Habari za Punde

Utekelezaji wa Mipango ya Serikali ya Kukifungua kisiwa cha Pemba katika fursa mbali mbali za kiuchumi na kimaendeleo

 Na.Mwandishi wa OMKR.

Imeelezwa kwamba kuanza kwa hatua za ujenzi Bandari Rasmi katika Kijiji cha Shumba mjini Wilaya ya Micheweni Kisiwani Pemba ni utekelezaji wa mipango ya serikali ya Kukifungua kisiwa cha Pemba katika fursa mbali mbali za kiuchumi na kimaendeleo.

Hayo yameelezwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, alipotembelea kukagua na kuona maendeleo ya Ujenzi wa Bandari rasmi huko katika kijiji hicho kilichopo wilaya ya Micheweni Pemba.

Amesema kwamba Zanzibar imedhamiria kuona kwamba kisiwa cha Pemba kinafunguka kiuchumi kwa kuwepo na kuendelezwa fursa mbali mbali za kibiashara zitakazochangia pato la wananchi na kuchangia kukuza uchumi wa Zanzibar.

Amesema kwamba bandari hiyo itakapokamilika mbali na kuwasaidia sana wakaazi wa kisiwa cha Pemba hasa wa Kijiji cha Shumbamjini lakini itasaidia  sana kuimarisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Zanzibar.

Mhe. Othman amesema kutokana na umuhimu wa Bandari kibiashara na kiuchumi tayari baadhi ya wafanyabiashara kutoka Kenya wameanza kufika Kisiwani humo kuona fursa za kibiashara zitakazopatikana kupitia ujenzi huo wa bandari itakapokamilika mwazi Oktoba mwakani.

Ameitaka Kampuni iliyopewa kazi hiyo kuhakikisha kwamba wanakamilisha ujenzi huo wa Bandari kama ilivyokubali itakapo fika mwezi wa Oktoba  mwaka ujao.

Aidha amewataka wananchi wote hasa wa eneo hilo kuhakikisha kwamba wanatoa mashirikiano ya kutosha na Mkandarasi anayejenga Banadari hiyo ili kazi iliyokusudiwa ikamilike kwa wakati na tija kwa wananchi na Zanzibar kwa ujumla iweze kupatikana.

Mapema Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirika la Bandari Zanzibar Ndugu Salum Udi amemueleza Mhe.Othman Masoud kwamba shughuli zinazoendelea katika ujenzi huo ni kazi za kitaalamu ambazo zimekamilika na kwamba michoro ya bandari hiyo ipo tayari na itapeleka kwa wadau kwa ajili ya kufanyiwa mapitio ili kazi rasmi iweze kuanza.

Alifahamisha kwamba miongoni mwa kazi nyengine zilizofanyika ni pamoja  uchuguzi wa udongo , kupima kupima kina chama maji na kwamba imebaini kwamba ujenzi huo utafanyika kwa njia ya tuta  badala ya mfumo mwengine wa ujenzi wa bandari.

Amesema ujenzi wa bandari hiyo yenye urefu wa   mita 40 kwa ishirini itakapokamilika itakuwa na uwezo wa  kutia ndanga meli zenye ujazo wa mizigo ipatayo tani 2000 na inatarajiwa kukamilika Oktoba 2023.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mabarouk Khatib , amemueleza Mhe. Makamu kwamba viongozi wa mkoa huo kwa kushirikiana na wananchi na wadau ,mbali mbali watahakikisha kwamba kazi hiyo inakamilika kwa wakati ulipangwa na wananchi waweze kunufaika.

Mapema Mhe. Makamu alijumuika na waumini wa Dini ya Kiislamu Katika  ibada ya swala ya ijumaa huko masjid Likadim Shumba mjini ambapo aliwataka waumini hao kuendelea na juhudi ya malezi bora kwa vijana ili kuzuia upotevu wa uadilifu na maadili uliopo hivi sasa ndani ya jamii.

Amesema kwamba visiwa vya Zanzibar hivi sasa vimekumbwa na janga kubwa la ukosefu wa uadilifu na hivyo kuwafanya vijana kutamani kupata kwa njia yoyete hata zikiwa ni za dhulma.

Mapema Khatib wa swala ya Ijumaa katika msikiti huo Sheikh  Haji Masoud Kombo amewakumbusha waislamu kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo maamuru ya mwenyezimungu kwa kuwa huko ndio kumcha mungu Muumba.

 Imetolewa na ofisiu ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Kupitia Kitengo chake cha Habari Leo tarehe 02.12.2022.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.