Habari za Punde

AIRTEL TANZANIA YAIUNGA MKONO BODI YA FILAMU TANZANIA KUFANIKISHA TAMASHA LA TUZO ZA FILAMU TANZANIA 2022

Meneja wa Airtel Kanda ya Kaskazini Bi. Monica Ernest (mwenye gauni jeupe) akikabidhi Tuzo ya Filamu bora - Mapambo athari kwa mshindi wa kipengele hicho Bw. Jafari Athumani kupitia Filamu ya Mateka katika Tuzo za Filamu Tanzania 2022 zilizofanyika Tarehe 17 Disemba, 2022 jijini Arusha - AICC.

Kampuni ya Airtel Tanzania inayotoa huduma za mawasiliano ya simu imekuwa sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua Sekta ya Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini ambapo ilikuwa moja ya Makampuni yaliyodhamini Tamasha la Tuzo za Filamu Tanzania linaloratibiwa na Serikali kupitia Taasisi yakeya Bodi ya Filamu Tanzania.

Kilele cha Tamasha la Tuzo za Filamu Tanzania 2022 kimefanyika Tarehe 17
Disemba, 2022 jijini Arusha katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha - AICC,
ni Tamasha la pili kuratibiwa na Serikali kupitia Bodi ya Filamu, ambapo limetoa
jumla ya washindi wa Tuzo 32 kutoka katika Filamu 59 zilizofanikiwa kuingia kwenye
kinyang’anyiro. Aidha, Tamasha la kwanza lilifanyika mwaka 2021 jijini Mbeya.
Akizungumza katika usiku wa kilele hicho Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo
Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye pia alikuwa mgeni rasmi alisisitiza kuwa,
dhamira ya Serikali ni kuendelea kuwekeza katika kuwasaidia Wasanii ili waweze
kufanya vizuri, ambapo tayari Serikali imeanzisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa
ambao utaanza kutoa mikopo kwa Wasanii kuanzia jumatano ya Disemba 21, 2022.
“Sekta ya Filamu inakua, na inaendelea kutoa ajira kwa vijana wengi pamoja na
kuchangia katika Pato la Taifa, hivyo sisi kama Serikali tutaendelea kuweka nguvu
katika Sekta hiyo" amesema Mhe. Mchengerwa.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo alisema nia ya Serikali ya kuanzisha Programu hii ya kutunuku wadau wake Tuzo ni:
a. “kutambua mchango wa wanatasnia ya Filamu,
b. kutambua vipaji vilivyojificha vya wanatasnia ya Filamu,
c. kuongeza hamasa kwa wanatasnia ya kuzalisha kazi nyingi zaidi za Filamu,
d. kuongeza hamasa kwa wanatasnia ya Filamu kuzalisha kazi bora za Filamu
na hatimaye kuwa na ushindani mkubwa ndani na nje ya nchi, na
e. kusisimua fursa za uwekezaji katika Sekta ya Filamu nchini”.

Aidha, kupitia zoezi hili zima la Tamasha la Tuzo hapa nchini, Serikali itapata
Taswira itakayoweza kusaidia kuandaa program maalumu za kuwajengea uwezo
watendaji wetu wa filamu kulingana na mahitaji yao halisi.

Kampuni ya Airtel Tanzania ilikuwa moja ya Makampuni yaliyodhamini Tamasha la
Tuzo za Filamu 2022 na iliwakilishwa na Meneja wa Kanda ya Kaskazini Bi. Monica
Ernest ambapo alipata nafasi ya kukabidhi Tuzo ya Filamu bora - Mapambo Athari
kwa mshindi wa kipengele hicho Bw. Jafari Athumani kupitia Filamu ya Mateka.
Aidha, Meneja huyo alisema kuwa Kampuni ya Airtel Tanzania imekuwa mstari wa
mbele katika kusaidia Sekta za Sanaa hususani Filamu, ambapo imeanzisha
Televisheni Mtandao (Airtel Tv) yenye lengo la kusaidia Wasanii wa Filamu nchini
kuuza kazi zao kupitia mtandao huo, ambapo wasanii hao wanapata fedha kutokana
na wingi wa watazamaji ndani na nje ya nchini hivyo kuongeza pato la Wasanii
mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla kupitia Kodi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.