Habari za Punde

Mhe Hemed akutana na kufanya mazungumzo na Kamishna wa jeshi la Polisi ZanzibarMakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amemtaka Kamishna wa jeshi la  Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa Askari  ili kukuza hadhi ya Jeshi hilo Nchini.

Mhe. Hemed ameeleza hayo Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad alipofika kujitambulisha baada ya kushika wadhifa huo.

Ameeleza kuwa Wananchi wa Zanzibar wanaamini Jeshi la Polisi kuwa ni sehemu salama kwao ambapo uwajibikaji wao utasaidia kuwaweka salama zaidi Raia na mali zao na hata wageni wanaokuja na kuondoka  Nchini.

Mhe. Hemed amemtaka  Kamishna Hamad  kusimamia na kuongeza mashirikiano baina ya Jeshi la Polisi na Vikosi vya Idara Maalum za SMZ hatua ambayo itasaidia kuondosha matendo maovu Nchini.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ni vyema jeshi hilo kusimamia Haki za Raia kwa kufuata Sheria zilizopo na kufanya kazi kwa Weledi bila ya Chuki na uonevu wa aina yoyote.

Aidha Mhe. Hemed amemueleza Kamishna huyo kuwa Serikali inaendelea kupigana na matendo maovu ikiwemo Janga la  Madawa ya kulevya na Vitendo vya udhalilishaji ambapo amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kufuatilia matukio hayo na kuwa karibu na Wananchi ili kesi hizo zisichukue muda mrefu kwenye upelelezi wake na hatimae kuweza kufikishwa kwenye Vyombo husika kwa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pamoja na mambo mengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza suala la Nidhamu Jeshini ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao na kumtaka Kamishna huyo kuacha muhali katika usimamizi wa Nidhamu kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi.

"Suala la Nidhamu nakuomba acha muhali kasimamie Jeshi la Polisi liwe na Nidhamu Wananchi wanaamini Polisi ndio sehemu salama kwao na ndio mana wanapokutwa na tatizo lolote hufika vituoni kwa ajili ya kuripoti kwa kuchukuliwa hatua zaidi"  amesema

Aidha amelitaka Jeshi hilo kuwa na Lugha nzuri wanapopokea malalamiko kutoka kwa Wanachi pindi wanapofika vituoni kutaka huduma au msaada wa kisheria ili kuendeleza Imani walionayo Wananchi kwa jeshi hilo.

Kwa upande wake Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad amemuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa ataendeleza mazuri yote  yaliyoachwa na waliomtangulia kwa lengo la kuiweka Zanzibar kuwa katika hali ya Usalama.

Aidha kamishna Hamad ameahidi mashirikiano baina yao na Vikosi vya Idara Maalum za SMZ kwa kuandaa Mafunzo mbali mbali  ya Pamoja ili kuongeza ufanisi katika kazi kwa kubadilishana mbinu za kiutendaji kwa Maslahi ya wazanzibari na Taifa kwa ujumla.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.