mpige makofi, habari za nyimbo humu hairuhusiwi.

“Kwa kwa ’kwa…” Makofi yanasikika.

Yote hayo ni ya Juni 15, 2022 ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati mheshimiwa Mwigulu Nchemba Waziri wa Mipango na Fedha akisoma Bajeti Kuu ya Serikali.

Wimbo huo wa pongezi wa CCM uliimbwa na wengi, pengine Jackline Ngonyani ndiye aliyeanzisha na wengine kuitikia kutokana na midadi ya furaha ya mapendekezo hayo ya serikali ya kuondoka karo kwa kidato cha tano na sita.

Hakuna anayechukizwa na maamuzi ya serikali inapompunguzia mzigo mwananchi wake, kila mmoja anapaswa kushukuru. Hakuna Mtanzania ambaye hafahamu umuhimu wa elimu bure kwa kuwa wengi wamenufahika na elimu bure tangu wakati wa ujamaa.

Furaha ya kuondoa karo kwa kidato cha tano na sita inaweza kuingia shubiri, kama hali itakuwa kama ilivyo elimu bure ya sasa tangu darasa la kwanza hadi kidato cha nne.  Maana wanafunzi, wazazi / walezi, walimu, kamati/bodi za shule na hata viongozi wa ngazi zote wanatambua changamoto kadhaa zilizopo.

Kwanza matumzi ya shule ni mengi kuliko fedha inayoingia, mfano pesa inayopokelewa tangu januari hadi juni kwa elimu bure haitoshi kabisa kwa matumizi ya shule hizo.

“Pesa hiyo ikikusanywa bila ya kutumiwa kwa miezi sita ndiyo inatosha tu kulipia gharama za vifaa vya maabara kwa ajili ya mitihani ya vitendo ya masomo ya sayansi pekee, wapi pesa ya kulipia mitihani ya mock? Wapi pesa ya kulipia chaki ? Wapi pesa ya kulipia karatasi? Ipo wapi pesa ya kulipia UMISETA? Ipo wapi pesa ya kununua dawa za sanduku la huduma ya kwanza lenye sodo za wasichana shuleni?”

Hayo ni maswali machache miongoni mwa orodha ndefu ya maswali juu ya elimu bure ya sasa ambapo mtunzi wa kitabu chenye majibu bado hajamaliza kazi hiyo. Kumbuka kuwa kabla ya mapendekezo haya mapya wanafunzi wa kidato cha tano na sita shule za umma walikuwa wakilipa karo ya shilingi 70,000/ kwa mwaka.

Kwa mkulima wa miwa katika kijiji cha Ikangao–Ketaketa Ulanga mkoani Morogoro mua mmoja kwa jumla shambani unauzwa shilingi 500/-, kwa hiyo miwa 140 inatosha kwa fedha ya karo ya mwanafunzi wa kidato cha tano.

Pesa hiyo ni bei ya temba mmoja anayeuzwa kati ya shilingi 10,000-13,000/-kijijini Kilimatinde Manyoni-Singida, huku jogoo mmoja anauzwa kati ya shilingi 17,000-25,000/- hapo Muhalala-Manyoni Singida. Ndiyo kusema temba saba na jogoo wanne wanatosha kulipa karo ya wanafunzi wawili wa kidato cha tano katika shule za umma kwa sasa. Binafsi nina imani kuwa hoja ya kulipa karo siyo tatizo, hoja ni maboresho ya elimu yetu kwa yale majukumu ya serikali kama katika vifaa vya maabara, madawati, zana kufundishia, vitabu na maboresho ya maslahi ya walimu.

Walimu wengi katika shule za umma zenye kidato cha kwanza hadi cha sita, fedha hii ya karo iliwasaidia mno kutumia kununua vifaa kadhaa vya uendeshaji wa shule wakati wakikusanya fedha ya elimu bure ambayo inafika shuleni kidogo kidogo.

Jambo hili halina siri kwa kuwa shule hizi ni zetu, walimu ni ndugu zetu, wajumbe wa Bodi/Kamati za shule ni ndugu zetu, taarifa za hali ya fedha za shule zetu zinafahamika siyo uchawi kwa kuwa zinasomwa katika vikao vya wazazi.

Hali ya kifedha ya shule nyingi za umma kwa sasa zinavuka mwaka zikiwa na madeni kwa wazabuni mijadala kwenye kamati /bodi za shule ni madeni tu, hoja ikiwa ni hii hii ya elimu bure ya sasa ambayo mara zote husindikizwa na makofi na shangwe.

Kwa hiyo kuondoa karo kwa kidato cha tano na sita kwa shule za umma kutaongeza madeni kwa wazabuni na watoa huduma katika shule zetu, hilo litafanya wazabuni wengi kusitisha huduma, wakuu wa shule na bodi watakuwa hawana pesa za kuokoa jahazi, hali ya shule itakuwa mbaya, wale walimu wakuu, wajumbe wa bodi za shule wataanza kuyakataa majukumu kwa namna mbalimbali kama vile ugonjwa na wazazi wenye uwezo watakimbiza watoto wao katika shule za binafsi.Huko watabaki watoto wa masikini ambao watakuwa hawana namna.

Labda pesa ya elimu bure iongezwe mara tatu kwa kila kichwa cha mwanafunzi kwa mwezi kama inatolewa shilingi 1500/- basi iwe shilingi 4500/- kwa mwezi. Hata hiyo pia ni pesa ndogo sana ila kwa kuanzia tunaweza.

Hapa tunaweza kutolea mfano mdogo kwa watoto wa kike, gharama ya sodo ambayo inatakiwa kuwepo katika sanduku la huduma ya kwanza ni kati ya shilingi 2000/-4500/-Kiasi hicho kikizidishwa tu na idadi ya wanafunzi 500 wa sekondari ambao ni wahitaji utapata shilingi 1,500,000/- kwa mwezi mmoja tu. Je pesa inayatolewa kwa elimu bure kwa mwezi ni kiasi gani? Mwanakwetu ukishiriki vikao vya wazazi vya shule inasikitisha.

Pili pesa ifike kwa wakati na malipo yasiwe na changamoto za mifumo.

“Ohhh sijui tunafunga mwaka sasa malipo yamesimama.” Haya yatakwamisha makusudio mazuri ya serikali.

Kwa hakika mapendekezo hayo elimu ya kidato cha tano na sita bila karo yalipaswa kungoja kwanza, heri pesa hizo zinazoingizwa huko zingetumika kuboresha elimu bure ya darasa la kwanza hadi kidato cha nne, changamoto hizo zingefanyiwa kazi na hilo lingeongeza idadi ya wnafunzi wanaofaulu kidato cha nne ndipo elimu kwa kidato cha tano na sita ianze kuwa bure.

Binafsi nina imani kuwa furaha ya Mheshimiwa Jackline Ngonyani, wote walioitikia wimbo huo na hata mimi na wewe itakamilika kama haya machache ya leo yatafanyiwa kazi.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.