Habari za Punde

Jamii yatakiwa kutowaficha watu wenye ulemavu wakati wa Sensa

 Na.Andrew Chimesela.Dar Es Salaam.

Kuelekea zoezi la sensa ya watu na Makazi Agosti 23 mwaka huu, jamii imeaswa kutowaficha watu wenye ulemavu badala yake wawawezeshe kuhesabiwa ili serikali ipate takwimu sahihi za kundi hilo kwa faida yao na taifa kwa jumla.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati ya watu wenye ulemavu Mkoa wa Morogoro Bi. Magtagres Mkanga Agosti 18, 2022 wakati akifunga kikao cha wajumbe wa kamati hiyo  kilichofanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Bi. Mkanga amewataka wazazi ama walezi wa watu wenye ulemavu wakishirikiana na wenyeviti wa Mitaa ama vitongoji kutowaficha watu wenye ulemavu ifikapo Agosti 23 mwaka huu ili Serikali kupata takwimu sahihi za watu wenye ulemavu zitakazosaidia mipango yake lakini pia takwimu hizo zitasaidia utekelezaji wa mipango ya Kamati hiyo waliojiwekea.

“nasisitiza suala la watu wenye ulemavu wasifichwe na hizo familia husika au na hao wenyeviti wa mitaa husika” amesema Bi. Mkanga

“...lakini pia hapa ndipo itakaposaidia action plan yetu ili tujue exctly tuna watu wenye ulemavu wangapi Mkoa huu na wa aina zipi” amesisitiza Mwenyekiti huyo.

Akitoa taarifa ya Mkoa kuhusu watu wenye ulemavu, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro Bi. Jesca Kagunila amesema Mkoa wa Morogoro kwa mwaka wa fedha 2021/2022 wametambua jumla ya watu wazima wenye ulemavu 11,415 na watoto wenye ulemavu 3,298.

Aidha, amesema jumla ya watu wenye ulemavu 1,374 wamepewa huduma mbalimbali huduma zilizolenga kutoa hamasa kujiunga na vikundi ili waweze kufaidika na asilimia 2 ya mikopo inayotolewa na Halmashauri.

Mbali na huduma hizo huduma nyingine zilizotolewa kwa watu wenye ulemavu kwa mwaka 2021/2022 ni pamoja na wengine kupatiwa msaada wa kisaikolojia, vifaa saidizi pamoja na watu wenye ulemavu 190 kupewa misamaha ya matibabu au matibabu bila malipo.

Aidha, Bi. Jesca amebainisha huduma nyingine walizopewa watu wenye ulemavu kuwa ni pamoja na watu wenye ulemavu wa ngozi 237 kupewa huduma ya Afya ya ngozi na kufanyiwa uchunguzi zaidi kwa jitihada za Serikali ngazi ya Mkoa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Standing Voice, huku watu wenye ulemavu 347 wampewa huduma ya macho kwa kushirikiana na shirika la sight savers.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) Mkoa wa Morogoro Oscsar Changala ametoa onyo kwa vijana wanaowatumia watu wenye ulemavu kama kitega uchumi kwa kuzunguka nao mitaani kuomba fedha kuacha tabia hiyo mara moja na kwamba kuanzia sasa watakaokaidi onyo hilo watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

 “Kwa hiyo nawaeleza wazi kwa watu wanaofanya hiyo bishara kila mtu aanze kutafuta pori” ameonya Mwenyekiti huyo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.