Habari za Punde

Mizengo Pinda awataka Viongozi wa CCM ngazi za chini kutafutia ufumbuzi changamoto

 Na Rahima Mohamed  Maelezo  20/8/2022

 

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Taifa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya nne  Mhe.  Mizengo Kayanza Peter Pinda amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kushuka katika ngazi za chini za chama ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wanachama wao.

 

Hayo ameyasema wakati alipofanya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo na utendaji kazi wa Tawi la Ijitimai Mwanakwere B. amesema viongozi wahakikishe wanashuka katika mashina na  matawi yao ili kubaini kasoro zilizopo na kuzitatua ili kuepuka udhoreteshaji na utendaji wa Chama hicho.

 

Waziri Mkuu huyo amesema  shina ni eneo la msingi sana katika siasa hivyo viongozi hao wanawajibu wa kuwathamini wanachama ambao wamewachagua ili kuunganisha nguvu za pamoja  kwa kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.

 

 

"Chama kinawahitaji wabunge na wawakilishi ambao hoja zao za msingi ni maendeleo ya wanachama wote ambao wapo katika ngazi ya shina ambapo Chama ndio kilipo" Alisema Waziri Mkuu huyo.

 

Aidha amesema siasa ni mahusiano ya wale waliowachagua katika kuleta maendeleo ya pamoja na ushindani wa Chama ni lazima na kuhakikisha unakwenda kutumika katika jumuiya za Chama hicho.

 

Vilevile amewataka kina mama kushirikiana pamoja ili kuhakikisha Chama hicho kinasonga mbele na kushika hatamu ya kuongoza nchi katika vipindi vyengine vijavyo.

 

Nae Naibu Katibu Mkuu  wa Chama cha Mapinduzi Taifa Zanzibar Abdalla Juma Mabodi amesema hali ya siasa inazidi kuimarika kutokana na kukuwa kwa kasi ya maendeleo kwa kusimamia halmashauri za wilaya na kuimarisha miradi ya maendeleo kwa utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.

 

Akisoma risala Khadija Ali makame  amesema wanampango wa kuhakikisha wanatafuta vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kujipatia mapato katika tawi lao, kutoa elimu ya itikadi na uenezi  kwa vijana pamoja kuimarisha ofisi za tawi hilo.

 

Aidha alisema jitihada zinaendelea za kuhamasisha vijana kujiunga katika Chama hicho ili kuongeza idadi ya wanachama na kuwa mfano wa kuigwa kwa matawi mengine ya CCM.

 

Alieleza kuwa hadi sasa tawi lao linakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo mashirikiano madogo kwa wagombea wao katika ngazi tofauti  jambo ambalo linakwamisha maendeleo  ya chama .

 

Alisema viongozi wakishachaguliwa hawatoi ushirikiano kwa viongozi wa matawi na kuonekana kwao huwa ni siku za uchaguzi zinapokaribia na kupelekea matawi mengi kudhoofika.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.