Habari za Punde

UMOJA WA MATAIFA (UN) YAUNGA MKONO MAADHIMISHO YA SIKU YA AFYA YA AKILI

Mratibu wa   Umoja wa Mataifa (UN)  Zanzibar Dorothy Temu Usiri  akifanyiwa vipimo vya  sindikizo la damu (BP) wakati wa matembezi maalum ya kuhamasisha afya ya akili ikiwa ni shamrashamra kuelekea maadhimisho ya siku ya akili Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 10,hafla iliyofanyika Kinazini Mjini Zanzibar.
PICHA NA FAUZIA  MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR
Na Rahma Khamis Maelezo –Zanzibar                                                                                

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Salim Slim amesema ni vyema jamii kuweka mfumo madhubuti wa kufanya mazoezi ili kujikinga na maradhi mbalimbali ikiwemo magonjwa ya Afya ya Akili.

Ushauri huo ameutoa huko Kinazini mara baada ya kumaliza matembezi maalum ya kuunga mkono siku ya Afya ya Akili Duniani yanayofanyika kila mwaka  ifikapo  oktoba 10 ikiwa ni shamrashamra kuelekea siku hiyo.

Amesema kuwa ili mtu awe na Afya nzuri lazima awe na mfumo mzuri wa kufanya mazoezi kwani bila ya kufanya hivyo,mfumo wa damu utakua mzito na kupelekea kupata madhara ya kupoteza kumbukumbu.

“Ikiwa hatufanyi mazoezi katika maisha yetu angalau kwa dakika 20 kwa kila siku damu itaganda na kuweza kushindwa kufanya kazi vizuri baada ya hapo kinachofuata ni maradhi kutokana na kuganda kwa damu katika miili yetu”,alisema Dkt Slim.

Aidha amefahamisha kuwa mfumo wa kufanya kazi kwa kujiacha unaathiri mwenendo wa afya katika jamii,hivyo kila mtu aangalie hali ya maisha kwa kufanya mazoezi kwa mujibu wa hali ya Afya aliyonayo.

“Wafanya kazi wengi siku hizi wamejiacha sana kwani kila mtu anatumia usafiri sehemu ndogo usafiri uwe wa binafsi au daladala hii ni sababu kubwa inayopelekea watu kupata maradhi,”alisema Dokt huyo.

Hata hivyo Dokt Slim amewashukuru wadau wa afya kutoka ( UN) kwa kuleta wazo la kuanzisha mazoezi kwani kufanya hivyo kunaboresha afya ya binadamu.

Nae Daktari dhamana wa Kitengo cha Magonjwa ya Akili Hospitali ya Kidongochekundu Khadija Abdulrahman amesema kuwa mazoezi yana uhusiano mkubwa na afya ya Akili katika maisha ya kila siku.

Amefahamisha kuwa watu wengi katika jamii hasa wafanyakazi hukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi, kati yao wanakua na msongo wa mawazo hivyo kufanya mazoezi kutawasaidia kuondosha vichochezi vya magonjwa ya Akili na mengine ikiwemo kisukari na shindikizo la damu.

Aidha ameisa jamii kutobweteka na kujitahidi kubadilika kwa kufanya mazoezi ili kupunguza ongezeko la maradhi ya Afya nchini.

 Nao wadau wa Afya kutoka Umoja wa Mataifa (UN) wamesema kuwa wameamua kufanya hivyo ili kuhamasisha jamii kushiriki katika kufanya mazoezi ili kuimarisha Afya ya Akili na kujikinga na maradhi mbalimbali.

Aidha wamefahamisha kuwa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani mtu mmoja  kati ya wanne  Ulimwenguni  kote  anaishi na tatizo la Afya ya Akili , hivyo ni wajibu wakila mmoja kufanya mazoezi ili kujiepusha na tatizo hilo.

Matembezi ya kilo mita tano  yaliyoambatana na mazoezi ya viungo na upimaji wa Afya yameandaliwa na wadau wa Afya Zanzibar ikiwemo WHO, UNICEF na UNDP ambapo matembezi hayo yameanzia Kinazini kuelekea Malindi Vuga,Mnzimmoja Michenzani na kurejea Kinazini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.