Habari za Punde

Uchumi wa Zanzibar Unaendelea Kukua Mbali na Changamoto Zinazoikabili Dunia - Dk.Hussein

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waandishi wa Habari na Wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali, wakati wa mkutano wake na Waandishi kila mwisho wa mwezi  uliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 5-11-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua, mbali na changamoto mbali mbali zinazoikabili Dunia.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na waandishi wa Vyombo mbali mbali vya habari nchini, ikiwa ni muendelezo wa utaratibu aliojipangia wa kukutana na waandishi  wa habari kila mwisho  mwezi na kujibu maswali mbali mbali,  tukio linalokwenda sambamba na miaka miwili ya Uongozi wake.

Ameeleza kuwa pamoja na changamoto za kuwepo kwa Ugonjwa wa UVICO 19 pamoja na Vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukrane, Uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua, hususan kupitia sekta ya Utalii na kusema kumekuwepo  ongezeko kubwa la watalii wanaozuru nchini.

Alisema kukua huko kwa uchumi pia kumechangiwa na kuongezeka kwa makusanyo katika Uwanja wa Ndege wa  Abeid Amani Karume, akibainisha taasisi hiyo imekusanya zaidi ya shilingi  Bilioni 6.7 katika kipindi cha kuanzia mwezi wa Julai hadi Septemba, 2022, sambamba na Bodi ya Mapato Zanzibar  (ZRB) na Shirika la Bandari ambazo vimekuwa  katika kiwango bora cha kukusanya kodi.

Alisema mapato katika Shirika la Idara ya  Bandari yameongezeka kutokana na kuwepo mfumo bora wa makusanyo; hata hivyo akaelezea tatizo kubwa linaloikabili Bandari hiyo ya Malindi kuwa ni kukosekana  ufanisi kwa vile imekuwa na Gati moja na hivyo akabainisha azma ya Serikali ya kumpata mwekezaji ili kuiendesha kwa ufanisi.

Dk. Mwinyi alisema Sekta ya Uwekezaji nayo imepata mafanikio makubwa, ambapo Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imefanikiwa kusajili miradi 181 yenye thamani ya zaidi ya Dola Bilioni tatu, huku wastani wa wananchi 11,289 wakitarajiwa kupata ajira.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema Serikali inakusudia kufanikisha miradi mbali mbali katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, ukiwemo mradi wa Ujenzi wa Bandari Mangapwani, Ujenzi wa barabara kuu  Unguja na Pemba, Ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Karume Pemba pamoja na ujenzi wa barabara za ndani utakaonza mwezi Disemba , 2022 utakaohusisha ujenzi wa ‘Fly over’ katika maeneo ya Mwanakwerekwe na Round About ya Amani.

Alisema Serikali inatambua kuwepo kwa mfumko wa bei za bidhaa na kuathiri maisha ya wananchi wa kawaida, na kubainisha kuwa jambo hilo linaikabili dunia nzima ikiwemo nchi zilizoendelea.

Alisema  hali hiyo inatokana na kupanda kwa bei za chakula pamoja na mafuta, kunakotokana na majanga ya Kilimwengu na akatumia fursa hiyo kuelezea  baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kupunguza makali , ikiwemo kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma, kuangalia Pencheni za wastaafu, kuweka fidia katika mafuta pamoja na kutoa huduma bora Bandarini ili kuharakisha utoaji wa bidhaa.

Dk. Mwinyi aliwatoa khofu wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ya kupoteza ajira zao kwa madai ya kuwepo kwa Kampuni ya DNATA.

Alisema Kampuni ya DNATA  inashughulikia masuala ya mizigo katika jengo la Terminal 111 pekee na kubainisha azma ya Serikali ya kuipa kazi kampuni hiyo kuwa inalenga kupata kampuni yenye ujuzi  na kutoa huduma bora.

Alisema Kampuni hiyo imeleta ufanisi mkubwa katika kuhudumia uwanja huo, kiasi ambacho Uwanja wa huo umekuwa ukiongoza kati ya viwanja vyote viliopo nchini kwa kuingiza wageni wengi.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali inatafuta mwekezaji  kwa ajili ya kukiendeleza  Kiwanda cha Maziwa cha Azam kiliopo Fumba kinachomilikiwa na Said Salim Bakhressa  baada ya kusimamisha uzalishaji na kufungwa, ikiwa ni hatua ya kunusuru bidhaa za wazalishaji wa ndani.

Vile vile, alisema Serikali inaangalia namna ya kubadili mfumo wa adhabu kwa makosa ya usalama barabarani ya papo kwa papo, kwa kigezo cha kuwa mfumo uliopo hivi sasa sio bora.

Akigusia juu ya ziara yake ya hivi karibuni nchini Oman, Dk. Mwinyi alisema Serikali inakusudia kuwarejeshea nyumba zao wananchi wanaoishi Oman ambao waliishi Zanzibar na hatimae kuondoka, hali ya kuwa nyumba hizo hazikutaifishwa na Serikali; pale watakapothitisha kwa kuwa na nyaraka halali.

Mapema, Dk. Mwinyi aliwashukuru wananchi kwa kuendeleeza amani, umoja, na mshikamano, jambo lililoiwezesha serikali kuendeleeza malengo yake ya maendeleo.    

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.