Habari za Punde

PSSSF INAINGIZA KARIBU SHILINGI BILIONI 200 KWENYE UCHUMI WA NCHIKILA MWEZI KAMA MALIPO YA PENSHENI NA MAFAO KWA WANACHAMA WAKE

 

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. James Mlowe (kulia) akiwa na Afisa Uhusiano Mkuu wa Mfuko huo Bw. Abdul Njaidi akifafanua jambo wakati alipotembelea chumba cha habari cha magazeti ya Chama Uhuru barabara ya Lumumba jijini Dar es Salaam.

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, DAR ES SALAAM

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unaingiza karibu bilioni 200 kila mwezi kwenye uchumi wa nchi kupitia malipo ya Mafao wanayolipa Wanachama wake, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko huo, Bw. James Mlowe amesema.

Bw. Mlowe ameyasema hayo kwa nyakati tofauti kwenye ziara yake ya kutembelea vyombo vya habari jijini Dar es Salaam iliyokamilika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akifafanua Bw. Mlowe amesema, PSSSF ina wastaafu 150,000 ambao hulipwa shilingi bilioni 60 kama malipo ya pensheni ya kila mwezi sambamba na kulipa zaidi ya shilingi bilioni 120 kila mwezi kama malipo ya Mafao mbalimbali kwa wanachama ambao bado hawajafikia umri wa kustaafu.

“Wastaafu na wanachama wetu wamesambaa kila kona ya nchi, wastaafu wengi pensheni yao siyo pesa ya kuwekeza ni ya matumizi ambayo inaenda kwa mama ntilie, na huduma mbalimbali za kijamii kwa hivyo inachachua uchumi, kwa hiyo bilioni 120 ukijumlisha na bilioni 60 ni bilioni 180 na wakati mwinhine hufikia shilingi bilioni 200 ambazo kila mwezi zinaenda kwenye uchumi wa nchi.” Alifafanua Bw. Mlowe.

HUDUMA ZA TEHAMA

Akizungumzia maboresho ya utoaji huduma kwa Wastaafu na Wanachama wa Mfuko huo Bw. Mlowe ambaye alifuatana na Afisa Uhusiano Mkuu Bw. Abdul Njaidi alisema, Mfuko umeimarisha mifumo yake ya TEHAMA ambapo Mwnachama na Mwajiri wanawasiliana na Mfuko kwa urahisi zaidi kwa njia ya kidijitali.

“Tuna huduma za PSSSF Kiganjani na huduma ya PSSSF Popote Ulipo Mtandaoni, lakini pia Wastaafu ambao wanatakiwa kujihakiki kila mwezi sasa wanajihakiki kupitia alama za vidole (Biometric).” Alifafanua.

MALIPO YA MALIMBIKIZO YA PENSHENI YA KILA MWEZI

Bw. Mlowe amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuuwezesha Mfuko kulipa Malimbikizo ya Pensheni ambapo ametoa cash bond ya shilingi trilioni 2.17 sawa na asilinmia 50% ya deni na tayari ameanza kuweka pesa hizo.

“Ni uamuzi wa kupongezwa ameufanya Mhe. Rais, kwani tayari tumelipa malimbikizo yanayofikia shilingi trilioni 1 na sasa tunaendelea na kulipa mafao mapya ya hivi sasa.” Alifafanua.

UWEKEZAJI.

Alisema Mfuko unawekeza kwa kufuata Sera ya Uwekezaji ya Mfuko, miongozo/kanuni za Benki Kuu ya Tanzania na Wizara yenye dhamana ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii.

“Tumewekeza kwenye Ardhi na Majengo, Dhamana za Serikali (Government Bonds), Amana za Mabenki, Hisa kwenye soko la Mitaji na Viwanda.”

Akifafanua kwanini Mfuko unawekeza, Bw. Mlowe alisema “Kulinda thamani ya michango ya wanachama, kuboresha mafao kwa wanachama na kuchangia juhudiza serikali kuinua uchumi wan chi.”


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.